December 29, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mahundi amtaka Mkandarasi Lushoto kukamilisha mradi kwa wakati

Na Yusuph Mussa, Timesmajira Online,Lushoto

NAIBU Waziri wa Maji Mhandisi Maryprisca Mahundi amemtaka Mkandarasi anaejenga anayetekeleza mradi wa maji Magamba Lushoto Mjini, M/S PNR Services Ltd ya mkoani Dar es Salaam, kukamilisha mradi huo ifikapo Aprili, mwaka huu, kwani hawataweza kumuongezea muda mwingine.

Kipande anachotakiwa kukamilisha ni cha bomba kubwa lenye kipenyo cha inchi 12 la kutoa maji kutoka chanzo cha maji kilichopo Kibohelo hadi lilipo tenki la maji Magamba Cost lenye urefu wa kilomita 5.4.

Naibu Waziri wa Maji Mhandisi Maryprisca Mahundi akipanda kwenye tenki la maji mradi wa maji Ngulwi uliopo Kata ya Ngulwi, Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto.

Ameyasema hayo Januari 6, 2024 alipotembelea chanzo cha maji Kibohelo ikiwa ni ziara ya siku tatu ya kukagua miradi ya maji kwenye majimbo matatu ya Lushoto, Bumbuli na Mlalo yaliyopo Wilaya ya Lushoto mkoani Tanga.

“Natoa agizo, na hili ni kwa wakandarasi wote nchini hatutaongeza muda wa kukamilisha miradi ya maji,tunataka miradi ikamilishwe kwa wakati ili wananchi wapate maji viongozi wanapokwenda kukagua miradi wapate majibu ya kutosheleza kuhusu utekelezaji wa mradi,”amesema Mhandisi Mahundi.

Hivyo wanataka mradi huo ukamilike Aprili, mwaka huu kwa kukamilisha kazi zilizobaki ikiwemo ujenzi wa bomba kubwa la kutoa maji kwenye chanzo hadi kwenye tenki kwani nia yao ni kuona wananchi wa Mji wa Lushoto wanapata maji ya uhakika.

Awali, Meneja wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Wilaya ya Lushoto Mhandisi Erwin Sizinga amesema kuwa mradi huo unatekelezwa na RUWASA Wilaya ya Lushoto kwa fedha za Mfuko wa Maji wa Taifa (NWF), na ni muendelezo wa mradi wa maji Lushoto, ambapo tayari kumejengwa tenki la maji lenye ujazo wa lita 650,000 eneo la Magamba Cost.

Naibu Waziri wa Maji Mhandisi Maryprisca Mahundi (katikati) akiwasili kwenye chanzo cha maji (Intake) Kibohelo cha mradi wa maji Magamba Lushoto Mjini.

Mhandisi Sizinga amesema mradi huo utakaogharimu zaidi ya bilioni 1.8 huku mkandarasi akiwa ameshalipwa zaidi ya milioni 647, na ujenzi wake ukiwa umefikia asilimia 70, utanufaisha wananchi zaidi ya 30,835 kwenye Mji wa Lushoto na viunga vyake.

“Kazi zilizofanyika ni ujenzi wa chanzo kipya cha maji eneo la Kibohelo kwa asilimia 100 ni uchimbaji wa mitaro njia za mitawanyo zenye urefu wa mita 14,600, uchimbaji wa mitaro katika njia kuu ya bomba yenye urefu wa mita 5,400 (kazi haijaanza), uunganishaji na ulazaji wa bomba katika njia za mitawanyo za bomba zenye urefu wa mita 14,600 (asilimia 98), na ujenzi wa chemba za airvalve na washaout (ujenzi bado),”amesema Mhandisi Sizinga.

Mhandisi Sizinga amsema mkataba wa mradi huo ulisainiwa Machi Mosi, 2022, na ulipaswa kukamilika Januari 30, 2023, lakini kutokana na changamoto ya msamaha wa kodi, mradi ulianza rasmi Novemba 17, 2022, na mkataba unaisha Machi 30, 2024.

Naibu Waziri wa Maji Mhandisi Maryprisca Mahundi (wa pili kulia) akiwa kwenye chanzo cha maji (Intake) Kibohelo cha mradi wa maji Magamba Lushoto Mjini.

Naibu Waziri, pia ametembelea mradi wa maji Irente- Yoghoi- Ngulwi- Bombo uliopo Kata ya Ngulwi, ambapo baada ya kupokea malalamiko ya upendeleo wa mgao wa maji, aliiagiza RUWASA kuendelea kusimamia Vyombo vya Watoa Huduma ya Maji Ngazi ya Jamii (CBWSO’s) pamoja na kubadilisha wafanyakazi wanaogawa maji kwenye eneo hilo ili kuweka wengine watakaogawa maji kwa usawa.

Akizungumza kwenye mikutano ya hadhara kwa nyakati tofauti na wananchi wa Kata za Ubiri na Gare, Mhandisi Mahundi ameahidi kuzitafutia maji ya uhakika kata hizo huku wananchi wa vijiji vya Miegeo na Handei kwenye Kata ya Ubiri kupata maji wiki ijayo kutoka kwenye mradi wa maji Ngulwi, huku Kata ya Gare ikichimbiwa visima kabla ya kusubiri mradi mkubwa wa maji ya bomba ya kata 13.

Naibu Waziri wa Maji Mhandisi Maryprisca Mahundi (wa pili kushoto) akiwa juu ya tenki la maji Mradi wa Maji Ngulwi, huku akipata maelezo kutoka kwa Meneja wa RUWASA Wilaya ya Lushoto Mhandisi Erwin Sizinga (katikati). (