December 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Majaliwa: Utekelezaji wa mipango ya kilimo upewe kipaumbele

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Onine

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameiagiza Wizara ya Fedha na Mipango ihakikishe inaweka kipaumbele cha utekelezaji wa Mipango ya Maendeleo ya Kilimo ya Wilaya (DADPs) ikiwa ni pamoja na kutafuta fedha zitakazowezesha utekelezaji wake.

Ametoa agizo hilo leo (Jumatano, Machi 2, 2022) wakati akizindua Mipango ya Maendeleo ya Kilimo ya Wilaya (DADPs) katika ukumbi wa Chuo cha Mipango, jijini Dodoma. Pia amezitaka taasisi za fedha zijipange kutambua hati miliki za ardhi za wakulima kama dhamana ya kupata mikopo.

Kadhalika, Mheshimiwa Majaliwa amezielekeza Halmashauri zote nchini zihakikishe zinatenga fedha kutoka katika mapato yake ya ndani kwa ajili ya utekelezaji wa Mipango ya Maendeleo ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi ya Wilaya.

“Kwa kuwa asilimia kubwa ya rasilimali za utekelezaji wa ASDP II zinalenga kuelekezwa katika Mamlaka ya Serikali za Mitaa, Wakuu wa Mikoa, Makatibu Tawala wa Mikoa na Wakurugenzi Watendaji wa Mamlaka za Serikali za Mitaa waongeze usimamizi wa fedha na rasilimali.”

Waziri Mkuu amewaagiza Wakuu wa Mikoa, Makatibu Tawala wa Mikoa na Wakurugenzi Watendaji wa Mamlaka za Serikali za Mitaa wahakikishe wanawajenga uwezo wa kusimamia utekelezaji wa miradi katika ngazi mbalimbali na kubuni vyanzo vingine vya kupata fedha za kuendeleza miradi ya kuendeleza kilimo.

Mheshimiwa Majaliwa ameiagiza Ofisi ya Rais – TAMISEMI kupitia Halmashauri zote nchini ziendelee kutenga maeneo ili kuwawezesha wananchi kufanya shughuli za kilimo na shughuli nyingine kama vile ufugaji.

“Ofisi ya Rais TAMISEMI na Wizara ya Kilimo ziandae na kusimamia utekelezaji wa mkakati madhubuti wa kusimamia utendaji kazi wa maafisa ugani ili kuongeza uzalishaji na tija katika kilimo. Maafisa Ugani wasimamiwe kikamilifu ili kuimarisha huduma za ugani kwa wakulima.”

Kwa upande wake, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Innocent Bashungwa amesema watashirikiana na Wizara za Sekta ya Kilimo kutekeleza Mipango ya Maendeleo ya Kilimo ya Wilaya kwa kutafuta rasilimali fedha na kusimamia kikamilifu matumizi na utekelezaji wake pamoja na kuimarisha mifumo ya kiteknolojia ya habari na mawasiliano katika sekta ya kilimo (TEHAMA) na kuwezesha upatikanaji wa huduma za kifedha.