Na Esther Macha,Timesmajira Online,Mbeya
RAIS wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC)na Askofu Mkuu wa Jimbo Katoliki la Mbeya Mhashamu Askofu Gervas Nyaisonga amesema wamesikitishwa na maafa ya maporomoko ya udongo yaliyotokea mlima Hanang Mkoa wa Manyara.
Ambayo yameathiri Mji Mdogo wa Katesh na kusababisha vifo vya watu 65 na kaya zaidi ya 1,150 pamoja na watu 5,600 kuathirika na mafuriko huku walionusurika wakiwa wamehifadhiwa kwenye majengo ya kanisa,shule na kwa watu wengine wenye mapenzi mema.
Mhashamu Askofu Nyaisonga ametoa kauli hiyo Jumatano ,Desemba 6,2023 kwa niaba ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) wakati akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi za Jimbo Kuu la Mbeya kuhusiana na maafa hayo yalioikumba taifa.
“Hili ni tukio baya ambalo linasikitisha tunatoa pole kwa wananchi wote wa Hanang na Mkoa mzima wa Manyara ,watanzania wote pia kwa Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan na tunakiri maafa haya yana mguso wa kimazingira yasiyo epukika kwa udharura wa papo kwa papo,“amesema ameongeza kuwa
“Tunakiri kuwa maafa haya yamesababisha vifo vingi na upotevu wa mali pamoja na uharibifu wa miundombinu na kupelekea usumbufu mkubwa wa watu , kikubwa tuishukuru serikali kwa hatua za dharura walizochukua ,wanajeshi, askari wetu, na watu wote waliojituma kushughulikia uokoaji wa haraka kwa watu walioathirika,”.
Aidha Askofu Nyaisonga amewatia moyo walioathiriwa na maafa hayo na kuwashukuru wale wote waliotoa msaada huku akiwataka watanzania wote kutokata tamaa kwa kuwa wakarimu kwa wananchi waliokutwa na maafa hayo waendelee kumuamini Mungu kuwa anawapenda na kuwapa ujasiri pamoja na kuendelea kuwaombea majeruhi wote.
Akizungumzia kuhusu msaada kwa waathirika Askofu Nyaisonga amesema kuwa tayari wameanza kuratibu utaratibu wa kupeleka msaada kupitia kitengo cha Caritas kinachoshughulikia maafa ikiwepo dawa , vyakula , mavazi na mbegu za shambani tayari waraka umesaniwa kwa ajili ya kukabidhi vitu hivyo.
Pia ameeleza kuwa wanaendelea kuwasiliana na wahisani wao ndani na nje ya nchi pamoja na washirika ili kuendelea kutoa misaada.
More Stories
AZAKI yawasilisha mapendekezo yao kwa Serikali katika kuboresha Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050
CP.Wakilyamba :Uvamizi maeneo ya hifadhi ya taifa katavi haukubaliki
Watu wawili wanaodhaniwa majambazi wapigwa risasi na Polisi