March 29, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Majaliwa: Zoezi la Uwekaji Alama za Mipaka Pori Tengefu Loliondo limekamilika

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online, Loliondo.

Waziri Mkuu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa leo ametangaza kukamilika kwa zoezi la uwekaji wa alama za mipaka katika Pori Tengefu la Loliondo, Ngorongoro mkoani Arusha.

Majaliwa amepongeza washiriki wote wa zoezi hilo na kuwataka wananchi kuepuka taarifa hasi za upotoshwaji kuhusu eneo hilo. Amesema kuwa zoezi hilo limefanyika kwa nia njema ya kuhifadhi eneo hilo na kuwa hakuna wananchi wowote waliohamishwa katika eneo hilo.

“Eneo hili ni muhimu kwa kuwa na vyanzo vya maji na mazalia ya nyumbu ambayo ni muhimu kwa uwepo wa maeneo ya hifadhi za Serengeti na Ngorongoro”, alisema Majaliwa.

Waziri Mkuu amebainisha kuwa eneo hili litaendelea kulindwa kwa wakati wote ili kuhifadhi eneo hilo ambalo ni muhimu kwa uhifadhi kitaifa na kimataifa.

Kwa upande wake, Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Pindi Chana alisema kuwa wizara na taasisi zilizo chini yake wataendelea kusimamia maeneo yote ya uhifadhi kwa niaba ya wananchi.

Mapema akimkaribisha Waziri Mkuu, Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. John Mongella alisema kuwa zoezi hilo limekamilika kwa wakati na kwa mafanikio makubwa.

Mongella ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama wa Mkoa wa Arusha na msimamizi wa zoezi hilo, alisema kuwa wameamua kumpa heshima askari Garlus Mwita aliyepoteza maisha akiwa katika zoezi hilo kwa kujenga mnara katika kigingi namba moja kama alama ya kumuenzi shujaa huyo.