December 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mafunzo ya Gasshuku 2020 kufanyika Ruvuma

Na Yusuph Digossi, TimesMajira Online

UONGOZI wa Chama cha Mchezo wa Karate Tanzania JKA/WF-TZ umeandaa semina ya mafunzo ya mchezo huo (Gasshuku 2020) yatakayofanyikia Songea Mkoani Ruvuma kuanzia Desemba 4 hadi 6 mwaka huu.

Semina hiyo ambayo imekuwa ikifanyika kila mwaka katika Mikoa mbalimbali, mwaka jana ilifanyikia katika Mkoa wa Morogoro huku lengo kuu likiwa ni kuangalia viwango vya makarateka hapa nchini.

Mkufunzi Mkuu wa Karate Tanzani (J.K.A), Jerome Mhagama amesema, mafunzo hayo ya siku tatu yatahusisha watu wa kada mbalimbali wakiwemo walimu na wanafunzi.

Ujumbe mkuu katika mafunzo hayo ni kuhamasishana na kufanyia tathmini viwango vyao vya Karate ikiwemo kutengeneza ujirani mwema wa klabu moja na nyingine.

Mkufunzi huyo amesema kuwa, jambo kubwa kwa sasa ni kuwahamasisha watu mbalimbali kujiunga kushiriki mashindano hayo kwani hayatakuwa na kiingilio.

Sababu kubwa za kufanyia mafunzo hayo Ruvuma ni kuhasasisha kuundwa kwa klabu mbalimbali za mchezo huo na kuhamasisha jamii kupenda Karate.

“Sisi kama Makarateka kutoka klabu zote Tanzania, tutakutana katika mafunzo hayo ya pamoja kuelimishana mambo mbalimbali yanayohusu taaluma yetu, ” amesema Mhagama.