Na Tawani Salum – Mahakama
JAJI wa Mahakama ya Rufani Tanzania, Dkt. Jaji Gerald Ndika, amewataka Majaji na Mahakimu kutafsiri sheria zinaohusu masuala ya wanawake na watoto ili ziendane na mazingira ya sasa katika kuendesha mashauri yanayohusu masuala la unyanyasaji na ukatili wa kijinsia.
Akizunguza wakati wa Mafunzo ya Haki za Binadamu na Unyanyasaji hususani kwa wanawake na watoto, yanayofanyika Mjini Bagamoyo Mkoa wa Pwani, Jaji Ndika amesema sheria zilizopo kwa kiwango kikubwa zinajitosheleza kinachotakiwa jinsi ya kuzitafsiri, hivyo Majaji na Mahakimu watoe tafsiri ambayo inaendana na mazingira ya matukio yalivyo.
Jaji Ndika ambaye ni mshiriki katika mafunzo hayo, amesema kuwa moja ya faida zake ni kuwaandaa wawezeshaji katika eneo hilo ili kusaidia Mahakama ya Tanzania, Majaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania, Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mahakimu,watumishi mbalimbali ambao wanatoa maamuzi juu ya vitendo vya unyanyasaji na ukatili wa wanawake na watoto kuwa na umahiri.
“Matukio haya yanatokana na mambo mengi ikiwemo mila potofu pamoja na uelewa wao mdogo, wanaona kumpiga mke au mtoto ni jambo la kawaida na ana haki ya kufanya hivyo.
Lakini mafunzo haya yatasaidia kupata wakufunzi ambao wataenda kuwapa wengine elimu juu ya kuweza kupambana na ukatili na unyanyasaji wa wanawake na watoto,” alisisitiza Jaji Ndika.
Ameongeza kwamba mafunzo hayo ni ya mara ya tatu kufanyika yakiwa ni endelevu katika kutoa elimu hiyo.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha Majaji na Mahakimu Wanawake Tanzania (TAWJA) ambaye ni Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Joaquine De Mello akifungua rasmi mafunzo hayo, amesema kuwa yana lengo la kuwawezesha watoa maamuzi kuwa na uweledi zaidi wa kutoa haki na pia kuielimisha jamii juu ya haki zao za msingi na tatizo la unyanyasaji na ukatili wa kijinsia ambalo limekithiri.
Ameongeza kwamba kumekuwa taarifa nyingi zinazotolewa na vyombo vya habari pamoja na wanajamii ambao wamejitokeza wazi kutoa matukio mbalimbali juu ya suala hilo. Pia tafiti mbalimbali ambazo zimefanywa, hivyo wamegundua kuwa matukio mengi ya unyanyasaji na ukatili wa kijinsia yanafanywa wahusika wanaotuhumiwa kuwa ni familia au ndugu wa karibu.
Amesema kuna mapungufu katika jamii kama vile utamaduni wa kutokuwa na utayari wa kusimamia na kuyapigia kelele tatizo hilo, ikiwa ni sababu mojawapo ya unyanyasaji na ukatili huo.
“Kupitia mafunzo haya kama watoa maamuzi tunataka wapate jicho la kipekee shauri linapokuja mbele yako mara moja unapata picha kuwa hili ni la kikatili na unalipa nafasi yake na hii itasaidia katika kuandaa taarifa ya matukio haya kwa usahihi, ikiwemo kuwa na takwimu ambazo tunazihitaji ili kujua nguiu gani ya ziada inahitajika katika kusimamia jambo hili,’’ amesema Jaji De Mello.
Mshiriki mwingine wa mafunzo hayo, ambaye Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Sokoine,iliyopo Jijini Dar es Salaam, Hanifa Mwingira amesema jamii inapaswa kuona kuwa vitendo hivyo ni vibaya na kila mtu anapaswa kusema ‘ukatili sasa basi na mtoto wa mwenzako kuwa ni mtoto wako na hupaswi kumfanyia ukatili,’.
Mwingira amefafanua kuwa mafunzo hayo yametolewa kwa viongozi wa dini ambao watawaelimisha waumini wao, wakiwemo Wenyeviti wa vijiji, kata pamoja na mitaa na Maafisa wa Ustawi wa Jamii, Polisi, Magereza na wadau wengine wa sheria.
Mafunzo hayo yanayoendelea Mjini Bagamoyo Mkoani Pwani yalihudhuriwa na Majaji Wataafu kama vile Jaji Mstaafu wa Mahakama ya Rufani Tanzania, Mhe. Salum Massati ambaye anashiriki kama mtoa mada.
Jumla ya washiriki 26 wanapatiwa mafunzo hayo yaliyoanza Juni 27, mwaka huu na yatamalizika Julai Mosi, mwaka huu, wakiwemo wawili toka Zanzibar.
More Stories
ITA chatakiwa kutoa mafunzo ya viwango vya juu na kasi ya maendeleo ya Kisayansi
Wagombea CHADEMA wakipewa ridhaa,watakuwa wawazi
TTCL yafanya maboresho katika huduma zake