Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online
“TICTS ni wazembe sana. Utendaji kazi wao ni mbovu, kuanzia asubuhi hadi sasa hivi saa sita ya usiku tumekwama hapa bandarini kutokana na ucheleweshaji wa huduma ya upakiaji wa makontena,” alisema Mohammed Abdallah, dereva wa lori la makontena, usiku wa mgomo ulipoanza.
Madereva hao, ambao wamekuwa wakigoma mara kwa mara kutokana na huduma mbovu za TICTS, wamesema miundombinu ya eneo la Kitopeni bandarini lililo chini ya TICTS ni mibovu, ikiwemo uhaba wa vyoo.
“Licha ya kucheleweshewa huduma za makontena kwa visingizio vya kreni kuharibika mara kwa mara na msongamano wa malori, kuna matundu ya vyoo mawili tu ambayo yanahudumia mamia ya madereva,” alisema Abdallah.
Siku ambayo madereva malori wameanza mgomo wao mpya, Rais Tshisekedi, ambaye nchi yake ya DRC ndiyo mteja mkubwa kuliko wote wa bandari ya Dar es Salaam, aliwasili Zanzibar kwa mapumziko binafsi kabla ya kuanza ziara rasmi ya kikazi nchini Tanzania Oktoba 23.
Moja ya shughuli ambayo Rais wa Congo alipangiwa kufanya wakati wa ziara yake nchini ni kutembelea bandari ya Dar es Salaam.
“Tunashukuru kuwa Rais Tshisekedi alipata udhuru akalazimika kukatisha ziara yake nchini, hivyo hakwenda tena bandarini Dar es Salaam. Maana kama angeenda bandarini angekutana na mgomo wa madereva malori kutokana na huduma mbovu ya TICTS na hii ingekuwa ni fedheha kubwa kwa taifa,” alisema Juma Hafidh, mdau wa bandari ya Dar es Salaam.
Hivi karibuni, wafanyakazi wa TICTS walilaumiwa kwa kudondosha makontena kwenye bahari na kufanya meli zishindwe kupita kwenda kupakua mafuta eneo la Kurasini KOJ kwa siku kadhaa na kuisababishia taifa hasara.
Kumekuwa na mlolongo wa tuhuma za uzembe na ukosefu wa ufanisi wa TICTS ambayo imekuwa ikisimamia eneo la makontena la bandari ya Dar es Salaam kwa zaidi ya miaka 20 bila tija.
Serikali ya Tanzania kwa sasa iko kwenye majadiliano na TICTS kuhusu kuongeza au kutoongeza mkataba wake, huku kampuni hiyo ikilaumiwa na wadau wa biashara na usafirishaji kwa kukosa ufanisi.
Wadau wa sekta za biashara na usafirishaji wameitaka serikali kutoipa kampuni ya TICTS mkataba mpya wa kuendesha eneo la kontena la bandari ya Dar es Salaam kwa kushindwa kufikia lengo la kuongeza wingi wa mzigo kwa asilimia 37 kwa mwaka na kuwa na ufanisi mdogo.
More Stories
Mbowe akuna wengi kuhusu maridhiano
Waziri Chana amuapisha Kamishna uhifadhi NCAA, ampa maagizo mazito
Amos Lengael Nnko afariki kwa ajali ya gari