Na Esther Joel, TimesMajira Online
TANGU Rais Samia Suluhu Hassan, aingie madarakani mwaka 2021 hadi sasa ameonesha utashi mkubwa wa kisiasa katika kukuza sekta ya michezo kwa kufanya uwekezaji na mabadiliko kwenye sekta hiyo.
Miongoni mwa mambo ambayo yanadhihirisha dhahiri utashi wa Rais Samia katika kukuza michezo ni pamoja na maboresho makubwa yaliyofanyika katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, jijini Dar es Salaam.
Maboresho yamewezesha uwanja huo kuwa na huduma ya intaneti (Wi-Fi).
Aidha, maboresho mengine yamefanyika katika eneo la kuchezea, kukarabati miundombinu ya maji na umeme. Maboresho hayo yamegusa kila eneo la uwanja huo na yamefanya Uwanja wa Benjamin Mkapa kuwa miongoni mwa viwanja bora Afrika na umeitangaza Tanzania ulimwenguni pamoja na kutoa ajira kwa Watanzania.
Lakini pia, ukarabati umefanyika kwenye vyumba vya wachezaji vya kubadilishia nguo, chumba cha matibabu, chumba cha VAR na chumba cha kufuatilia kamera za ulinzi wa uwanjani.
Ukarabati huo umeridhisha viongozi mbalimbali wa Serikali waliokagua uwanja huo baada ya ukarabati.
Aidha,uamuzi wa Rais Samia kuufanyia maboresho uwanja huo ni uthibitisho tosha kwamba anataka kuhakikisha Tanzania inafikia hatua ambazo mataifa mengine yameshafikia kwenye sekta ya michezo.
Kimsingi ukarabati huo ni baadhi tu ya mambo ya kujivunia katika kipindi hiki cha utawala wa Rais Samia katika kukuza sekta ya michezo.
Kimsingi, Rais Samia anastahili kupongezwa kwa hilo, kwa uwanja huo ulikuwa unastahili kukarabatiwa.
Hiyo ni kwa sababu Tangu Uwanja wa Benjamin Mkapa ukamilike mwaka 2007, haukuwahi kufanyiwa ukarabati mkubwa kama ambavyo imefanyika sasa.
Mfano, viti vilitakiwa kubadilishwa baada ya miaka 10, lakini jambo hilo halikuwa limefanyika. Eneo la kukimbilia riadha nalo, lilitakiwa kufanyiwa ukarabati tangu mwaka 2012, lakini hilo halijafanyika.
Vitu kama mfumo wa vyoo vinavyotumika uwanjani, taa zinazotumika zilikuwa zimepitwa na wakati kulingana na mahitaji ya sasa, vifaa vya zimamoto na uokoaji na miundo ya tehama vilikuwa ni hitaji muhimu kufanyiwa ukarabati ili uwanja huo ubaki na heshima yake kama uwanja bora katika eneo la Afrika Mashariki na Kati.
Uwanja wa Mkapa kwa sasa ndiyo unatambulika kama uwanja bora katika ukanda huu wa Afrika na ndiyo sababu sasa ni wa uwanja wa nyumbani wa mataifa mbalimbali.
Ili kubaki katika sifa yake hiyo, ukarabati uliofanywa na Rais Samia ulitakiwa kufanyika.
Uamuzi huo wa Serikali kuufanyia maboresho umefanya Uwanja huo wa Mkapa kukidhi masharti yaliyotolewa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF).
Lakini pia ukarabati wa Uwanja wa Benjamin Mkapa ni ukarabati unaolipa kiuchumi.
Wakati Liverpool ilipoamua kukarabati uwanja wake wa Anfield, iliamua kuongeza viti takribani 8,500, huku zaidi ya nusu vikiwa ni eneo la matajiri.
Kuongeza viti vya matajiri uwanjani kunaongeza mapato kwa uwanja kutokana na wanaoingia na mapato kwa wajasiriamali ambao huduma zao zitatumiwa na watu wenye ukwasi.
