June 26, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Machinga jijini Mwanza wazua taharuki kwa kuandamana na kupiga mawe

Na Judith Ferdinand, TimesMajira Online Mwanza

Watu wanaodaiwa ni wafanyabiashara ndogo ndogo maarufu kama machinga jijini Mwanza wamezua taharuki baada ya kuandamana katika baadhi ya mitaa na kupiga mawe maduka.

Hali hiyo ambayo imesababisha sinto fahamu kwa wafanyabiashara wa maduka na wakazi wa mitaa hiyo iliopo katikati ya Jiji la Mwanza mpaka pale Jeshi la Polisi lilipoingia mtaani na kujaribu kutuliza hali hiyo ya vurugu.

Baadhi ya wafanyabiashara wa maduka wapo waliolalamika kuibiwa baadhi ya vitu na kupondwa mawe.

Hata hivyo machinga hao kilio chao kikubwa wameomba kurejesha katika maeneo hayo ya awali ya kufanyia biashara ili waweze kuendeleza biashara zao.

Mmoja wa machinga Chausiku Mwita, ameeleza kuwa kitu kinachopaswa kufanyika ni Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana pamoja na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza kukaa pamoja na wapange maeneo ya wafanyabiashara rasmi.

Ambapo wameomba wameneo ambayo wanahitaji yatengwe kwa ajili ya wao kufanya biashara ni Makoroboi,Dampo,Sahara na Kariakoo.

Pia ameeleza kuwa wale wa round about ya Nyerere walindwe wasipange bidhaa kama wanaone sehemu hiyo ni hatari kwa wafanyabiashara.

Ameeleza kuwa kilochotokea Leo muda wa saa nne yeye alikuwa ameleta chai ambayo uwa anapikia nyumbani na kuuza kwa wateja hivyo alivyotetemka chini kwa wauza nguo za mitumba alikuta machinga wamejikusanya,defenda imepaki na mgambo na gari lao wamepaki akauliza kuna nini wakaanza kusema twendeni twendeni.

Yeye akiondoka kuendelea kuhudumia wateja wengine wa chai muda kidogo akasikia mawe watu wanakimbizana alivyouliza kuna nini akaambiwa ni mgambo na machinga, kinachofanya watu wanapigana ni njaa kama umeshiba uwezi kupigana

“Mtu akija anatuambia pangeni,akija Gwajima pangeni,akija Mkuu wa Wilaya anakataa mgambo anawakimbiza sasa tunaenda wapi na tunatoka wapi,sisi tuna watoto wanasoma,watoto hawasomi na hawaendi shuleni ela hamna hali ni ngumu na bado watuone na sisi ni wazazi,”.

Naye machinga ambaye alitambulika kwa jina la Prosper, ameeleza kuwa changamoto iliojitokeza katika siku hiyo ya jana kwanza kabisa ni njaa,maisha yameharibika sana.

“Maisha ya machinga sasa hivi yanebadilika sana ni njaa,tuna mwaka mzima tumetolewa Makoroboi na kupeleka katika masoko yale,hakuna biashara unaweza kukaa wiki nzima ukawa umepata mteja mmoja tu,unafamilia watoto wanaenda shule, utapata ridhiki kweli,” ameeleza Prosper.

Pia ameiomba serikali iwarejeshe katika maeneo hayo kwa kutenga muda wa kufanya biashara angalau kuanzia muda ya jioni ili machinga hao waweze kupata ridhiki.

Akizungumzia sakata hilo kwa waandishi wa habari,Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza Wilbroad Mutafungwa, ameeleza Februari 8, mwaka huu majira ya saa 3,asubuhi mtaa wa Makoroboi, Nyerere Square na mtaa wa Lumumba wilayani Nyamagana mkoani Mwanza Askari wa Jeshi la Akiba maarufu mgambo chini ya uongozi wa Jiji la Mwanza walikuwa katika operesheni ya kuzuia wafanyabiashara ndogo ndogo maarufu kama machinga kufanya biashara zao katika maeneo ambayo hayaruhusiwi.

Mutafungwa ameeleza kuwa,wakati mgambo hao wakiendelea na kazi hiyo ambayo wanaofanya kila siku kuanzia asubuhi mpaka jioni.

Na wakati wakiendelea na kazi hiyo ndipo kundi la vijana ambao wanasadikika kuwa ni wafanyabiashara ndogo ndogo (machinga),walianza kuwarushia mawe mgambo,ili kuwazuia wasitekeleze kazi yao ya kuwaondoa machinga kwenye maeneo hayo ambayo kimsingi tayari yameisha katazwa kufanyia biashara hizo ndogo ndogo.

