December 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Madiwani halmashauri ya mji wa Korogwe wamshukuru Rais Samia kuhamasisha utalii

Na Hadija Bagasha, TimesMajira Online, Manyara

MADIWANI wa halmashauri ya mji wa Korogwe, wamesema kitendo hatua ya Mhe. Rais kutembelea na kuhamasisha utalii wa ndani kwenye hifadhi za Taifa kinapaswa kuendelezwa na watendaji ili kuvutia watalii wa ndani na nje ya nchi kwa maslahi ya Taifa.

Madiwani hao wametoa kauli hiyo wakati walipofanya ziara ya kutembelea hifadhi ya Taifa ya Tarangire na katika Mkoa wa Manyara na Mkomazi.

Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Fransis Komba alisema hatua hiyo inaunga mkoni jitihada za Mh Rais Samia Suluhu Hassan za kuhamasisha utalii wa ndani wenye lengo la kuongeza mchango wake kwenye pato la Taifa.

Komba alisema jamii kwa ujumla inapaswa kujenga utamaduni wa kutembelea vivutio vya ndani na kubadilisha utamaduni kuwa wanaopaswa kutembelea hifadhi kujionea wanyama na vitu vingine ni watalii kutoka nje ya nchi.

Kwa upande wake makamu mwenyekiti wa halmashauri hiyo,Neema Kingoso amezitaka halmashauri nyingine nchini kwa upande wa madiwani kuweka safari ya kutembelea hifadhi huku wakitumia majukwaa yao ya kisiasa kuutangaza utalii wa ndani.

Naye diwani wa kata ya Magunga Idd Kabwele alisema pamoja na mambo mengine amefurahishwa kuona tembo wakubwa wengi kwa makundi na kwamba wapo watanzania ambao hawajui upekee wa hifadhi hiyo.

Diwani Iddy alisema wao kama waheshimiwa madiwani kitendo cha kutembelea kwenye hifadhi hiyo kimewatia nguvu baada ya kuchoshwa na majukumu ya kuwahudumia wananchi kwa kipindi kirefu kwenye maeneo yao.

Diwani wa kata ya Kwamsisi,Nasoro Hassan alisema Tarangire kwake inakuwa ni mbuga ambayo anaamini watanzania wengi wakiitembelea wanaweza kujivunia mara tu baada ya kujionea wanyama na ndege wa aina mbalimbali waliopo kwenye hifadhi hiyo.

Kwa upande wake Frank Royal ,mkazi wa nchini Holand na Konie Royakishi mkazi wa nchini Holand walisema hifadhi hiyo imekidhi hitaji lao la kuja nchini Tanzania.

Mbali na Tembo kwenye hifadhi ya Tarangire ,wanaya wengine wanaopatikana ni Pundamilia ,Nyumbu,Swala ,Simba,Nyati na Kongoni.

Wengine ni kama vile Chui,Duma, sambamba na aina za ndege zipatazo 550.