December 26, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Majaliwa:ASAS zalisheni maziwa kwa wingi

Na Doreen Aloyce,TimesMajira Online,Dodoma

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amewataka wamiliki wa kampuni ya ASAS,inayozalisha maziwa kuendelea kuhudumia jamii hususani kuzalisha maziwa kwa wingi na yenye ubora.

Kauli hiyo ameitoa katika viwanja vya Bunge jijini Dodoma wakati alipokuwa akitembelea maonesho ya wafugaji na wavuvi kwa ajili ya kuonesha protini yaliyoandaliwa na Wizara ya Mifugo na uvuvi .

Waziri Mkuu ametumia nafasi hiyo kuipongeza kampuni hiyo na kuitaka iendelee kuhudumia jamii kwa kuzalisha maziwa mengi na bora ambayo watayasafirisha ndani na nje ya nchi.

Ametumia fursa hiyo kumuagiza Waziri wa Mifugo na Uvuvi Abdallah Ulega,aangalie namna ya kuweza kuzisaidia kampuni kama ASAS na nyingine kwani zinafanya kazi kubwa ya kuzalisha bidhaa ambazo zinaweza kuuzika hata nje ya nchi.

Wizara imeonesha mikakati ya namna inavyoboresha sekta ya mifugo na uvuvi huku serikali inayoongozwa na Rais Samia iliridhia kutenga fedha ya kutosha kwa sekta mbili na tumeweza kupata mafanikio na tumeona changamoto zilizojitokeza huko nyuma.

“Tukiwa tunaendelea na mawasilisho yetu ipo fursa ya Wabunge kuchangia kwa sekta hizi mbili za mifugo na uvuvi kwa kuchangia maoni ya wananchi wanavyoeleza na pia wanatoa muelekeo wa nini Wizara ifanye,”amesema Waziri Mkuu huyo.

Kwa upande wake Waziri wa Mifugo na uvuvi Abdallah Ulega amesema kuwa watahakikisha wanashirikiana na ASAS wawe wanapata maziwa ya kutosha ili kupunguza uaguzaji wa maziwa ya unga.

“Watanzania tumepiga hatua kwani mifugo na uvuvi ni utajiri unaweza kuinua pato la nchi na uchumi wa mtu mmoja mmoja,tunakila sababu ya kujivunia hili na kuendelea kuongeza kasi katika kuitunza mifugo yetu ili tuendeleze kuzalisha mifugo mingi na bora zaidi,”amesema Ulega.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa ASAS Fuad Asas amesema Wizara ya Mifugo na Uvuvi imewapa ushirikiano hasa katika kusaidia uzalishaji wa maziwa na upatikanaji wa ng’ombe bora kwa kuwaunganisha na wafugaji wa ng’ombe bora.

Amesema kuwa ipo haja ya Wizara ya Mifugo kuhakikisha inatoa elimu ya kutosha kwa wafugaji ili kuepusha matatizo yatokanayo na maziwa kutoka kwa ng’ombe kwenda Kwa mlaji.

Balozi wa ASAS Lucas Mhuvile alimaarufu JOTIamesama kuwa lengo kuu ni kuhakikisha jamii kwa ujumla inapata elimu ikiwa sambamba na kutumia maziwa kwa wingi ili kuimarisha na kuboresha afya zao.

Maonesho hayo yamehudhuriwa na wabunge mbalimbali kwa lengo la kujifunza na kujionea bidhaa zinazozalishwa kutokana na mifugo .