November 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Madereva daladala,Serikali wakubaliana wiki mbili kutatua chanzo cha mgomo

Judith Ferdinand, Timesmajira Online, Mwanza

Madereva wa daladala jijini Mwanza pamoja na serikali wamekubaliana ndani ya wiki mbili kuwa wametatua changamoto ya muingiliano kati ya daladala na bajaji jijini humo.

Ambazo zimesababisha kuwepo kwa mgomo uliotokea Machi 11,2024 uliodumu kwa saa kadha na kusababisha adha ya usafiri kwa wananchi ikiwemo wanafunzi baada ya madereva hao kutofanya shughuli za usafirishaji abiria ikiwa ni njia ya kuikumbusha serikali kuweza kutatua malalamiko yao ambayo yamedaiwa kudumu kwa muda mrefu.

Akizungumza na Madereva hao Machi 11,2024 kwenye uwanja wa Furahisha kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza,Mkuu wa Wilaya ya Ilemela Hassan Masala ameeleza kuwa wanavikao ambavyo ni muendelezo wa kufikia muafa wa malalamiko ya madereva hao walioyatoa huku akieleza siyo vyema kufanya kazi kwa kuviziana katika kutoa huduma ya usafiri kwa wananchi.

“Mnapowarejeshea huduma wananchi na sisi inatupa urahisi wa kuiondoa hiyo huduma mbadala inayotumika ambayo siyo tunaitoa barabarani nyinyi wenyewe mmekubali bali tunawapangia vituo na kuwawekea utaratibu ambao siyo suala la kusema nikitoka hapa dakika kumi ukizunguka hapo usimuone mtu wa bajaji,”amesema Masala na kuongeza:

“Sisi tutawaita watu wa bajaji na tutapeana utaratibu,tukubaliane kuwa wakati tunarejesha huduma barabarani basi tupeane muda kesho haiwezekani siwezi kutoa ahadi ambao haitekelezeki hivyo tumekubaliana wiki mbili ambazo ni za kutambua vituo,kupanga bajaji ambapo mpaka Jumatano tutakuwa tumeisha fanya utaratibu wote na baada ya siku hizo tutakuwa tumekaa sawa,”.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha wa Wamiliki na Wasafirishaji abiria Mkoa wa Mwanza Yusuph Lupilya ameeleza kuwa kitendo cha leo cha kuwanyima huduma na kuwakosesha haki wananchi ni kwa sababu serikali hajachukua hatua za kusimamia sheria na kuzuia tatizo ambalo limesababisha mgomo huo.

Daladala ikisimama eneo ambalo halina kituo faini 30,000, bajaji inafika eneo la pundamilia(zebra) inachukua abiria kitu hicho kinaweza kusababisha uvunjifu wa amani.

“Sisi tulisitisha huduma kuikumbusha serikali ya Mkoa wa Mwanza ifuate sheria,LATRA imesema bajaji ni teksi inatakiwa ikae kwenye maegesho ikodishwe kama watu wanatokea Buzuruga wenye malengo mmoja wa kuja mjini ifike mjini kisha irudi kwenye kituo,”.

Mwenyekiti wa Madereva wa daladala Mkoa wa Mwanza Mjarifu Manyasi,ametoa rai kwa madereva wenzake kuingia barabarani kufanya kazi na waamini kile ambacho serikali imekisema kuwa kinaendelea kufanyiwa kazi.

“Waendelee kutoa huduma kwa wananchi kwani uongozi wa Mkoa na Wilaya unaendelea kutatua changamoto zetu na kamati ilioundwa itaanisha na kuzitatua na mikoa mingine ije kuiga kwetu,”.

Awali baadhi ya madereva hao wa daladala wameeleza malalamiko yao yaliosababisha kugoma ikiwemo muingiliano wa bajaji ambazo zimekuwa zikikiuka sheria za barabarani pia zikifanya kazi tofauti na leseni yao inavyoelekeza ya kuwa itafanya kazi kama taksi na siyo kama daladala.

Mmoja wa Dereva wa daladala hizo Richard John ameeleza kuwa ukienda Buhongwa kuna bajaji ambazo zinabeba abiria wa njia zote na zinapakia sehemu yoyote ikiwemo Mkolani,Nyegezi na kwa gharama ya shilingi 500 wakati daladala kituo hadi kituo ni shilingi 600.

Ambapo ameeleza kuwa bajaji inabeba abiria mbele ya trafki au kwenye zebra lakini hawakamatwi ila wao wanakamatwa na kuandikiwa faini ya shilingi 30000 na kuendelea.

