January 9, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Madereva bodaboda wajengewa uwezo kuhakikisha elimu kuhusu kupinga ukatili imefanikiwa

Na Jackline Martin, TimesMajira Online

Chuo cha ustawi wa jamii kimetoa mafunzo ya kuwajengea uwezo madereva bodaboda Kata ya Kijitonyama ili kuhakikisha elimu kuhusu kupinga ukatili imefanikiwa.

Mafunzo hayo ya siku moja yametolewa kwa viongozi wa bodaboda 50 kwa kundi la kwanza ambapo idadi itazidi kuongezeka kwa kutoa mafunzo katika maeneo mengine ya jiji la Dar es Salaam na nje ya Dar es Salaam.

Akizungumza na waandishi wa Habari leo Jijini Dar es Salaam, Mkuu wa Chuo hicho, Dkt.Joyce Nyoni amesema kuwa mafunzo hayo endapo yatafanyiwa jitihada kwenye sehemu zao za kazi ukatili utapungua na kuisha kabisa.

“Tunaona kwamba tunasehemu ya kufanya katika kuwajengea uelewa, baada ya hapa muende mkawe mabalozi kwa madereva wenzenu”

“Kuna vitendo vingi tunavyokuwa tunavifanya lakini huelewi kama ni ukatili hadi utakapofundishwa ndiyo unajua kuwa ni ukatili hivyo mafunzo haya ya leo muendelee nayo kwenye jamii kwani tutafika kwenye sehemu zenu za kazi na kujua maendeleo yenu” Amesema Dkt. Nyoni.

Kwa upande wake Mratibu wa kitengo cha ushiriki Jamii na mafunzo kwa viongozi wa bodaboda kwa manispaa ya kinondoni,
Danstan Haule amesema mbali na mafunzo hayo kulenga zaidi kwenye masuala ya ukatili wa kijinsia lakini pia yamelenga madereva hao kuweza kujua sababu za msongo wa mawazo na namna ya kujiepusha nayo.

“Hii yote ikilenga kuongezea afya na kuwaekea mazingira mazuri ya kazi yao ili waweze kujitafutia kipato na kukidhi mahitaji yao”

“Tumekua tukiwafikia makundi tofauti tofauti ikiwemo vijana mashuleni kwenye shule za sekondari na msingi lakini pia vijana vijiweni kuhusu mambo mbalimbali ya kujiwekea akiba ya kujiandaa na maisha ya baadae n.k”

Pia amesema kundi lingine walilokusudia kulifikia ni kundi la madereva wa magari ya kubeba watoto mashuleni ambalo wanatarajia kulifikia kwa ukubwa zaidi kutokana na vitendo vya ukatili vinavyotokana na madereva hao.

“Tunaandaa programu ambayo tutahamasisha mashule yaweze kuwaleta au kuwafikia pale walipo madereva pamoja na makondakta wao kuwapa uwezo kwani kuna baadhi ya matukio ya unyanyasaji n.k vimekua vinatokea sana”

Mwenyekiti wa Bodaboda kata ya kijitonyama , John Peter amesema elimu aliyoipata chuoni hapo itawafikia madereva wote wa kata hiyo ili kuepukana na ukatili wa kijinsia katika jamii hasa kwa abiria wanaowabeba.

Naye Katibu wa Bodaboda Kata ya Kijitonyama, Mussa Julius amesema amefurahishwa na elimu iliyotolewa na chuo hiko kwani itawafanya wawe mabalozi katika vituo vyao vya kazi.

“Tutaenda kuwaelezea bodaboda wenzetu waelimike kuhusu ukatili wa kijinsia kwani ukatili upo wa aina nyingi hasa kwa sisi madereva tunakutana nao Sana”