December 22, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Magufuli afanya uteuzi, agusa Wizara ya Afya

Na Mwandishi Wetu

RAIS John  Magufuli amemteua Dkt. Zainab Chaula kuwa Katibu Mkuu wa Mawasiliano.

Kabla ya uteuzi huo, Dkt.Chaula alikuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto na amechukua nafasi iliyoachwa na Dkt. Maria Sasabo ambaye amestaafu.

Prof. Mabula Daudi Mchembe akila kiapo mbele ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto. Hafla iliyofanyika Wilayani Chato Mkoani Geita , Aprili 22, 2020.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari jana na Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu ilieleza kwamba Rais Magufuli amemteua Prof. Mabula  Mchembe kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto.

Kabla ya uteuzi huo, Prof. Mchembe alikuwa Msaidizi wa Rais katika masuala ya afya. Katika hatua nyingine, Rais Magufuli amemteua Prof. Abel Makubi kuwa Mganga Mkuu wa Serikali.

Kabla ya uteuzi huo, Prof. Abel Makubi alikuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando na amechukua nafasi iliyoachwa na Prof. Mohamed Kambi ambaye amestaafu. Kwa mujibu wa taarifa hiyo uteuzi wa viongozi hao umeanza jana.