December 22, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akiwa pamoja na viongozi mbalimbali wa Arusha na Kilimanjaro akikata utepe kuashiria uzinduzi wa huduma ya usafiri wa Treni ya Abiria ya Shirika la Reli TRC kutoka Dar es Salaam hadi Arusha katika hafla fupi iliyofanyika katika Stesheni ya Arusha leo tarehe 24 Oktoba 2020

Magufuli akemea ubinafsishaji meli,ndege na reli

Na Penina Malundo,TimesMajira,Online

RAIS John Magufuli amesema suala la ubinafsishaji wa vyombo mbalimbali vya usafiri ikiwemo Reli,Ndege na Meli ni dhambi kubwa kwa serikalini kutokubali ubinafsishwaji wa vyombo hivyo tena .

Kauli hiyo ameitoa leo Mkoani Arusha wakati wa Uzinduzi wa Safari za Treni Dar,Tanga hadi Arusha,Magufuli amesema nchi ilifikia pabaya kwa hatua ya kubinafsisha vyombo hivyo na hilo liwe fundisho kwa viongozi wa sasa.

“Tulibinafsisha ndege zote zikaisha tukaanza upya…Treni nayo tukaanza upya tulikuwa na Meli zilizoachwa tangu enzi ya Baba wa Taifa zikabinafsishwa hii iwe fundisho,mimi sitokuwa Rais wa Maisha natoa fundisho kwa viongozi watakao kuja baada kuacha kubinafsisha vyombo hivi,”amesema na kuongeza

“Tulipobinafsisha hili shirika la reli ,wakawa wanachukua mabehewa yetu wanapeleka kule, kwahiyo hapakuwa na chochote kilichobaki,watendaji nao wakastaafishwa ,wafanyakazi nao wakaachishwa kazi hili tunajifunza,amesema Magufuli

Magufuli amewashukuru watendaji wa Shirika hilo kwa kufanya maajabu kwaajili ya taifa, kwani kuna kipindi walimfata na kumuomba kiasi cha fedha Bilioni 5 kwaajili ya kufufua mabehewa na zilifanya kazi hadi kukamilika kwa reli hiyo.

“Watendaji hawa wamefanya maajabu makubwa sana hadi leo,nawahakikishia TRC na Wizara ya Uchukuzi tutaendelea kuwaunga mkono mara tutakapomaliza Uchaguzi Mkuu,”amesema

Aidha Magufuli amesema wamepanga kununua vichwa vya Treni 39 kwa njia kuu,Vichwa 18 vya sogeza songeza,Mabehewa 800 ya mizigo na 37 ya abiria .

Amesema wanataka shirika hilo kuwa mfano kwa Afrika kwa mashirika yanayofanya Biashara na kazi kwa kuhudumia wananchi wake wakiwemo wanyonge.

Magufuli amewataka watu wa TRC kuhakikisha wanaimarisha na kuboresha huduma zao na kuhakikisha gharama zao zinakuwa chini na kuhakikisha wanapinga rushwa ili watanzaniawaweze kunufaika na usafiri huo.

Pia amewataka watanzania hususani wakazi wa mikoa ya Kaskazini kutumia reli vizuri ili kuweze kunufaika nayo kwani ni wajibu wawatanzania kulinda miundombinu hiyo.

‘’kuna wakati palikuwepo na watu waliokuwa wanafanya njama kuharibu reli naomba watanzania wa kanda hii na mahali popote panapopita treni watunze ili iweze kutuhudumia vizuri,ujio wa treni hili utasaidia uchumi wake kupanda na watu kufanya biashara,’’amesema

Ameeleza kuwa TRC wameongeza abiria kwenye reli ya Dar es Salaam kutoka milioni 1.27 mwa mwaka 2014/15 hadi abiria milioni 6.73.