Na David John,Timesmajiraonline
MEDEREVA nchini wameshauriwa kutimiza wajibu wao kwa kufuata sheria za usalama barabarani ili kuepusha ajali ambazo zimekuwa zikisababisha ulemavu wa kudumu na wakati mwingine vifo miongoni mwa Watanzania.
Ushauri huo umetolewa leo jijini Dar es Salaam wakati wa uotoaji wa elimu ya usalama barabarani kupitia Mahakama Kifani(Mahakama ya Watoto) inayotoa hukumu kwa madereva waliovunja sharia maeneo ya shule ambayo imeratibiwa na Shirika la Amend kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama barabarani.
Akizungumza baada ya kutolewa elimu hiyo iliyokuwa na lengo la kuwakumbusha madereva kuzingatia sheria , Mkaguzi Msaidizi wa Polisi katika Makao Makuu ya kikosi cha Usalama Barabarani Faustina Ndunguru amesema kumekuwa na changamoto kubwa ya ajali za barabarani ambazo nyingi zinasababishwa na watumiaji wa vyombo vya moto hususaan madereva kutozingatia sharia za usalama barabarani.
“Tunaelekea katika wiki ya usalama barabarani duniani, hivyo Jeshi la Polisi kikosi cha Usalama barabarani kwa kushirikiana na Shirika la Amend tumeamua kutoa mafunzo ya usalama barabarani kwa wanafunzi wa shule za msingi ikiwemo Shule ya Msingi Kisiwani.Lengo letu ni kuwakumbusha madereva kuzingatia sheria za usalama barabara hasa maeneo ya shule ambayo kunakuwa na idadi kubwa ya watoto waovuka barabara.
“Huwa tunasema barabara inaongea maana dereva anapokuwa anaendesha gari kila kitu kinamuelekeza , kama kuna eneo la wavuka kwa miguu ataona alama, kama kuna kona, au ni eneo la kuvuka wanyama lazima utaona alama, lakini pia hata mwendo gani wa kutembea upo kwenye vibao, hivyo wahahakikishe wanafuata sheria,”amesema Nduguru
Amesisitiza Tanzania bila ajali inawezekana, hivyo madereva watimize wajibu wao huku akitumia nafasi hiyo kueleza Mahakama ya Watoto imekuwa na mafanikio makubwa kwani kupitia elimu ambayo wanafunzi wameipata wamekuwa na uwezo mkubwa wa kuhoji madereva wavunja sharia na kuchukua hatua na wote ambao wamekuwa wakifikishwa kwenye mahakama hiyo wanakiri na kula kiapo cha kutovunja sheria.
Kwa upande wake Meneja Programu wa Shirika lisilo la kiserikali la Amend Neema Swai amesema kuwa kwa sasa wanaendelea na utafiti wa kisayansi kubaini elimu ya usalama barabarani inayotolewa kwenye programu ya Mahakama Kifani imekuwa chachu ya kupunguza ajali kwa kiwango gani huku akisisitiza matarajio yao ni kuhakikisha elimu ya usalama barabarani inafika katika maeneo mengi ya shule kwani tangu imeanza mwaka 2018 imekuwa na mafanikio.
“Shirika letu la Amend kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama barabarani tumekuwa tukitoa mafunzo kuhusu elimu ya usalama barabarani kwa kuwakumbusha madereva na watumiaji wengine wa barabara kwamba wakifuata sharia tunaweza kupunguza ajali kwa kiwango kikubwa.
“Hivi sasa tunaelekea kwenye Maadhimisho ya Wiki ya usalama barabarani kimataifa na sisi kama Amend kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi tunao wajibu wa kutoa elimu kwa vitendo kupitia program ya Mahakama Kifani kupitia wanafunzi ambao wamepata elimu hiyo na sasa wanapeleka ujumbe kwa jamii,”amesema Swai.
Awali baadhi ya madereva ambao wameshiriki katika utoaji wa elimu hiyo kupitia Mahakama ya Watoto wameeleza namna ambavyo elimu inapaswa kuendelea kutolewa kwa madereva ili kuhakikisha watembea kwa miguu hasa wanafunzi kwenye maeneo ya shule wanakuwa salama.
Kwa upande wa Wakili Salome Masaga amesema kuwa amefarijika kuona jitihada ambazo zinachukulia na wadau hao katika kutoa elimu na kwamba kumekuwepo na ajali nyingi za barabarani ambazo nyingi zinatokana na madereva kutofuata sharia za usalama barabarani.
Dereva Babaji anayefanya safari zake kati ya Feri na Kisiwani wilayani Kigamboni Emmanuel Masimo amesema kitendo cha kushindwa kusimama eneo la wavuka kwa miguu na kupelekwa kwenye Mahama ya Watoto amejisikia aibu lakini imempa somo kwamba lazima sharia ya barabarani izingatiwe, hivyo atakuwa balozi mzuri kwa madereva wenzake.
Mkazi wa Kigamboni Paul Makanja amesema kitendo Cha wanafunzi kuwa na uelewa mpana kuhusu sheria za barabarani itasaidia kupunguza ajali za barabarani huku akitumia nafasi hiyo kueleza Iko haja ya elimu ya usalama barabarani kuwafikia watu wengi zaidi na hiyo ni njia mojawapo.
Wanafunzi wa Shule ya Msingi kisiwani Maria Chacha, Saimon Abdallah na Nuru Issa ambao walikuwa sehemu ya mahakimu katika Mahakama ya Watoto wameeleza kuwa ujumbe wao kubwa kwa madereva ni kuwaomba wanapopita maeneo ya shule wazingatia sheria, kwani wanafunzi ni watoto wao, hivyo hawaoni sababu ya kukatisha ndoto za watu wanaowapenda.
More Stories
Kiswaga:Magu imepokea bilioni 143, utekelezaji miradi
Zaidi ya milioni 600 kupeleka umeme Kisiwa cha Ijinga
Kamishna Hifadhi ya Ngorongoro atakiwa kupanua wigo wa Utalii nchini