Na Yusuph Mussa, Timesmajira Online,Lushoto
NAIBU Waziri wa Maji Mhandisi Maryprisca Mahundi amewaasa wanafunzi wa shule ya sekondari ya wasichana St. Mary’s Mazinde Juu kusoma kwa kujiamini huku wakizingatia ndoto zao za kuwa wanataka kuwa nani kwenye maisha yao.
Amesema kusoma shule hiyo ni fursa kwenye maisha, sababu watafundishwa mambo mengi ikiwemo taaluma, maadili, nidhamu pamoja na utulivu wanaopata, hivyo wanatakiwa kusoma kwa kujiamini, huku wakiwa wamebeba ndoto kwenye maisha ili kujisaidia wao,familia,jamii na taifa.
Mhandisi Mahindi ameyasema hayo alipotembelea shule hiyo ambayo alisoma kuanzia kidato cha kwanza hadi cha tano mwaka 1995 hadi 1999, na kwenda kumalizia kidato cha sita Makongo High School jijini Dar es Salaam.
Pamoja na mambo mengine amewapa zawadi ya taulo za kike, biskuti na pipi wanafunzi wa shule hiyo.
“Tunataka kuona viongozi wa kesho wanatoka hapa,Mawaziri wanatoka hapa, wakuu wa mikoa, wahandisi na wataalamu wengine,mimi nilipambana kuona ninakuwa kiongozi hata nilivyokuwa hapa, nilikuwa Dada Mkuu, hivyo na ninyi mnatakiwa kuwa na ndoto kwa kila jambo mnalofanya,”amesema Mahundi.
Mkuu wa Shule hiyo ambayo inaendeshwa na Masista wa Shirika la Mama wa Usambara (COLU) chini ya Kanisa Katoliki Jimbo la Tanga, Mtawa Evetha Kilamba, amemshukuru Naibu Waziri kwa zawadi alizowapelekea, lakini kikubwa kuweza kuwakumbuka na kufika shuleni hapo baada ya kupita miaka 26 tangu kusoma shule hiyo.
Dada Mkuu (mstaafu) ambaye pia anasoma kidato cha sita kwenye shule hiyo Margareth Mboya, amesema kuwa huo ni upendo mkubwa, na wao wataendelea kuthamini zawadi hizo, na kumtakia kila la kheri Naibu Waziri kwenye majukumu yake ya kila siku.
More Stories
Maofisa Watendaji watakiwa kufanya kazi kwa weledi
Muhoji Sekondari kumaliza changamoto ya umbali kwa wanafunzi Musoma vijijini
Tanzania mwenyeji mkutano wa nishati wa Wakuu wa Nchi za Afrika