“Katika kundi hilo la machinga pia limeingia kundi la vijana ambao ni wadogo wadogo bado tunafuatilia ni wahalifu pia,ambao walushirikiana na machinga na kuongeza kundi kubwa la watu wakiwa wanarusha mawe ambayo yameweza kuleta uharibifu kwenye magari,” ameeleza Mutafungwa.

Ambapo ametaja magari yaliopata uharibifu ni kuwa gari moja limeharibiwa kioo cha mbele namba SU 43732, Toyota Land Cruise,mali ya Shirika la Viwango Tanzania na gari namba T 974 aina ya Toyota mali ya mtu anayeitwa Ferdinand Makombe.

Mutafungwa ameeleza kuwa,thamani ya uharibifu huo bado haijafahamika kwa sababu wanaendelea kufanya uchunguzi huku katika tukio Hilo hakuna madhara kwa binadamu yaliojitokeza mpaka muda huo anaotoa taarifa hawajapata taarifa ya mtu yoyote aliye umizwa au kupata madhara kufuatia sinto fahamu hiyo iliyojitokeza.

“Mara baada ya Jeshi letu kupata taarifa kupitia wafanyabiashara waliopo mjini na Askari wetu waliokuwa doria,mara moja walitanda katika maeneo hayo kwa ajili ya kuongeza ulinzi na usalama,”ameeleza.

Ameeleza kuwa kwa juhudi walizofanya jeshi hilo waneweza kuzima vurugu hizo zilizosababishwa na kundi la vijana hao na kuweza kutawanya kabisa vijana hao waliotaka kuleta fujo kubwa.

Pia ameeleza kuwa katika tukio hilo wamefanikiwa kuwakamata vijana wawili ambao ndio walionekana ndio viongozi wa kundi hilo la kimachinga walioanzisha vurugu hizo,na wanahojiwa kuhusiana na tukio hilo na majina hayo yamehifadhiwa kwa sababu za kiupelelezi.

Aidha ameeleza kuwa Jiji la Mwanza katika mitaa hiyo yote,imedhibitiwa hli ya usalama ipo vizuri na wafanyabiashara wanaendelea kufanya biashara na zinaendelea vizuri kama kawaida.

Sanjari na hayo ameeleza kuwa Jeshi hilo linaendelea na jitihada za kuwasaka vijana wote waliohusika katika tukio hilo na kuhakikisha kwamba wanakamatwa na wanachukukiwa hatua kwa mujibu wa sheria na kanuni za nchi.

Mutafungwa,ametoa onyo kwa machinga yoyote au mtu yoyote atakaye thubutu kufanya vurugu za aina yoyote kama walivyojaribu katika tukio hilo,Jeshi la Polisi wamejioanga kuhakikisha kwamba wanawakamata pasipo kujali idadi yao ili mradi tu wamefanya kosa.

Hata hivyo ameeleza kuwa Askari walioshiriki katika kuzuia vurugu hizo wapo salama huku machinga kama wanayo malalamiko kwamba wanafanyiwa vurugu na mgambo,anaye fanyiwa vurugu anatakiwa kufika kituo cha Polisi na kutoa taarifa na jeshi hilo lipo tayari kufanyia kazi na kuzichunguza taarifa zao.

“Hakuna mgambo ambaye anafanya kazi Jiji ambaye yupo juu ya sheria,wanatakiwa kufanya kazi kwa kufuata maadili na taratibu za kazi zao akienda kinyume na taratibu za kazi aliyopewa naye atashughulikiwa kwa mujibu wa sheria,machinga wasijisikie wanyonge kuacha kuja kituoni kutoa taarifa,” ameeleza Mutafungwa.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza Wilbroad Mutafungwa, akizungumza na waandishi wa habari mkoani Mwanza,hawapo pichani juu la tukio la kundi la watu wanaodaiwa kuwa ni machinga kufanya vurugu Jijini Mwanza.
Wafanyabiashara na wananchi wakiendelea na shughuli zao baada ya Jeshi la polisi kufanikiwa kutuliza vurugu zinazodaiwa kufanywa na kundi la vijana ambao ni machinga jijini Mwanza.
Baadhi ya maduka yakiwa bado yamefungwa kufuatia vurugu zilizofanywa na kundi la vijana wanaodaiwa kuwa ni machinga katika mitaa ya Jiji la Mwanza.