September 20, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

MAIPAC, kuelimisha madhara ya ukeketaji jamii ya kifugaji

Na Mwandishi wetu , Timesmajira Online,Longido

SHIRIKA la Wanahabari la Usaidizi wa Jamii za Pembezoni(MAIPAC),linatarajia kuzindua mradi kabambe wa kuelimisha athari za ukeketaji kwa watoto wa kike, katika jamii ya kifugaji ya Kimasai.Ikiwa ni pamoja na kuwajengea uwezo wanawake wa kutetea haki zao.

Mradi huo unafadhiliwa na shirika la Cultural Survival,unatarajiwa kusaidia pia kupaza sauti za vijana wanaopinga vitendo vya ukeketaji.

Mkurugenzi wa Shirika la MAIPAC, Mussa Juma ametoa taarifa hiyo katika ziara iliyofanywa na Asasi za Kirai katika wiki ya Asasi hizo iliyofanyika wilayani Longido .

“MAIPAC imebaini kuwa watoto wa miaka miwili,ukeketwa katika jamii ya Kimasai.Tunampango wa kuzindua mradi wa kuelemisha kuhusu ukeketaji na ukatili kwa watoto wa kike.Pia kuwajengea uwezo,wanawake wa kimasai wa kujiamini na kuweza kutetea haki zao za msingi hasa kukemea ukatili,” amesema.

Wadau wa asasi hizo wamepata wasaa wakutembelea kikundi cha wanawake wanaofadhiliwa na shirika la Legal Service Facility(LSF) na Vodacom Foundation.Ambapo Mkurugenzi wa LSF ,Lulu Ng’wanakilala amesema shirika hilo limekuwa likisaidia vikundi 11 vya wanawake wa jamii ya kifugaji kata Kimokoa wilaya ya Longido.

Ng’wanakilala amesema wanawake wa jamii za kifugaji bado wanakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo za kiuchumi,ushiriki katika siasa na changamoto za kiafya.

Hata hivyo amesema kupitia mradi wanaotekeleza Longido, wameweza kusaidia jamii ya wanawake,kiuchumi kwa kuwa na miradi midogo,ushiriki katika masuala ya kisiasa na kupambana na changamoto za kiafya ikiwepo ikeketaji.