Ameeleza kuwa mbali na changamoto ya bajaji pia wanalalamika gharama za ushuru ambazo kwa gari moja kwa siku ni 6000 mpaka 7000 huku akitokea mfano gari inayotoka Airport- Nyashishi ikifika kituo cha Kona ya Bwiru inalazimika kutoa ushuru wa 2000, ikifika stendi ya Igombe (mjini) 2000 na Nyashishi 2000 huku njia ya Nyashishi -Kisesa wanalipa Nyashishi 2000, ,Natta 2000, Buzuruga 2000 na Kisesa 1000.

“Kwa mwezi sawa na 180,000 kwa mwaka ni zaidi ya milioni 2,kwa gari moja hapa mjini kuna gari zaidi ya 1000 zinazofanya kazi,shida inaanza changamoto ya barabara Buhongwa sehemu ya kituo kikubwa cha daladala ya kushusha na kupakia abiria, sehemu ya kutokea kuna shimo ambalo lina mwezi mzima ukiiingia tu na gari utavunja spiringi na utapasua tairi,” ameeleza na kuongeza

“Nyashishi mlango wa kuingilia na kutokea barabara ni mbovu hakupitiki ,Igogo kule juu kwenye reli pale barabara imechimbika na mvua, gari zinapanda kwa shida ikiingia vibaya unapasua tairi na kukata spring,tunazungushwa Nyegezi stendi chini ule mzunguko ambao barabara yake ni mbovu wakati sisi kila siku tunatoa ushuru lakini shida hizo serikali bado haijaziona,”.

Sanjari na hayo ameeleza kilio chao kikubwa mbali na suala la bajaji pia miundombinu ya barabara iboreshe,ushuru gharama zipungue maana mwanzo ilikuwa 500 kwa 1000 ila sasa ni 1500 kwa 2000.

Hata hivyo Dereva Mwingine Hussein Hilary ameeleza kuwa katika kutekeleza makubaliano hayo ya kurejesha huduma amemuomba Mkuu wa Wilaya huyo kuwaachilia wenzao waliokamatwa na jeshi la polisi asubuhi wakati mgomo huo ilivyokuwa unaendelea.

“Tunalalamikia mfumo wa bajaji ambazo upo kinyume na leseni walizopewa na mamlaka ambazo zipo chini yako,tunachohitaji siyo kutoa bajaji ila zifuate sheria kama walivyoomba leseni kwa sababu ikikutwa gari ya Kisesa stendi ya Igombe mita 150, kutoka Kona ya Pamba unapigwa faini kuwa imekwenda kinyume na sheria,hilo ndio linawauma tumekubali kukaa njaa hata mwaka ili tuelewe hatima ya leseni zetu zinavyofanya kazi na za bajaji pia,”amesema Hussein na kuongeza kuwa

“Jiji la Mwanza bado lina nafasi kubwa ya bajaji kufanya kazi katika maeneo ambayo daladala hazifiki,Julai mwaka jana ndio mwaka mpya wa kiserikali lakini Wilaya ya Ilemela ndani ya miezi miwili mbele Septemba ushuru ulipanda,tena ndani ya miezi mitatu ushuru ukapanda,tulianza na 1000 ikaongezwa 500 mwezi wa tisa ikawa 1500 mwezi wa kwanza mwaka huu ikaongezwa mia tano ikawa 2000 na hawa unaowaona wanalipa 7000 kila siku,”.

Naye mmoja wa madereva hao alijulikana kwa jina moja la Omera ameeleza kuwa changamoto iliopo ni bajaji kuingia hadi kwenye vituo vyao vya daladala na kuanza kugombea wateja hivyo ameiomba serikali kupitia Mkuu huyo wa Wilaya kutoa tamko kuwa bajaji zisitishe huduma ya kuingia mjini wakati wakisubilia marekebisho.

“Kwa siku tuna faini ya 90,000 ukijumlisha tozo zote,ambapo ukichukua bajaji 100, hailipi kodi ya daladala moja tunaumia,sisi tumesitisha na wao wasitishe uone kama kutakuwa na madhara kwa wananchi kama ya daladala tuna maumivu ya muda mrefu,”ameeleza Omera.

Mmoja wa wananchi jijini hapa ameeleza kuwa hali hiyo imesababisha adha kwako na kutumia gharama kubwa kwenda kwenye shughuli za kujiingizia kipato.

“Nikiwa nafuata bidhaa soko la Mirongo kawaida natumia 1200 kwenda 600 kurudi 600 ila leo nimemtumia zaidi ya 2000, kwa kweli mgomo wa daladala unatuathiri sisi wananchi hasa wenye kipato cha chini naomba serikali wakae mezani na Madereva ili kutusaidia sisi,”.

Miongoni mwa daladala zilizoanza kufanya kazi baada ya makubaliano baina ya madereva wa daladala na serikali