Na Yusuph Mussa,Timesmajiraonline,Korogwe
BAADHI ya Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe mkoani Tanga wamemtaka Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) kutafuta fedha ili kukamilisha miradi ya maji kabla ya Uchaguzi Mkuu, mwaka huu.
Wamesema kwa wananchi maji ni siasa, hivyo kama miradi ya maji haitakamilika kwenye maeneo yao, kuna watu watatumia nafasi hiyo kuwachonganisha wao, Serikali, na Chama Cha Mapinduzi (CCM), kuwa wameshindwa kutimiza ahadi ya kumtua Mama ndoo kichwani.
Wameyasema hayo Februari 19, 2025 wakati wanachangia makisio ya bajeti ya RUWASA kwa mwaka wa fedha 2025/2926 yaliyowasilishwa na Kaimu Meneja wa RUWASA Wilaya ya Korogwe Mhandisi France Malya kwenye kikao cha Baraza la Bajeti la Madiwani Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe.

“RUWASA tunawaomba mtafute fedha ili kukamilisha miradi ya maji kwenye maeneo yetu. Kwetu sisi maji ni siasa. Kuna watu wamejipanga kuweza kuwapotosha wananchi juu ya Serikali yao iwapo miradi hiyo haitakamilika hadi Uchaguzi Mkuu.
“Pia, naunga mkono jitihada za Serikali ya Awamu ya Sita ya Dkt. Samia Suluhu Hassan kutuwekea bajeti ya sh. bil. 19.9 kwa mwaka 2025/2026, lakini fedha hizo zipelekwe kwa Wakandarasi kwa wakati, tusije tukaumizwa kwenye Uchaguzi Mkuu kwa watu kuelezwa kuwa mmedanganywa” alisema Idd Shebila Diwani wa Kata ya Makumba.
Shebila alisema kuna tatizo kwenye baadhi ya Vyombo vya Watoa Huduma ya Maji ngazi ya Jamii (CBWSO’s), kwani viongozi wake hawasomi mapato na matumizi, hivyo wananchi hawajui mapato na matumizi kwenye vyombo hivyo. Na kutaka kuwe na sheria za kuwalazimisha wafanye Mkutano Mkuu wa kila baada ya miezi mitatu
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe Sadick Kallaghe akichangia bajeti ya RUWASA, alisema ili kuweza kupata ufanisi, RUWASA waweke mabango kwenye vyanzo vya maji, huku wakipanda miti kwenye vyanzo hivyo ili viwe endelevu.
Kallaghe aliongeza kuwa, halmashauri hiyo maeneo mengi wanatumia maji ya mserereko, lakini kwenye maeneo ambayo hayana vyanzo, RUWASA wapeleke gari la mitambo ya kuchimba maji kwenye visima virefu.
Akisoma rasimu ya bajeti, Mhandisi Malya alisema katika mwaka wa fedha 2025/2026, RUWASA Wilaya ya Korogwe inatarajia kutekeleza miradi 28 yenye thamani ya sh. 19,950,639,282.
Malya alisema katika mwaka wa fedha 2024/2025, wanatarajia kutekeleza miradi ya maji 10 yenye thamani ya sh. 4,270,715,199, na itahudumia wananchi 38,318 katika vijiji 15.

“Miradi inayoendelea kutekelezwa hadi Desemba, 2024. RUWASA Wilaya ya Korogwe imeweza kuendelea na utekelezaji wa miradi ya maji 12 yenye thamani ya sh. 13,915,311,470 ambayo itahudumia vijiji 30 vyenye wananchi wapatao 66,116.
“Ambapo miradi hii ikikamilika, itaongeza hali ya upatikanaji wa huduma ya maji kutoka asilimia 67 ya sasa hadi kufikia asilimia 85.9 ikiwa ni ongezeko la asilimia 0.9 ya lengo la Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2020-2025” alisema Mhandisi Malya.
Mhandisi Malya alisema tangu Rais Dkt. Samia kuingia madarakani Machi 19, 2021 hadi Oktoba, 2024, RUWASA Wilaya ya Korogwe imefanikiwa kukamilisha jumla ya miradi ya maji 14 yenye thamani ya sh. 6,039,208,852, ambapo vijiji 33 vyenye wananchi 65,217 wanapata huduma ya maji, na imeweza kuongeza hali ya upatikanaji wa maji kutoka asilimia 63.6 hadi kufikia asilimia 67 ya sasa.
“Katika mwaka wa fedha 2024/2025, RUWASA Wilaya ya Korogwe imekamilisha utekelezaji wa miradi sita yenye thamani ya sh. 1,374,567,035, na inahudumia watu 16,267 katika vijiji vinane (8). Na katika mwaka wa fedha 2023/2024, RUWASA Wilaya ya Korogwe imekamilisha utekelezaji wa miradi sita yenye thamani ya sh. 2,045,399,927, na inahudumia watu 26,388 katika vijiji vitano ” alisema Mhandisi Malya.


More Stories
Serikali ,Washirika wa Maendeleo waweka mkakati utekelezaji Dira ya 2050
Dkt.Mpango aipongeza STAMICO kuwa mfano bora utekelezaji matumizi nishati safi ya kupikia
Wezi wa mapato manispaa Tabora kukiona cha moto