March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mabalozi RSA wahimizwa kuelimisha jamii kuhusu umuhimu wa usalama barabarani

Na Lubango Mleka,Timesmajira Online – Dodoma. 

MABALOZI wa Usalama Barabarani (RSA) wamehimizwa kuendelea kujitoa kuielimisha jamii na madereva juu ya kufuata sheria za usalama barabarani ili kuepusha ajali zisizo za lazima. 

Hayo yamezungumzwa na wadau wa usalama barabarani katika mkutano wa mwaka wa Mabalozi wa Usalama Barabarani ulifanyika ukumbi wa Polisi Jamii jijini Dodoma. 

Ambapo Chuo cha Ufundi Stadi na Mafunzo ya Ufundi (VETA) kimetajwa kuwa mdau muhimu katika kuimarisha usalama barabarani nchini, kupitia mchango wake wa kutoa mafunzo kwa madereva katika vyuo vyake mbalimbali.

Kaimu Mkurugenzi wa Mafunzo wa VETA, Bwire Ally, amesema chuo hicho kimekuwa mstari wa mbele kuhakikisha madereva wanapata umahiri na uelewa wa kutosha kuhusu sheria na kanuni za barabarani.

 “Tuna jumla ya vyuo 80, na hadi kufikia mwisho wa mwaka huu tunatarajia kufikisha vyuo 125. Asilimia kubwa ya vyuo hivi vinatoa mafunzo kwa madereva, hivyo usalama barabarani unategemea sana umahiri wao. Kwa msingi huo, VETA ni mdau wa usalama barabarani,”amesema Bwire.

Kwa upande wake mwakilishi wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, ASF.Castory Willa, amesema jeshi hilo litaendelea kushirikiana kwa karibu na mabalozi wa usalama barabarani ili kulinda maisha na mali za wananchi.

Naye Mkurugenzi wa Udhibiti Usafiri wa Barabara kutoka LATRA, DCP.Johansen Kahatano, amesema mafanikio ya kampeni za usalama barabarani yanatokana na ushirikiano wa wadau mbalimbali wakiwemo mabalozi wa usalama.

 “Kuanzia mwaka jana tumeshuhudia mabadiliko chanya. Tulifanya majaribio ya safari za saa 24, na RSA walikuwa vinara wa utekelezaji huo kwa kushirikiana na serikali, LATRA na Jeshi la Polisi. Mafanikio hayo ni ushahidi wa umuhimu wa ushirikiano,” amesema.

Awali akisoma risala ya taasisi hiyo, Mtendaji Mkuu wa Road Safety Ambassadors (RSA), Augustus Fungo, alieleza mafanikio yaliyopatikana, ikiwemo ongezeko la wanachama kutoka 38 hadi zaidi ya 300 pamoja na usajili rasmi wa taasisi hiyo.

Mwenyekiti wa RSA Taifa, Mohamed Mpinga, aliwataka mabalozi wa usalama barabarani kuendelea kujitoa kwa moyo mmoja ili kufanikisha lengo la kupunguza ajali na kuokoa maisha ya Watanzania.

Kwa niaba ya Mkuu wa Jeshi la Polisi, IGP Camillius Wambura, Afisa Mnadhimu wa Kamisheni ya Operesheni na Mafunzo, SACP Abdi Issango, amesema usalama barabarani ni suala la lazima kwa kuwa maisha ya mwanadamu hayawezi kutenganishwa na usafiri.

 “Lengo kuu la usafiri ni kufika salama. Mabalozi mna jukumu kubwa la kupaza sauti, kutoa elimu kwa madereva na watumiaji wengine wa barabara ili kuhakikisha sheria na taratibu zinafuatwa kikamilifu,” amesema Issango.