April 26, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Paroko wa Kanisa Kuu la Jimbo Katoliki la Kahama , Parokia ya Kahama mjini Padri Salvatore Guerera akibariki matawi katika misa ya matawi iliyofanyika hapo jana asubuhi kwa kufuata maelekezo ya serikali na Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania juu ya kujikinga na ugonjwa wa Corona , (Picha na Patrick Mabula)

Mahubiri ya Corona yakolea makanisani

Na Waandishi Wetu

VIONGOZI mbalimbali wa dini wamewataka waumini kote chini kufanya maombi kwa ajili ya kumuomba Mungu kuiepusha Tanzania na dunia kwa ujumla na ugonjwa wa Corona ambao unazidi kutetea maelfu ya watu duniani.

Viongozi hao wametoa wito huo kwa nyakati tofauti wakati wa Ibada yaJuma Kuu la Pasaka iliyofanyika kwenye makanisa mbalimbali nchini.

Kwa upande wake Askofu wa Jimbo Kuu Katoliki la Mbeya,Gervas Nyaisonga, aliwataka waumini wa kanisa hilo kutumia Juma Kuu la Pasaka kuliombea taifa na Dunia kwa ujumla ili Mungu atuepushe na ugonjwa wa Corona (COVID-19).

Askofu Nyaisonga ambaye pia ni Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) aliyasema hayo jana wakati akihubiri kwenye misa takatafu ya Dominika ya Matawi katika Parokia ya Mtakatifu Mathias Mtume,Simike jijini hapa.

Katika Mahubiri yake alisema dunia inahitaji maombi kwa Mungu atuepushe na ugonjwa wa Corona. “Ndugu zangu tunapokumbuka mateso ya Bwana Yesu Kristo katika kipindi hiki tuzidi kumuomba Mungu atukinge na atuepushe na janga la Corona,”alisema.

Alisema ili kukabiliana na maambukizi ya Corona wazazi na walezi  wanatakiwa kuchukua tahadhari kwa kutowaruhusu watoto kutoka nyumbani badala yake muda huo wautumie kujisomea.

Katika hatua nyingine aliwatahadharisha vijana kujiepusha na maambukizi ya ya UKIMWI kwa kuwa kundi hilo lipo katika  hatari ya kupata ugonjwa huo.

Alisema katika kipindi hiki,kanisa linahitaji kuwaombea vijana ili wajiepushe na ugonjwa huo hatari kwa sababu kundi hilo linapita katika majaribu mengi.

Akinukuu takwimu,Askofu Nyaisonga alisema Tanzania kila siku watu 200 wanaambukizwa VVU na wengi wao ni vijana, hivyo wanatakiwa kujiepusha na ugonjwa huo.

Katika hatua nyingine Paroko wa Kanisa Kuu la Jimbo Katoliki la Kahama, Padri Salvatore Guerera, amewataka waumini kulitumia Juma Kuu la Pasaka lililoanza  jana kufanya maombi  ili Mungu aweze kuondoa janga la Corona.

Akizungumza katika misa ya matawi jana iliyofanyika katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Karoli Lwanga Parokia ya Kahama Mjini, Padri Guerera, aliwataka waumi kusali na kumuomba Mungu ili atuondolee janga la Corona.

Padri Guerera alisema Corona imevuruga amani duniani hivyo waumini popote walipo wazidi kumuomba Mungu atuondolee janga hilo.

“Tunapoanza Juma Kuu la Pasaka pamoja na kushiriki mateso ya Yesu Kristo kila mmoja popote alipo amuombe Mungu atuondolea janga la Corona,”alisema.

Alisema sala zetu pia ziwe za kuombea watu wanaoumwa Corona na waliofariki.

Wakati huo huo Mkuu wa Mkoa wa Singida, Dkt. Rehema Nchimbi amesema Serikali mkoani hapa inatarajia kuwafungia watu wote wanaofanya biashara za kuuza pombe za kienyeji kwa watakaokaidi maelekezo ya kujikinga na Corona.

Dkt Nchimbi alitoa agizo hilo kwenye mkutano wa Baraza la Jumuiya wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) Mkoa wa Singida waliokutana kujadiliana hatua za kujikinga Corona.

Alisema katika kipindi hiki wauzaji wa pombe wanatatakiwa kuhakikisha kila mteja wanayemuhudumia mtu anakuwa na chombo chake cha kuwekewa kinywaji hicho, tofauti na ilivyozoeleka wakitumia  kimoja.

“Kila mmoja anayetaka kufanya biashara hiyo ni lazima ahakikishe  ananawa mikono yake kwa kutumia maji yanayotiririka na sabuni,kukaa mbali mbali ni lazima kila mmoja awe na chombo chake hatuoni vibaya kama kila mtu atakwenda na kifaa chake,”alisema.

Alisema  sio kila mtu atakuwa akijichote pombe   na kwamba mfanyabiashara hatatekeleza maagaizo hayo atafungiwa biashara zake.

Imeandikwa na Esther Macha,Mbeya, Patrick Mabula, Kahama. Na Jumbe Ismailly, Singida.