*Regina asisitiza kuanza na changamoto ya miundombinu Pasiansi
*Ndaro kuanza na sekta ya afya
Na Judith Ferdinand, Timesmajira Online-Mwanza
Baada ya kula kiapo baadhi ya Madiwani wa Halmashauri ya Manispaa Ilemela,wameeleza namna walivyojipanga kuhakikisha wanawatumikia wananchi wa Kata zao katika kipindi cha miaka mitano ya uongozi wao.
Hayo wamebaisha Novemba 2,2025, katika mkutano wa kwanza wa Halmashauri ambao umehusisha Madiwani kula viapo,uchaguzi wa Meya, Naibu Meya na wajumbe wa kamati za kudumu,kuunda kamati za kudumu za Halmashauri.
Pia kupitisha ratiba ya vikao vya halmashauri na kamati za kudumu pamoja na kupokea taarifa ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya utekelezaji wa shughuli za halmashauri zilizofanyika kipindi ambacho Baraza la Madiwani lilivunjwa.

Diwani wa Kata ya Pasiansi Regina Lubala,amesema wamekula kipao kwa ajili ya kwenda kuwatumikia wananchi,hivyo ametoa wito kwa wananchi kuwapatia ushirikiano.
“Tunapokwenda kuwatumikia wananchi tunaomba watusaidie,watupe ushirikiano na sisi tutatoa ushirikiano kwa sababu kazi yetu kubwa ni kwenda kuleta maendeleoa ya Kata zetu na hatimaye Wilaya nzima ya Ilemela,”amesema Regina na kuongeza:
“Nawahidi wananchi wa Kata ya Pasiansi utumishi uliotukuka,nitakuwa mnyenyekevu kwao,nitajitoa kwa nguvu zangu zote,ninaamnini watakapo nipa ushirikiano nitatoa ushirikiano na kazi zitakwenda vizuri,”.
Amesema changamoto kubwa katika Kata ya Pasiansi ni miundombinu ya barabara na ndio kipaumbele chake cha kwanza ambacho anakwenda kushughulikia.
“Yapo matatizo mengine lakini kubwa ni miundombinu ya barabara,najua wakati mwingine Serikali bajeti yake inakuwa ndogo,lakini kwa kushirikiana na wananchi tutakwenda kurekebisha miundombinu ile na ninaamnini Kata ya Pasiansi itakwenda kuwa juu sana,”amesema Regina.
Diwani wa Kata ya Kitangiri, Donald Ndaro,ameahidi kuwatumikia wananchi wa Kata hiyo kwa kusimamia masuala ya huduma na ustawi wa jamii huku akisisitiza kuwa kipaumbele chake ni kutatua changamoto mbalimbali katika maeneo ya afya, elimu na maendeleo.
Amesema baadhi ya miradi itakayopewa kipaumbele ni kukamilisha kituo cha afya cha Kitangiri pamoja na kuimarisha huduma za afya ngazi ya mtaa.
“Tuna mradi wa kituo cha afya cha Kata yetu, ambao haujakamilika na ni kiporo, lazima tuendelee kukamilisha miradi viporo pamoja na maendeleo mengine. Tutaendeleza kituo cha afya ambacho kipo hatua ya renta,kwaio kikao cha kwanza cha Baraza nitakumbusha bajeti ya kwenda kumalizia kituo hicho,”amesema Ndaro.

Kwa upande wake,Mwenyekiti wa Kamati ya Elimu na Afya,Diwani wa Kata ya Shibula,Dede Swila, amesema wakazi wa eneo hilo wanapaswa kuwa na imani na uongozi uliopo kwani utasimamia kwa karibu miradi ya maendeleo.
Amesema,wataweka mkazo kwenye, kusimamia miradi ya elimu,kuboresha miundombinu ya shule na kukamilisha ujenzi wa madarasa na shule mpya ikiwemo Semba pamoja na kusaidia upatikanaji wa zahanati mpya.
“Tumejenga zahanati nne katika kata ya Shibula na tunaendelea kuboresha huduma kwa wananchi. Lengo ni kuhakikisha hakuna mwanafunzi anayekosa mazingira bora ya kusomea,” amesema Swila.


More Stories
Usajili wa Laini za Simu: Jilinde Dhidi ya Kutumiwa Vibaya kwa Utambulisho Wako
TTCL yaadhimisha siku ya Wanawake kwa kutoa msaada JKCI
Wananchi Dodoma washauri TBA kujenga nyumba za kupangisha watu binafsi