January 6, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Madaktari bingwa wa macho waweka kambi ndani ya Gereza la Mkoa Mbeya ,

Na Esther Macha, Timesmajira Online, Mbeya

MADAKTARI bingwa watatu kutoka nchini Ujerumani wameweka kambi katika Gereza Kuu la Ruanda Mkoa wa Mbeya kwa ajili kufanya huduma za matibabu na kiuchunguzi kwa wafungwa 150 ambao watabainika na tatizo la mtoto wa jicho kwa kufanyiwa upasuaji.

Akizungumza mbele ya Naibu Waziri wa Maji, Mhandisi Maryprisca Mahundi (Mb)ambaye ndiye mdhamini wa kampeni hiyo ,Mrakibu wa Magereza Dkt.Alex Buhinu amesema katika gereza hilo kuna changamoto ya tatizo la macho kwa wafungwa.

“Tunakushukuru Naibu Waziri na Mbunge kwa kuleta madaktari hawa kutoa huduma kwa wafungwa 150 ambapo awali tulikuwa tukilazimika kuwapeleka katika hospitali ya Rufaa ya Kanda na Mkoa kwa ajili ya matibabu ya macho, ”amesema.

Amesema ujio huo wa madaktari bingwa utarejesha matumaini kwa wafungwa ambao watabainika kuwa na tatizo la mtoto wa jicho na kufanyiwa upasuaji bure.

Mrakibu wa Magereza gereza la Ruanda jijini Mbeya Sebastian Mganga,amesema gereza hilo lina wafungwa 1,050 kati yao wapo wafungwa waliofungwa vifungo vya kawaida,mahabusu,vifungo virefu na wanafungwa wa kunyongwa .

Naibu Waziri wa Maji Mhandisi ,Maryprisca Mahundi (Mb)ambaye mdhamini wa kampeni hiyo amesema kambi hiyo maalum italenga kutoa huduma muhimu kwa jamii yenye changamoto ya tatizo la mtoto wa jicho.

‘Siku ya leo tumeweza kuwatembelea katika Gereza Kuu la Ruanda lengo ni kuonesha namna tunavyowakumbuka na jinsi tunavyowajali ndugu zetu ambao wapo kwenye vifungo mbalimbali tunacho kiamini magereza ni shule kwa wenzetu walioteleza kwenye jamii ni sehemu tu ya kurekebishana tabia na kurudishana kwenye mwendo sahihi na si kwamba ni adhabu kuwa hafai kwenye jamii na tufanya haya yote tunampa moyo,”amesema.

Mhandisi Mahundi amesema kwa kutambua hilo wakaona kambi maalum ya matatizo ya mtoto wa jicho kwa hospitali ya Rufaa ya Mbeya wakaona ni vyema wafungwa nao waguswe na matibabu hayo.

“Tunatarajia kuwafanyia uchunguzi wafungwa 150 na watakaokutwa na tatizo la mtoto wa jicho watafanyiwa upasuaji ili waweze kurejea katika hali ya usalama wa macho yao”amesema Mhandisi Mahundi.

Aidha Mhandisi Mahundi ametoa wito kwa wananchi mkoani Mbeya kuwa kambi hiyo ni ya kipekee ni maalum kwa ajili ya mtoto wa jicho na si kwa ajili ya matatizo ya macho sababu kuna matatizo mbalimbali ya macho mwingine anahitaji dawa tu na miwani ,hapa ni kwa ajili ya upasuaji wa mtoto wa jicho .

“Wakati Kambi ya macho inaendelea kumekuwa na malalamiko ya hapa na pale napenda waelewe kuwa watakaogundulika na mtoto wa jicho hao watafanyiwa upasuaji ili waweze kupatiwa tiba inayohusiana na mtoto wa jicho na si vinginevyo hivyo kwa matatizo mengine watatafuta wasaa mwingine ama huenda akaja kiongozi mwingine akasaidia hayo matatizo mengine,” amesema Mhandisi Mahundi.

Haya hivyo amewashukuru wananchi kujitokeza kwa wingi na kusema kuwa mpaka sasa wamejitokeza watu zaidi ya 1,000 ambao wamefanyiwa uchunguzi huku zaidi ya watu 200 wamefanyiwa upasuaji hayo mafanikio makubwa.

Kwa upande wake Mkuu wa idara ya macho,Daktati bingwa wa macho hospitali ya Rufaa ya Mkoa Mbeya Dkt.Raymond Mwalonde amesema kuwa kambi hiyo ilianza Agost 22 mpaka sasa wameona wagonjwa 1,600 ambao wameweza kubaini matatizo mbalimbali ya macho kati yao 140 wamefanyiwa upasuaji.

Aidha amesema kuwa wamefika Gereza Kuu la Ruanda kwa ajili ya makundi maalum ambapo walitenga siku maalum ili waweze kuwaona wafungwa wenye shida tofauti lakini pia kesho watafika shule maalum wilayani Rungwe kufanya huduma za kitatibu na uchunguzi wa macho kwa watoto.