Na Moses Ng’wat,Timesmajiraonline,Mbozi.
MADIWANI katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi wamemtaka Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Abdalla Nandonde,kufanya utaratibu wa kuliwekea kifaa maalumu cha kusukuma mawimbi ya mawasiliano ya kijiografia (GPS) mtambo wa kuchimba (Excavator) ili kusaidia kupata taarifa za wakati kuhusu mahali na mwenendo wa utendaji kazi wa mtambo huo na hivyo kurahisisha ufuatiliaji na kudhibiti mapato.
Madiwani wametoa wito huo, Januari 25, 2024 katika kikao cha baraza kilichoketi katika ukumbi wa Halmashauri kwa ajili ya kupitisha mapendekezo ya makisio ya mpango na bajeti kwa mwaka wa fedha 2024/25.
Diwani wa kata ya Halungu, Maarifa Mwashitete,akichangia kwenye taarifa ya maoni ya kamati ya fedha, amesema mtambo huo ni chanzo kizuri na kinauwezo mkubwa wa kuchechemua mapato ya Halmashauri kama kitafuatiliwa na kusimamiwa vizuri.
“Hapa tunatakiwa tutengeneza mpango mkakati maalumu kwa kutumia akili kubwa sana ili sisi tuweze kuziona fedha…chanzo hiki ‘Excavator’ ni kizuri sana kwani tukitumia akili ya ziada kwa kufunga GPS mapato yataongezeka” alisema Mwashitete na kuungwa mkono na madiwani wenzake.
Katika makisio ya mpango na bajeti, Halmashauri hiyo inatarajia kukusanya kiasi cha shilingi milioni 250 kutoka katika chanzo hicho cha mtambo wa ‘excavator’ kutoka kiasi cha shilingi milioni 150 kilichokadiriwa hapo awali.
Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi katika mwaka 2022/23 ilitumia kiasi cha shilingi milioni 500 kununua mtambo huo kwa ajili ya shughuli mbalimbali za Halmashauri hiyo, pamoja na kulikodisha na kuwa moja ya chanzo cha mapato.
Akifunga kikao cha baraza, Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, George Msyani, amesema katika mwaka wa fedha 2024/25, Halmashauri hiyo inatarajia kukusanya na kutumia kiasi cha shilingi bilioni 71,682,165,500.
Akifafanua Zaidi, Msyani amesema kati ya makisio hayo ya bajeti, kiasi cha shilingi bilioni 48.11 ni fedha za ruzuku kutoka serikali kuu kwa ajili ya mishahara, wakati kiasi cha shilingi bilioni 6.62 ni fedha za makusanyo ya ndani.
“Halmashauri katika mpango huu wa bajeti imetenga kiasi cha shilingi bilioni 1,945,696,000 ambazo ni sawa na asilimia 40 kwa ajili ya kuchangia katika miradi ya maendeleo” amefafanua Zaidi Msyani.
More Stories
TAG yampongeza Rais Samia
CCM Tabora yamfariji mjane wa kada anayedaiwa kujiua
FDH yaanza kutekeleza mradi wa kuwajengea uwezo wanawake wenye ulemavu