Na Penina Malundo, TimesMajira Online,Chato
MGOMBEA urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi(CCM) Rais John Magufuli, amesema Tanzania ina kila sababu ya kuwa na uchumi wa kujitegemea badala ya kutegemea fedha za wafadhili kufanya maendeleo.
Akihotubia mkutano wake wa awamu ya pili ya kampeni zake ambazo zitakwa na raudi sita uliofanyika jana katika viwanja vya Mazaina na kuhudhuriwa na maelfu ya wananchi, Dkt. Magufuli aliomba wananchi kumchagua kuongoza tena nchi kwa kipindi cha miaka mitano.
Rais Magufuli alisema kuna watu ambao mawazo yao yamekuwa ni kusubiri fedha kutoka kwa wafadhili.
“Wafadhili wakuletee wewe, ukichukua fedha ya wafadhili wewe utalipa mara mbili au mara tatu yake, atakwambia anakuletea ufadhili halafu wanakuletea masharti mengi kiasi kwamba hadi hicho ambacho wameamua kukifadhili unakuwa umelipa mara mbili,”alisema.
Alisema kabla ya kuwa Rais alifanya kazi katika wizara tofauti tofauti ikiwemo Wizara ya Ujenzi, Wizara ya Ardhi,Nyumba na Maendeleo ya Makazi, pamoja na Wizara ya Mifugo na Uvuvi na kwamba anajua maana ya ufadhili.
Alisema anayetegemea cha ndugu mara nyingi hufa masikini na ukiona wanakuganda ujue wanataka kukunyonya. Pia alisema hata nchi za Ulaya nazo zimeendelea kwa sababu waliamua kujitegemea wenyewe na kuimarisha ulipaji kodi.
“Hata kwenye vitabu vya dini kodi inatajwa na ndio maana wanasema ya Kaisari muachie Kaisari, lakini inashangaza kuona mtu anasimama akisema akichaguliwa atafuta kodi,”alisema.
Aliongeza kuwa huwezi kuzungumza mtu anakula ubwabwa wakati hata nyumbani kwake haumtoshi.
“Na wengi wanasema wanakula bata wakati hata vitabu vya dini vinasema asiyefanya kazi na asile,” alisema Rais Magufuli na kuongeza;
“Lazima watu waambiwe ukweli na kikubwa katika kipindi hiki cha kampeni ni kusikiliza kwa makini sera za wagombea na kisha kufanya maamuzi sahihi.
Zingatieni sera za ukweli na msema kweli ni mpenzi wa Mungu.”
Hata hivyo alisema uongozi ni kujitoa sadaka, hivyo ameamua kutoa maisha yake kwenye uongozi kama sadaka kwa Watanzania, licha ya kuwa ni kazi ngumu, lakini anaweza kuifanya tena kwa miaka mingine mitano.
“Msifanye majaribio ya watu wengine, sioni kati ya wagombea wote urais ambaye anaweza kufanya mambo ambayo tumeyafanya kwa kipindi cha miaka mitano hata kwa robo, hayupo. Naawambia ukweli kama mnataka kujaribu jaribu na siku moja mtakuja kuniambia,”alisisitiza Dkt. Magufuli.
Hata hivyo alisema kama taifa katika miaka mitano limekutana na changamoto nyingi za kiuchumi, kiusalama, lakini kwa pamoja wameungana kuhakikisha tunaleta mabadiliko katika nchi yetu.
Alifafanua kwamba wakati anaingia madarakani nchi ya Tanzania ilikuwa nchi masikini, lakini leo hii inatambulika ni ya uchumi wa kati.
*** Kuhusu afya
Dkt. Magufuli alisema kipindi cha miaka mitano iliyopita wamejenga zahanti 1,200 nchi nzima, vituo vya afya 487 , hospitali za wilaya 98, mikoa 10 na hospitali za rufaa tatu na kwamba zingine zinakuja.
