November 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kiongozi wa Chama cha ACT, Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe

Mahakama yatoa hati kukamatwa kwa Zitto

Na Grace Gurisha

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, imetoa hati ya kukamatwa Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe kupitia tiketi ya Chama cha ACT- Wazalendo, kwa kushindwa kufika mahakamani bila kutoa taarifa yoyote.

Pia, mahakama hiyo imepanga kutoa hukumu ya kesi ya uchohezi inayomkabili Zitto Mei 29, baada ya kusikiliza mashahidi 15 wa upande wa mashtaka na mashahidi nane wa upande wa utetezi.

Amri hiyo ilitolewa jana na Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi wakati kesi hiyo ilipokuja kwa ajili ya kupangiwa tarehe ya hukumu baada ya kesi hiyo kumalizika kwa usikilizwaji.

Upande wa mashtaka uliwakilishwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Tumaini Kweka, ambapo upande wa utetezi haukuwa na uwakilishi wowote akiwemo mshtakiwa mwenyewe (Zitto). Zitto anatetewa na Wakili Peter Kibatala na Jebra Kambole.

“Hakuna mtu aliyekuja kusema mshtakiwa yuko wapi natoa hati ya kukamatwa kwa mshtakiwa,” alisema Hakimu Shaidi

Katika kesi ya msingi Zitto anakabiliwa na mashtaka matatu ya uchochezi ambapo, anadaiwa Oktoba 28, 2018 akiwa katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika katika Makao Mkuu ya ofisi ya Chama cha ACT Wazalendo alitoa maneno ya uchochezi yenye kuleta hisia ya hofu na chuki.

Inadaiwa kuwa mshtakiwa alitamka kuwa ‘’…watu ambao walikuwa ni majeruhi katika tukio la mapambano baina ya wananchi na Polisi wakiwa wamekwenda hospitali kupata matibabu katika kituo cha afya Nguruka, Polisi wakapata taarifa kuwa kuna watu wanne wamekwenda hospitali Kituo cha Afya Nguruka kupata matibabu wakawafuata kule wakawaua..’’

Katika shtaka la pili ilidaiwa Oktoba 28, mwaka huu maeneo ya Kijitonyama katika makao makuu ya chama hicho, jijini Dar es Salaam, alitoa maneno ya uchochezi dhidi ya Jeshi la Polisi akisema; “Lakini tumefuatilia kwa kina jambo hili, taarifa ambazo tumezipata kutoka kijijini Mpeta-Nguruka, Uvinza ni mbaya, ni taarifa ambazo zinaonesha wananchi wengi sana wameuawa na Polisi pamoja na kwamba afande Sirro amekwenda kule, haijatoa taarifa yoyote kuhusu wananchi.

Kama hawa Wanyantuzu walivamia eneo la Ranchi kuna taratibu za kisheria za kuchukua na sio kuwaua, wananchi wengi sana wamekufa.”Ilidaiwa kuwa katika tarehe hiyo hiyo, Zitto alitoa maneno ya uchochezi dhidi ya Jeshi la Polisi akisema;

“Tumekuwa tukifuatilia kwa kina yanayojiri yote huko Uvinza tunasikitika kusema kuwa taarifa tunazozipata kutoka Uvinza zinaogofya mno, kwani tunaambiwa kuwa wananchi zaidi ya 100 wa kabila la Wanyantuzu wamepoteza maisha kwa kupigwa risasi na Polisi, wengine wakisema kuuawa hata wakiwa kwenye matibabu hospitalini baada ya kujeruhiwa kwenye purukushani na Jeshi la Polisi…’’