Kwa sasa, Uwanja wa Benjamin Mkapa unaingiza takribani shilingi bilioni tano kwa mwaka kupitia mechi za mashindano mbalimbali yanayofanyika uwanjani hapo.
Sehemu kubwa ya mapato huenda kwa vilabu kama Simba na Yanga lakini kiasi cha walau kati ya shilingi bilioni 1.8 hadi bilioni mbili hubaki kwenye uwanja.
Hivyo, ukarabati uliofanyika utaweza kuingiza mapato zaidi hasa ukizingatia kwamba michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) yataandaliwa na Tanzania kwa kushirikiana na Kenya na Uganda mwaka 2027.
Lakini pia Uwanja wa Benjamin Mkapa uliitangaza zaidi Tanzania kufuatia uamuzi wa CAF kuwa mwenyeji wa mechi ya ufunguzi wa mashindano ya Super League.
Mechi hiyo ilihuhudiwa na wapenzi wa soka barani Afrika na duniani kwa ujumla. Katika mchezo wa ufunguzi, wageni wengi walitapata taswira halisi ya Tanzania kupitia kile walichokiona uwanjani siku hiyo.
Uzuri na umaridadi wa uwanja huo waliouona siku hiyo, utabaki kuwa taswira ya kudumu kwao kuhusu nchi yetu. Kama wataamua kurejea tena Tanzania – kwa mazoezi au kwa mechi; kama ambavyo nchi nyingine jirani zimeomba kutumia uwanja wetu.
Lakini pia kwa Tanzania kukubaliwa kuwa mwenyeji wa mashindano ya AFCON kwa kushirikiana na nchi za Kenya na Uganda, maboresho yaliyofanywa na Rais Samia uliiweka Tanzania kukidhi vigezo vyote vinavyokubalika na CAF.
Kizuri zaidi wakati wa ukarabati wa uwanja huo maelekezo ya Rais Samia, aliyoyatoa yametekelezwa kwa vitendo.
Mfano, Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) chini ya usimamizi wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, limetekeleza maagizo ya Rais la kutaka Uwanja wa Benjamin Mkapa uwekewe huduma ya Mtandao wa Inteneti ikiwa ni sehemu ya ukarabati katika uwanja huo.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa huduma hiyo ya Mtandao katika uwanja huo Novemba 5,2023, Waziri wa Habari,Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye, alisema kutekelezwa kwa agizo hilo la Dkt. Samia linakwenda kuwasaidia mashabiki na wapenzi wa masuala ya michezo.
Kwa hiyo watakuwa na uwezo wa kutuma na kupokea taarifa za matukio mbalimbali kiwanjani hapo kwa kutumia intaneti yenye kasi zaidi.
“Leo tunaanza kuzindua huduma hii ya intaneti yenye kasi katika Uwanja huu wa Mkapa na kwa maagizo ya Rais Samia ya kwamba viwanja vyote vipate huduma ya mtandao ili wanaohudhuria viwanjani wafurahie Mtandao,” alisema Nape wakati wa uzinduzi huo.
Lakini pia uamuzi wa Rais Dkt. Samia wa kuridhia asilimia tano ya kodi itokanayo na michezo ya kubashiri (sports betting) ipelekwe katika Mfuko wa Maendeleo ya Michezo ili kusaidia shughuli za maendeleo ya michezo hapa nchini umelenga kuikuza zaidi sekta hiyo.
Aidha, hatua ya Rais Samia kuiundia sekta ya michezo wizara yake ni uthibitisho tosha kwamba anataka kuhakikisha kwamba Tanzania inafikia hatua ambazo mataifa mengine yameshafikia kwenye sekta ya michezo.
Hayo ni baadhi tu ya mambo ya kujivunia katika kipindi hiki cha utawala wa Rais Samia.
More Stories
Tathimini ya Mpango wa ya Pili wa Kunusuru Kaya Maskini Wazinduliwa Viziwani Zanzibar
Safari ya binti kutoka ‘uhausigeli’hadi darasani
Samia anavyovunja rekodi kwa kupeleka fedha nyingi miradi ya maji vijijini