November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mahakama ya Mafisadi yawahukumu raia wa Iran miaka 30 kusafirisha dawa za kulevya

Na Grace Gurisha, TimesMajira Online

MAHAKAMA Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi maarufu ‘Mahakama Mafisadi’, imewahukumu Raia wawili wa Iran kifungo cha miaka 30 jela, baada ya kupatikana na hatia ya kusafirisha dawa za kulevya aina ya heroine zenye uzito wa kilo 111.02.

Pia Mahakama hiyo imetaifisha Jahazi lililokuwa likisafirisha sawa hizo na kuamuru kuteketezwa kwa dawa hizo za kulevya.

Raia hao ambao watatumikia kifungo hicho ni Nahodha, Nabibaksh Bibade na Injinia Muhammad Hanif wa Jahazi lililokuwa likisafirisha dawa hizo, na washtakiwa wengine 11 wameachiwa huru baada ya upande wa mashtaka kushindwa kuthibitisha mashtaka dhidi yao.

Walioachiwa ni Abdallah Sahib, UIbeidulla Abdi, Naim Ishaqa, Moslem Golmohamad, Rashid Badfar, Omary Ayoub, Tahir Mubarak and Abdulmajid Pirmuhamad, ambao ni Raia wa Iran na Ally Abdallah na Juma Amour ambao ni Watanzania.

Hukumu hiyo namba 14/2018 imesomwa na Jaji Imakulata Banzi wa Mahakama hiyo baada ya kupitia ushahidi wa mashahidi 10 wa upande wa mashtaka, sheria na vielelezo vilivyowasilishwa mahakamani hapo, wakati kesi hiyo ilipokuwa ikisikilizwa.

Jaji Banzi amesema, upande wa mashtaka umeweza kuthibitisha mashtaka dhidi ya Nahodha Bidade na Injinia Hanif bila kuacha shaka lolote kwa hiyo washtakiwa wamepatikana na hatia ya kusafirisha dawa hizo kinyume na sheria.

“Washtakiwa mtatumikia kifungo cha miaka 30 jela, baada ya kupatikana na hatia na pia, Mahakama imewaachia huru washtakiwa 11 ambao Jamhuri wameshindwa kuthibitisha kesi dhidi yao” amesema Jaji Banzi.

Upande wa mashtaka katika kesi hiyo umewakilishwa na Wakili wa Serikali, Monica Mbogo na Cecilia Shelli ambapo upande wa utetezi washtakiwa waliwakilishwa na wakili wa Juma Nassoro na Jethro Tiliemwesiga.

Kabla ya hukumu hiyo kusomwa, mawakili wa upande wa mashtaka Mbogo na Shelli waliomba adhabu kali itolewe kwa washtakiwa hao ili iwe fundisho kwa wengine.

Wakati wa kutoa utetezi wao, washtakiwa hao walijitetea wenyewe bila kuwa na mashahidi wengine.

Nahodha Bibade na wenzake 12 walikamatwa Oktoba 24,  2017 saa nne na robo usiku katika Bahari ya Hindi na Maafisa wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya ambapo mamlaka hiyo imeshirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama kuwakamata washtakiwa hao, ambao 10 ni raia wa nchini Iran na watatu ni watanzania.