May 17, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Majaliwa: Rais Dkt. Samia anathamini sekta binafsi

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira,Online,

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kuthamini na kutambua mchango wa sekta binafsi katika kuimarisha ustawi wa jamii ya Watanzania.

Ameyasema hayo Jumapili, Februari 18, 2024 alipomuwakilisha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kufungua hospitali ya Saifee Tanzania jijini Dar es Salaam. Amesema sekta binafsi zimekuwa zikiunga mkono jitihada za Serikali katika kutoa huduma mbalimbali kwa wananchi.

Waziri Mkuu amesema mchango wa sekta binafsi katika eneo la kutoa huduma kwa wananchi ni mkubwa na unadhihirika kupitia huduma mbalimbali wanazozitoa ambazo ni pamoja na huduma za afya, elimu, mawasiliano na maji.

Amesema kwa upande wa sekta ya Afya, Serikali inatekeleza kwa vitendo Sera ya Ubia kwa kufanya kazi pamoja na baadhi ya vituo vya kutolea huduma ya afya vinavyomilikiwa na sekta binafsi.

Pia, Waziri Mkuu amesema amefarijika na huduma zinazotolewa na hospitali hiyo zikiwemo za upasuaji wa moyo, mgongo, ubongo kwa kutumia teknolojia za kisasa za kitabibu na pia kuweka vipandikizi (implants) kwenye matibabu ya mifupa.

“Ni matumaini yangu kuwa Taasisi ya Saifee itasaidia kupunguza rufaa za wagonjwa kwenda nje ya nchi na kupunguza gharama kwa wananchi na Serikali kwa ujumla, hivyo uwekezaji huu una manufaa makubwa sana kwa Taifa.”

Amesema Hospitali ya Saifee na nyingine kama hizo nchini, ni nyenzo muhimu katika kuiharakisha Tanzania kuelekea kuwa kitovu cha utalii Tiba katika Ukanda wa Afrika Mashariki, Kati na Kusini pamoja na Visiwa vya Bahari ya Hindi.

Kwa upande wake, Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu amesema wataendelea kuwa wabunifu na kushirikiana na sekta binafsi katika kuboresha huduma za afya kwa Watanzania. Tanzania kuna vituo zaidi ya 12,000 vya kutolea huduma za afya kati yake asilimia 60 ni vya Serikali na asilimia 40 vinamilikiwa na sekta binafsi.

Pia, Waziri Ummy ametumia fursa hiyo kutoa wito kwa Watanzania wazingatie ulaji unaofaa pamoja na kufanya mazoezi ili kuepukana na magonjwa yasiyoambukiza yakiwemo ya moyo na kisukari.

Awali, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Hospitali ya Saifee, Murtaza Alibhai alisema hospitali yao ni taasisi ya kwanza kutoa huduma ya upasuaji wa moyo bila kufungua kifua kwa upande wa hospitali binafsi nchini.

Alisema lengo la hospitali hiyo ni kutoa huduma bora za matibabu kwa gharama nafuu kwa wananchi. Hospitali hiyo ina jumla ya wafanyakazi 370 kati yao Wwatanzania ni 350 na wageni 20.

Mwenyekiti huyo wa Bodi alisema mpango wa hospitali hiyo kwa siku za hivi karibuni ni kuanza upandikizaji wa figo. Alisema hospitali hiyo mbali na kupokea wagonjwa wa ndani ya nchi, pia wamekuwa wakipokea wagonjwa kutoka nchi za Kenya, Malawi na Visiwa vya Komoro.