*RPC Mwanza aeleza hatua walizochukua kulinda usalama wa wananchi
*Athibitisha hakuna kifo, majeruhi
*TANROADS yaeleza sababu na mpango uliopo
Judith Ferdinand, Timesmajira Online,Mwanza
Watumiaji wa barabara kuu ya Mwanza-Shinyanga, inayotoka na kuingia katikati ya jiji la Mwanza,Aprili 8,2025,wamekwama kwa saa kadhaa baada ya daraja la Mkuyuni kujaa maji na kushindwa kupitika,kufuatia mvua zinazoendelea kunyesha mkoani Mwanza.
Wakizungumzia adha waliopata baada kushindwa kupita kutoka upande mmoja kwenda mwingine,baadhi ya wananchi wameiomba Serikali kuangalia namna ya kuweza kuongeza urefu wa daraja la Mkuyuni, ili pindi mvua zinapokuwa nyingi maji yapite kwa chini huku wananchi wakiendelea na majukumu yao la kila siku.

Akizungumza na waandishi wa habari mmoja wa wanafunzi Alexander Daniel,amesema kilichotokea ni daraja la Mkuyuni kushindwa kuhimili maji ambayo yamekuwa mengi hivyo yakapita juu na kusababisha kukata mawasiliano ya pande mbili.
“Kutokana na hali hiyo imesababisha sisi wanafunzi kushindwa kwenda shuleni,kwa ajili ya kufanya mitihani.Tunaiomba Serikali wainue urefu wa daraja hili,ili siku nyingine kukiwa na changamoto kama hiyo ya kuwa na maji mengi, yapite chini na siyo juu, ili yasiathiri shughuli za watumiaji wa njia hiyo,”amesema Alexander.
Victoria Frederick ambaye ni mwanafunzi pos amesema,katika eneo hilo watu wanavushwa kwa kubebwa kwa kulipa shilingi 500,kwa upande wa wanafunzi kwao ni ngumu kwani wengine wanapatiwa kiasi hicho na wazazi wao kwa ajili ya kula shuleni au nauli.
Mathias Moses, amesema hali hiyo inasikitisha kwani wananchi wamekaa katika eneo hilo kwa muda mrefu hivyo kuathiri shughuli za kiuchumi na kijamii pia.hivyo Serikali iangaliw namna ya kufanya kutengeneza daraja.
Pendo Mkama Mkazi wa Pasiansi wilayani Ilemela mkoani Mwanza,amesema kuwa wamekwama katika eneo hilo kwa takribani saa moja hali ambayo imesababisha msongamano wa magari na watu kuwa wengi ukizingatia ana mtoto mdogo,hivyo ameiomba Serikali kufanya jitihada za kutengeneza daraja hilo.
Moses Andrew,amesema kutokana na hali hiyo kumekwamisha shughuli ikiwemo wajasiriamali wa dagaa ambao uchukua bidhaa hiyo mwalo wa Mkuyuni huku wengine wakuchelewa kufika katika maeneo yao ya kufanyia kazi.

Naye Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza Wilbroad Mutafungwa, amesema usiku wa kuamkia Aprili 8,2025, kulikuwa na mvua kubwa ambayo imenyesha jijini Mwanza na matokeo yake ni kuvunja daraja la Mkuyuni,ambalo limekuwa korofi kwa muda mrefu lakini sasa lipo katika matengenezo.
“Udongo umeondolewa katika barabara hii kwa sababu ya kasi kubwa ya maji ya mafuriko yaliokuwa yakapita kwenye hili daraja.Jeshi la Polisi baada ya kupata taarifa hizo,tumefika hapa alfajili kwa ajili ya kuweka hali ya usalama kwa watu wanaotumia barabara,”.
Hata hivyo amesema,katika kulinda watumiaji wa barabara hiyo wameelekeza magari yanayotoka njia ya Shinyanga kuelekea jijini Mwanza yatumie barabara ya Usagara-Kisesa kwa ajili ya kufika katikati ya Jiji pamoja na barabara ya Sahwa.Huku magari yanayotoka Mwanza kwa ajili ya kuelekea barabara ya Shinyanga watumie barabara ya kuelekea wa Magu watokezee Usagara na kuendelea na safari.
“Tumeelekeza hivyo lengo letu wakati tunaendelea kuweka hali ya usalama kwa watu wanaotumia barabara,kusitokee msongamano mkubwa ambapo tutashindwa kufanya kazi yetu vizuri,tumeweza kuruhusu watembea kwa miguu kuvuka pande zote mbili pamoja na bodaboda kwa ajili ya kusaidia raia kuvuka upande mmoja kwenda mwingine katika daraja hili,’.
Mutafungwa amesema licha ya changamoto hiyo katika eneo hilo mpaka muda huo hawajapata taarifa ya tukio lolote la mtu kupoteza maisha au kujeruhiwa kwa namna yoyote na mafuriko hayo.

Kwa upande wake Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania(TANROADS) Mkoa wa Mwanza, Mhandisi Ambrose Pascal,amesema kutokana na ujenzi wa reli ya kisasa unaoendelea,umesababisha maji kupita sehemu moja ambayo zamani yalikuwa yanatawanyika.
“Maji hayo yanatoka maeneo ya Fera na milimani, yote yanapita kwenye daraja la Mkuyuni,hivyo kuwa mengi na kupita juu ya barabara.Serikali kwa kuona hilo imeweza kutupatia fedha mwaka huu wa 2024/25, takribani bilioni 5, kwa ajili ya kujenga daraja hilo upya,ili kuondoa adha ya mafuriko yanayotokea mara kwa mara.Mkandarasi ameisha anza kazi kwa kunyanyua tuta la barabara ambayo itapanda juu angalau kwa mita 1.7,”amesema Ambrose.
Hata hivyo amesema muda wa mkataba wa utekelezaji wa mradi huo ni mwaka mmoja na ulianza Novemba 2024 hivyo wanatarajia Novemba,2025 mradi utakamilika.
More Stories
Polisi kuchunguza madai ya mwanafunzi kutupa kichanga chooni
Sekiboko ahimiza uwekezaji Elimu ya ufundi
Wazee wawili jela maisha kwa kubaka na kulawiti