Na Mwandishi Wetu,Timesmajira
MAHAKAMA ya Rufani nchini, leo Tarehe 4 June 2025, imetupilia mbali maombi ya rufani namba 658 ya 2023 yaliofunguliwa na kampuni ya Mwananchi Communication na Mhariri wa Gazeti la The Citizen.
Kampuni ya Mwananchi Communication, ilikata rufaa kupinga uamuzi wa Mahakama Kuu wa kumlipa fidia ya sh bilioni 2.5 Msajili wa Hazina, Nehemia Mchechu kwa kuandika habari iliyomchafua.
Katika habari hiyo iliyochapishwa na Gazeti la The Citizen tarehe 23 Machi mwaka 2018, iliripoti kuwa Mchechu wakati huo akiwa Mkurugenzi wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) ni fisadi na alitumbuliwa na Rais John Magufuli, jambo ambalo sio kweliRufaa hiyo ilipitiwa na majaji watatu wa Mahakama ya Rufaa ambao ni Jaji Rehema Kerefu, Jaji Omar Othman Makungu na Jaji Dk. Benhajj Masoud.
Katika uamuzi wake jana chini ya jopo la Majaji watatu, Mahakama ya Rufaa imekubaliana na uamuzi wa Mahakama Kuu kwenye kesi namba 48 ya 2021 kwamba habari hiyo ilikuwa ya uongo na imechafua hadhi na heshima ya Mchechu ndani na nje ya nchi, hivyo tozo iliyotolewa ni sahihi.Katika uamuzi wake, Mahakama ya Rufani iilipitia hoja tatu za msingi.
Hoja ya kwanza ni je, Mahakama Kuu ilikuwa na uwezo kusikiliza shauli hili, pili mdai (Mchechu), aliweza kuthibitisha madai yake ya kudhalilishwa na hoja ya tatu ni kama Mahakama Kuu ilitumia utaratibu sahihi kutoa nafuu kwa walalamikiwaKwa mujibu wa uamuzi huo, jopo hilo la majaji walikubaliana na hoja za wakili wa utetezi, Aliko Harry Mwamanenge kwamba Mahakama Kuu ilikuwa na uwezo wa kusikiliza kesi hiyo na kwamba mjibu rufani alifanikiwa kuthibitisha madai yake.
Jopo hilo la majaji pia wamekubali kwamba Mahakama Kuu ilitumia utaratibu sahihi kufikia tuzo ambayo ilitoa.Hivyo, Mahakama ya Rufani haikuona sababu ya kubatilisha au kubadilisha chochote kwenye maamuzi ya Mahakama Kuu na kuyabariki maamuzi hayo kama yalivyo.
Awali, Mahakama Kuu iliamuru Gazeti la The Citizen kumlipa Mchechu sh bilioni 2.5 kwa kuandika habari iliyomchafulia jina lake.
Katika adhabu hiyo, sh bilioni 2 ni kwa ajili ya kumlipa fidia kwa kuchafulia jina alilolijenga kwa muda mrefu na kumshushia heshima na sh milioni 500 kwa ajili ya kumsababishia hasara ya jumla.
Mbali ya kiasi hicho cha fedha, Gazeti la The Citizen limeamuriwa kulipa gharama zote za uendeshaji wa kesi kuandika habari ya kumwomba radhi katika ukurasa wake wa mbele kwa ukubwa ule ule na italipa fidia asilimi 12 kila mwaka endapo litashindwa kulipa fedha hizo kwa wakati kuanzia jana.
Katika hukumu hiyo, Mahakama Kuu pia imelionya Gazeti hilo kutomwandika tena Mchechu habari ya uongo na yenye kumchafulia jina kiasi hicho isipokuwa pale tu kunapokuwa na ukweli na ushahidi wa kutosha.
Hukumu hiyo imetokana na kesi iliyofunguliwa na Mcheche dhidi ya Gazeti la The Citizen, akiiomba mahakama iliamuru Gazeti hilo limlipe fidia ya Sh bilioni tatu na kumwomba radhi, kwa madai ya kumchafulia jina na kushusha hadhi na heshima yake katika jamii.
More Stories
Kiongozi wa Mwenge apongeza wananchi kupelekewa huduma ya maji Handeni
TFS yawakaribisha wawekezaji katika vivutio vya utalii wa misitu
Waziri Bashungwa:Tumieni teknolojia za kisasa kudhibiti uhalifu unaovuka mipaka