Na George Mwigulu, Timesmajira Online,Katavi.
Madaktari Bingwa na Mabingwa bobezi 12 kutoka Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kati ya Benjamin Mkapa-Dodoma wameweka kambi maalumu ya siku tano katika Mkoa wa Katavi kwa ajili kufanya uchunguzi na matibabu ya magonjwa mbalimbali pamoja na kuwajengea uwezo madaktari wa Mkoa huo.
Utoaji wa huduma hizo za afya kwa wananchi na kuwajengea uwezo madaktari ni maelekezo ya serikali ya kuhakikisha hospitali za kanda nchini zinakwenda pembezoni kutoa huduma ya matibabu kwa wananchi na kuwapatia elimu kabla hawajapatwa na matatizo makubwa.
Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Benjamin Mkapa-Dodoma Dkt.Alphonce Chandika,ameeleza hayo 11,Sept mwaka huu katika ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Katavi, ambapo amesema wamebaini hospitali hiyo imekuwa ikihudumia wagonjwa kutoka mikoa mingine nje ya kanda ya kati ikiwemo Katavi.
Mkurugenzi huyo amesema kuwa wanatarajia kutoa huduma za uchunguzi na matibabu kwa magonjwa ya figo,kisukari,shinikizo la damu, kiharusi,matatizo ya macho,masikio,pua na koo pamoja na usuaji wake,upasuaji wa mifupa salama,magonjwa ya mfumo wa chakula na magonjwa ya mifupa na ajali huku zaidi ya watu 450 wakitarajia kuwafikia.
Uchunguzi na matibabu mengine ni magojwa ya mfumo ya mkojo na nguvu za kiume,matatizo ya afya ya uzazi,wajawazito wenye changamoto mbalimbali ya uzazi,matibabu na uchunguzi wa magonjwa ya watoto ikiwemo magonjwa ya moyo kwa watoto pamoja na kuona wangonjwa wenye matatizo ya mishipa ya fahamu,upasuaji wa watoto wenye vichwa vikubwa na migogo wazi.
Dkt Chandika amefafanua kuwa licha ya kutoa huduma hizo lakini wanatumia fursa ya kutangaza huduma zinazotolewa na hospitali ya Benjamin Mkapa kwani huduma zote za kibingwa zinapatikana huku wakiendelea kuimarisha zaidi huduma za ubingwa bobevu (Super Specialist) na ikiwa hospitali ya pili nchini kwa upandikizaji wa figo.
“Serikali imewekeza sana na hivi karibuni tumeanzisha huduma pekee zinazotolewa hapa nchini na ukanda wa Afrika myashariki na Kati ikiwemo upandikizaji wa uroto,kuhudumia watoto wenye selimundu,tumeishaanza na ulizinduliwa na Waziri Mkuu na tunaendelea kutoa huduma,”amesema Dkt. Chandika.
Aidha katika hatua nyingine amesema serikali kupitia fedha za UVIKO-19 imeimarisha matumizi ya tehama kwenye kuboresha huduma za afya yaani tell medicine ambapo katika hosptali ya Benjamin Mkapa wamefungiwa vifaa hivyo kiasi kwamba wataalamu wanaweza kuzungumza kwa umbali mrefu wakati wanamtibu mgonjwa.
“Uwekezaji na uhusiano huu tulioanzisha umelenga kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora ili afya zao ziimarike waendelea kufanya kazi za kuzalisha mali na kukuza uchumi wao,”amesema Dkt Chandika.
Mkuu wa Mkoa wa Katavi,Mwanamvua Mrindoko amewapongeza madaktari wa hospitali ya Benjamin Mkapa kwa kazi nzuri ya kuwahudumia wagonjwa wanaotoka Mkoa huo kwani wamekuwa wakisifia huduma bora kutoka kwao.
Mrindoko ametoa ahadi kuwa madaktari hao watapewa ushirikiano mkubwa wa kuhakikisha wanafanikisha zoezi la utoaji huduma za afya kwa wananchi sambamba na kuhakikisha madaktari wa hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Katavi wanashiriki vema kwenye mafunzo ya kuongezewa uwezo.
Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Katavi Dkt.Damiani Maruba ameeleza kuwa ujio wa wataalamu hao utawasaidi wao kuweza kujiongezea utaalamu zaidi ambao hawakuwa nao awali .
Aidha amesema hospitali hiyo haina wataalamu mbalimbali kama vile wa watoto ,figo magonjwa ya ndani , mtaalamu wa magonjwa ya ufahamu mtaalamu mbobezi wa mfumo wa chakula.
Dkt Maruba amesema kwa timu hiyo ya madaktari inatarajiwa kufanya kazi katika Mkoa wa Katavi kwa muda wa siku tano ambao kwa siku ya kwanza wameweza kujitokeza watu zaidi ya 150.
More Stories
Waziri Jerry afanya uteuzi wa Makamu Mwenyekiti, Wajumbe watano wa bodi ya Shirika la Posta
Kapinga atoa maagizo TANESCO ,kuhusu Vijiji vinavyolipia gharama ya mijini kuunganisha umeme
Ukiukaji wa Uhuru wa Kidini na Kutovumiliana Huzusha Malumbano ya Kimataifa