“Pia katika miaka mitano bajeti ya dawa imeongezeka kutoka sh.bilioni 31, hadi sh,bilioni 270 kwa mwaka,” alisema Dkt. Magufuli.
“Haya sio mambo ya kupuuzwa hata kidogo, kwani hata usambazaji dawa kupitia maduka ya MSD umeongezeka,tumefanya hivyo ili kujenga muelekeo mpya wa nchi.
Ukitaka kujenga uchumi wowote wa nchi lazima ujenge uchumi wa watu wenye afya njema, huwezi kujenga uchumi wa wananchi wako ambao ni wagonjwa ambao wakienda kutibiwa hawapati dawa,”alisema.
Pia alisema katika kipindi cha miaka mitano walihakikisha wazee na watoto wanapata matibabu bure na kwa mkakati wa Serikali katika miaka mitano inayokuja Watanzania wote watakuwa na bima ya afya.
“Tuliamua kujikita katika fedha za makusanyo tunayoyapata kwa ajili ya kufanya uwekezaji wa kutosha katika eneo la afya. Tayari tumejenga vituo vingi vya afya na haya ni mafanikio,”alisema na kuongeza hayo yote yanayoendelea kufanyika ni kuitengeneza nchi kuwa ya kisasa, hivyo wapewe tena miaka mitano kuendelea kuleta maendeleo ya Watanzania.
***Kuhusu amani
Akizungumzia hali ya usalama nchini, Dkt. Magufuli alisema wakati anaingia madarakani wilayani Kibiti kulikuwa na mauji ambapo hata askari polisi 12 waliuawa kwa kupigwa risasi, hivyo walisimama imara kuimarisha ulinzi.
“Zamani ukitaka kusafiri lazima usindikizwe na Polisi, nikasema hapana, majambazi hawawezi kutawala katika nchi hii, navipongeza vyombo vya ulinzi na usalama kwa kusimamia hali ya ulinzi nchini kwetu,”alisema Dkt.Magufuli na kuongeza nchi ikikosa usalama hakuna kinachoweza kufanyika.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa CCM, Bashiru Ali Kakuru alisema Chama hicho katika uchaguzi mkuu mwaka huu wamepanga kufanya mashambulizi ya kampeni katika awamu sita na tayari awamu ya kwanza imekamilika na sasa wameingia awamu ya pili.
Pia alimuomba mgombea Dkt.Magufuli kuhakikisha anaendelea kushambulia kila kona, kwani wapinzani wamejileta wenyewe, hivyo asiwaonee huruma.
”Nipo kuomba kura wewe mwenyewe na wagombea wote wa CCM nchi nzima ili tuweze kuendelea kuongoza Taifa letu. Tumemaliza awamu ya kwanza, na tutakuwa na raundi sita, raundi ya kwanza tayari na leo (jana) tunaanza tunaanza raundi ya pili na kila raundi itakuwa nzito.
Raundi ya pili itakuwa nzito na kubwa kuliko raundi ya kwanza, na raundi ya tatu itakuwa nzito kuliko ya pili,”alisema.
Wakati huo huo, Dkt. Bashiru alikanusha uvumi unaoenezwa kwamba CCM inataka kushinda viti vingi katika Uchaguzi Mkuu mwaka huu ili ibadili Katiba.
”Nataka kukanusha uvumi eti CCM inataka kushinda viti vingi, kwamba wakiwa wengi wanataka kubadilisha Katiba, nataka niseme iwe mwisho, hao ni watu waliochoka na kufirisika kisiasa . Dtk.Magufuli anaomba miaka yake mitano ili amalize miaka 10,hata ongeza hata sekunde, mbona hiyo setensi ni nyepesi!”
More Stories
Watoto wenye uhitaji wapatiwa vifaa vya shule
Wananchi Kisondela waishukuru serikali ujenzi shule ya ufundi ya Amali
RC.Makongoro ataka miradi itekelezwe kwa viwango