Na Yusuph Mussa, Timesmajira Online,Tanga
WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amesema serikali imeweka mikakati na inaboresha mazingira ya Watanzania na kampuni za kitanzania kunufaika na fursa mbalimbali nchini ikiwemo kushiriki katika miradi ya kimkakati na uwekezaji unaofanyika hapa nchini.
Lengo ni kuhakikisha kuwa fursa zote zilizopo zinatumiwa ipasavyo na Watanzania hususani wanawake,vijana na watu wenye ulemavu.
“Ikumbukwe kwamba wanawake ni jeshi kubwa, hivyo kwa ukubwa huo huo serikali ina matarajio makubwa kuweza kuchangamkia fursa zote zinazojitokeza katika miradi inayoendelea kutekelezwa hapa nchini,”.
Hayo yamebainishwa kwenye hotuba ya Waziri Mkuu iliyosomwa na Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. Dorothy Gwajima,Agosti 24, 2023 wakati anafungua kongamano la Wanawake na Manunuzi ya Umma na Fursa za Biashara katika Bomba la Mafuta kutoka Uganda hadi Tanzania, ambayo imeandaliwa na taasisi ya Ng’arisha Maisha Foundation (NMF) chini ya Mkurugenzi Mtendaji ambaye pia ni Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Tanga Mhandisi Mwanaisha Ulenge linalofanyika jijini Tanga kwa siku mbili.
“Nitumie fursa hii kumpongeza Mhandisi Mwanaisha Ulenge (Mb.),Mkurugenzi Mtendaji na Mwanzilishi wa Ng’arisha Maisha Foundation kwa kutekeleza kwa vitendo maono ya Rais Dkt Samia Suluhu Hassan,kuhakikisha Watanzania hususani wanawake wanakuwa sehemu ya maendeleo ya nchi,”amesema Majaliwa na kuongeza kuwa
“Ninafahamu kwamba wengi wenu kama watu binafsi lakini pia kama sehemu ya sekta binafsi nchini hapa , mnakabiliwa na changamoto mbalimbali ambazo kwenye kushiriki katika miradi mikubwa ya kimkakati ikiwemo ukosefu wa mitaji, kutokukidhi vigezo na viwango vya kimataifa, ukosefu wa taarifa kamili, sahihi na kwa wakati kuhusu mahitaji ya wakandarasi na wawekezaji pamoja na ukosefu wa ujuzi na uzoefu katika kusimamia fedha na miradi mikubwa,”.
Pia amesema serikali kwa kushirikiana na wadau wengine itaendelea kufanyia kazi changamoto hizo ili kuhakikisha kuwa Watanzania na hususani wanawake wanashiriki kwa wingi katika utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati ama moja kwa moja au kupitia utoaji wa huduma saidizi kwenye utekelezaji wa miradi hiyo.
Awali Mkurugenzi Mtendaji wa NMF Mhandisi Ulenge ameeleza kuwa taasisi hiyo iliyoanzishwa mwaka 2021 kwa mujibu ya sheria ya mashirika yasiyo ya kiserikali na kusajiliwa kwa Na. 00NGO/R/2341 huku kongamano hilo limekwenda sambamba na uzinduzi na mafunzo yatayosaidia kuongeza ushiriki wa wanawake katika manunuzi ya umma na pia kuongeza ushiriki wa wazawa katika mradi wa bomba la mafuta.
“Taasisi haitasita kuleta mafunzo ya namna hii Ruangwa na mikoa mengine ya Tanzania, leo tumefanya Tanga kwa kuwa sadaka nzuri niile ianziayo nyumbani,NMF inatambua juhudi kubwa zinazofanywa na Serikali kupitia sekta mbalimbali ili kumletea Mtanzania maendeleo endelevu na tunapenda kumpongeza sana Rais wetu kwa uwezo mkubwa aliouonesha katika kutekeleza malengo endelevu ya dunia ikiwemo usawa wa jinsia,”ameeleza.
Pia ameeleza kuwa taasisi hiyo imedhamiria kuunga mkono jitihada za serikali katika kutatua changamoto za makundi maalumu wakiwemo wanawake ili kuyafanya maendeleo ya kiuchumi na kijamii kuwa endelevu na kuhakikisha hakuna anae achwa nyuma katika maendeleo endelevu.
Aidha ameeleza kuwa katika kutekeleza malengo iliyojiwekea ni kuhakikisha fursa mbalimbali zinazotokana na utekelezaji wa mipango ya Serikali zinawafikia walengwa wakiwemo wanawake.
“Nimekuwa nikifanya mambo kadhaa kuhakikisha utekelezaji wa mipango ya Serikali inawafikia walengwa na wanawake walionipa dhamana,mfano hai ni kuwa taasisi yetu ikayabeba maono ya serikali ambayo imekuwa ikihimiza kilimo cha alzeti ili kuondokana na uhaba wa mafuta kwa kuwafikishia mbegu bora za alizeti na mahindi kwa wanawake katika wilaya sita kwa sababu asilimia 70 ya wakulima vijijini ni wanawake,”amesema Mhandisi Ulenge.
Mhandisi Ulenga ameeleza kuwa kata zaidi ya 150 za Mkoa wa Tanga zimelima alzeti walau hekali mbili kwa mbegu bora na kata takribani 100 zimelima mahindi kwa mbegu bora ikiwa ni kuunga mkono usambazaji wa mbegu bora za kilimo na kupelekea wananchi kuachana na kilimo cha asili na kupata tija zaidi kwenye kilimo huku matarajio ni kuendelea kugawa mbegu bora kwa awamu ya pili ili kuhakikisha mbegu hizo zinaenea mkoa mzima.
Mhandisi Ulenge amesema, ili walime kilimo chenye tija zaidi wanamuomba Waziri Mkuu kupitia Wizara ya Kilimo na Baraza la Uwezashaji wananchi kiuchumi na wadau mbalimbali, wanawake wa Tanga wawezeshwe kwa kuchimbiwa visima na miundombinu ya umwagiliaji kwenye wilaya zao ili wasitegemee mvua.
Kongamano hilo limewashirikisha wanawake takribani 1,000 kutoka majimbo 12 ya Mkoa wa Tanga, halmashauri zote 11, wilaya nane za mkoa huo wakiwemo Madiwani wa Viti Maalumu.
More Stories
FDH yaanza kutekeleza mradi wa kuwajengea uwezo wanawake wenye ulemavu
Airtel yatoa zawadi kwa wateja wake
Mpango ashiriki mazishi ya Mama yake Serukamba