December 25, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Dkt. John Pombe Magufuli akizungumza katika Viwanja vya Uhuru Jijini Dar es Salaam katika tukio la kumuaga Hayati Benjamin William Mkapa,

Magufuli amwaga chozi hotuba ya kumuaga Mkapa

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online, Dar es Salaam

RAIS John Magufuli, amewatoa chozi viongozi mbalimbali wakiwemo marais wastaafu pale alipoanza kububujikwa na machozi wakati akieleza yale aliyofanyiwa na Rais Mstaafu Mstaafu wa Serikali ya Awamu ya Tatu, Marehemu Benjamin Mkapa katika maisha yake.

Akihotubia taifa kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam, Rais Magufuli amesema; “Mzee Mkapa ni shujaa wangu, hakutaka niaguke, alinilea kama mtoto wake kutoka kwake ni pigo kubwa kwangu.

Hivi nilivyo ni kwa ajili ya Mzee Mkapa.” Mara baada ya kauli hiyo, Rais Magufuli alianza kububujikwa na machozi, huku akilazimika kukatisha hotuba yake kwa kushindwa kuzungumza, alichukua kitambaa chake na kujifuta chozi.”

Huku akijitahidi kuendelea na hotuba yake, Rais Magufuli amesema kama Mzee Kikwete ambaye ni Kanali alishindwa kujizuia kulia na hii inaonesha kuwa inaumiza.

Rais Magufuli ameendelea kusema; “Kusema kweli nilikuwa nimemzoea sana Mzee Mkapa, kila Mtanzania aliyekuwa akiwaona marais mastaafu hawa alikuwa anafurahi, walikuwa kama mapacha wakiwa wote watatu, lakini leo tutakuwa tukiwaona wakiwa wawili, Mzee Mkapa hatutakuwa naye milele…hii inaumiza sana.”

Kauli hiyo ya Rais Magufuli amezidisha simanzi na huzuni kwa watu waliojitokeza kuaga mwili wake, huku wengine wakibubujikwa na machozi.

Rais Magufuli amezidi kusema; “Mtakumbuka katika siku za hivi karibuni viongozi hawa walikuwa pamoja kwenye uzinduzi kitabu cha Mzee Mkapa, walikuwa wote wakati wa uzinduzi wa awamu ya tatu ya TASAF na walikuwa wote wakati wa kuweka jiwe na msingi Ikulu ya Chamwino.”

Rais Magufuli ameongeza kuwa wakati wa kuvunja Bunge marais hao wastaafu watatu walikuwepo na Julai 11, mwaka huu walikuwepo kwenye Mkutano wa CCM.

“Lakini sasa hatutawaona wakiwa watatu, Mzee Mkapa hatutamuona tena. Mzee Mkapa niliongea naye akiwa Hospitalini kwa simu akaniambia, John usiwe na wasiwasi naendelea vizuri. Sikujua kuwa maneno yake yalikuwa ni ya kuniaga.

Namshukuru Mungu kwa zawadi ya mzee kazi ameikamilisha.. Mzee Mkapa, Mzee Mwinyi na Mzee Kikwete tulikuwa nao mara nyingi, lakini leo Mkapa hayupo,” amesisitiza Rais Magufuli na kububujiwa machozi tena.

Ametoa wito kwa Watanzania wajitaidi kufanya mambo mazuri ili tutakapoondoka tuvishwa taji. Alishukuru Watanzania kwa kudhihirisha umoja na mshikamano, alipongeza viongozi wa dini kwa kuendelea na mshikamano wetu na maneno ya kututia faraja.

Ameshukuru vyombo vya ulinzi na usalama tangu msiba umetokea, uwepo wa salamu za watu mbalimbali umewapa faraja na umewafanya kuonekana wapo karibu nasi.