December 25, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.John Magufuli.

Magufuli: Kujifukiza kumesaidia sana

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online

RAIS Magufuli amewataka Watanzania wasidharau dawa za kienyeji, kwani miti iliumbwa na Mungu kwa ajili ya kutusaidia, isipokuwa uchawi peke yake ndiyo mbaya.

Ametoa mwito kwa Watanzania kuendelea kuchukua hatadhari dhidi ya ugonjwa wa Corona, huku akisema kujifukiza kumesaidia sana.

Rais Magufuli ametoa kauli hiyo jijini Dodoma leo wakati akiweka jiwe la msingi la ujenzi wa barabara za kilometa 51.2 na kusisitiza kwamba ameishatoa maelekezo kwenye Wizara ya Afya ili kitendo cha dawa asili kiendelezwe kwa nguvu zote na bajeti yake iongezwe ili watu wanapotengeneza dawa zao wasidharauliwe.

“Kujifukiza kumesaidia sana. Corona bado haijaisha sana, lakini imepungua sana, tuendelea kuchukua tahadhari, wale waliotegemea tutakufa wengi sana na kwamba barabarani kutakuwa na maiti, wameshindwa na wakalegee kikweli kweli, Mungu wetu anatupenda na tuendelee kumuomba bila kusahau maarifa yetu ambayo tumekuwa tukiyatumia kupambana na maradhi mbalimbali.”

Amesema yatazungumzwa mengi na watu wao wanaowatuma, lakini tusikata tamaa Mungu ataendelea kubaki nasi.

“Tunamuomba na tutaendelea kumuomba na kwa hilo niwashukuru sana viongozi wa dini na wengine wote ambao waliguswa katika kipindi cha shida, Mungu hamtupi mtu anayemuomba,” amesema Rais Magufuli.

Amesema kumekuwa na kasumba watu wanapotengeza dawa za kienyeji wanasema ni madawa yaliyopitwa na wakati, wewe ndiye uliyepitwa na wakati.

“Dawa za kienyeji ni dawa kama zilivyo dawa nyingine, tulipumbazwa tusiamini kilicho chetu, tuamini kilicho chao. Niwaombe Watanzania tubadilike,” amesema Rais Magufuli.

Ametaka vitengo vyote vinavyoshughulika na dawa asili na wale wote wanaotengeneza dawa za asili, wasaidiwe na ndiyo maana ukienda nchi nyingine zilizoendelea hata China, kuna dawa, lakini kuna dawa za asili na kuna maduka kabisa kwa ajili ya kuuza dawa hizo.

“Hata ukienda Ulaya, ukienda Canada kuna madawa kabisa ya asili, niwaombe wizara na vitengo vinavyohusika, tusidharau vyetu, tujiendeleze tuweze kupambana na magonjwa mbalimbali,” amesema Rais Magufuli.