December 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Maghjee awataka wananchi kuungana na serikali kufanya maendeleo kwenye jamii

Na David John, TimesMajira Online

MWENYEKITI wa Taasisi ya The Desk Chair Foundation Muhamad Maghjee amezitaka taasisi mbalimbali nchini kujitokeza kuisaidia serikali katika kuwahudumia wananchi hususani katika kuwachimbia visima vya maji ili kuondolea aza ya maji ambayo imeonekana kuwa tatizo kubwa katika baadhi ya maeneo.

Wito huo umetolewa hivi karibuni Jijini Mwanza na Mwenyekiti wa Taasisi hiyo ya The Desk Chair Foundation.

Muhamad Madhjee wakati akikabidhi kisima cha maji kwa wananchi wa mtaa wa Kagomu uliopo kata ya Mahina ,Wilaya ya Nyamagana Jijini Mwanza ambapo amesema kuwa iko haja ya kuongeza kasi ya kuisaidia serikali kuchimba visima kama inavyofanya taasisi hiyo ili wananchi waweze kupata maji safi na salama.

Alisema kuwa katika mtaa huo kwa mujibu wa wananchi kulikuwa na tatizo kubwa la maji la muda mrefu hivyo walipeleka maombi ya mahitaji ya kuchimbiwa kisima ofisini kwao na wao kama taasisi hawakusita kusaidia kwasababu ndio zima yao kubwa kuona wananchi wanapata maji.

“Mfano mimi nimezaliwa hapa Mwanza katika wilaya Sengerema kulikuwa na shida kubwa ya maji hivyo sisi kama familia imetupelekea kuunda taasisi ambayo imejikita kutoa misaada mbalimbali ikiwepo kuchimba visima virefu vya maji safi na salama kwa ajili ya wananchi katika maeneo yenye ukame wa upatikanaji wa maji.’alisema Maghjee.

“Leo tunafuraha kubwa kukabidhi mradi huu wa maji ambao umekamilika kwaniaba ya wananchi wote wa eneo hili la Mahina ,naomba mpokee kisima hiki cha maji na mitambo kama pamp,Sola,Betteri,Tanki la kuhifadhia maji ,vifaa vya usafi na stoo ya kuhifadhia vitendea kazi.”Alisema ,Maghjee.

Pia aliwaeleza wananchi hao kuwa mradi huo wote sasa ni mali ya serikali ya mtaa na wahudumiwe wananchi wote bila kujali tofauti zao za kikabila ,dini,rangi, pamoja na jinsia.

“Tunashukuru sana viongozi wa ngazi zote wa eneo hili na wananchi wote na mafundi wote waliohusika kwenye mradi huu ambapo leo wamefanikisha kukamilika kwa mradi kwa wakati muafaka na tayari wananchi wote wanapata huduma ya maji.”amesisitiza

Maghjee alifafanua kuwa wao kama taasisi wataendelea kuchimba visima vingine vinne kwenye maeneo tofauti ili kupunguza msongamano kwenye kisima hicho cha kwanza huku akitoa rai kwa wananchi hao kukitunza na kukilinda na wao kama taasisi wasingependa kuona panajitokeza migogoro na ikabainika kuwa panamigogoro watakuwa wamewafukuza kabisa kwani wao sio waumini wa migogoro.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa mtaa huo Geoge Peche alisema kuwa wamepokea mradi huo kwa mikono miwili na wamehaidi kuuulinda kwa hali na mali na wameshaweka utaratibu wa kulinda mradi huo ambao ni mkubwa katika eneo lao.

Alisema kuwa moja ya utaratibu ambao wameuweka ni wananchi wenyewe kuhakikisha wanakuwa walinzi wa mradi huo sambamba na hilo lakini pia wameweka walinzi wanne ambao watakuwa wanalinda kwa zamu na katika huduma hiyo ya maji wananchi watakuwa wanachangia shilingi mitano kwa wiki ili kuwezesha kuwalipa walinzi hao ambao watakuwa na jukumu kubwa la kulinda mitambo kwenye kisima hicho.

Mwenyekiti wa Taasisi ya The Desk Chair Foundation Muhamad Maghjee akikabidhi vifaa vya kufanyia usafi mara baada ya kuzindua kisima kirefu cha Maji ambacho kimechimbwa na Taasisi hiyo Kwa wananchi wa mtaa Kagomu kata ya Mahina ,wilaya ya Nyamahana jijini Mwanza.
Mwenyekiti wa Taasisi ya The Desk Chair Foundation Muhamad Maghjee akisoma risala ya Taasisi hiyo baada ya kufanya uzinduzi wa kisima kirefu cha Maji Kwa wananchi wa mtaa wa Kagomu uliopo Wilaya ya Nyamahana mkoani Mwanza