Na Esther Macha, Timesmajira Online-Mbeya
MADEREVA 42 jijini Mbeya wamefungiwa leseni za udereva kwa kipindi cha Januarimpaka Juni ,2025 kutokana na kukiuka sheria za usalama barabarani .
Hayo yamesemwa Julai 18,2025 na Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Mbeya,Mrakibu Mwandamizi wa Polisi (SSP) Notker Kilewa,baada ya ukaguzi wa mabasi ya abiria kabla ya kuanza safari stendi kuu ya mabasi jijini Mbeya.
SSP.Kilewa,amesema kuwa Jeshi la Polisi mkoani humo, limeendelea kuwachukulia hatua za kisheria madereva wanaokiuka sheria za usalama barabarani ikiwemo kuwafungia leseni za udereva miezi mitatu,ambapo katika kipindi hicho cha miezi sita idadi hiyo ya madereva 42 wamefungiwa leseni.
Pia SSP .Notker,ametaja baadhi ya makosa hatarishi yaliosababisha madereva kufungiwa leseni ni pamoja na mwendo kasi, kuyapita magari mengine katika maeneo yasiyoruhusiwa pamoja na ulevi,hivyo amewataka madereva kutii sheria kwani Jeshi la Polisi halitakuwa na msamaha kwa dereva yeyote atakayekamatwa kwa makosa hatarishi.
Kwa upande wake Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani Naibu Kamishna wa Polisi (DCP) Fraisser Kashai, kutoka Kamisheni ya Oparesheni na Mafunzo,amewataka madereva wa mabasi ya abiria kuheshimu na kutii sheria za usalama barabarani ili kuepuka ajali,kwani atakayebainika kukiuka sheria hizo jeshi hilo halitasita kumchukulia hatua za kisheria.
Naye Ofisa Mfawidhi wa LATRA Mkoa wa Mbeya, Shaban Mdende,amesema kuwa mabasi ya abiria yamefungwa kifaa maalum cha mwenendo ambapo LATRA na Jeshi la Polisi,wamekuwa wakifanya kazi kwa ushirikiano na kufuatilia mwenendo wa mabasi kupitia mfumo wa VTS,ambapo kati ya madereva 42 waliofungiwa leseni, madereva 26 walibainika kupitia mfumo huo.
Ukaguzi uliofanywa na DCP Kashai umehusisha ukaguzi wa magari, leseni za udereva, kupima kilevi madereva na utoaji wa elimu ya usalama barabarani kwa abiria, huku lengo likiwa ni kufanya ufuatiliaji wa utekelezaji wa maelekezo yanayotolewa na kutoa elimu kwa madereva na abiria ili kuzuia na kudhibiti ajali za barabarani.

More Stories
Clara:Miaka 50 ya Sabasaba fursa mpya za Biashara na Uwekezaji
Usajili wa Laini za Simu: Jilinde Dhidi ya Kutumiwa Vibaya kwa Utambulisho Wako
TTCL yaadhimisha siku ya Wanawake kwa kutoa msaada JKCI