Na Rotary Haule,TimeMajira Online
SIKU chache baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kumteua aliyekuwa Spika wa Bunge, Anne Makinda kuwa Kamishna wa Sensa Tanzania Bara na Rais wa Zanzibar, Dkt. Hussein Mwinyi kumteua Balozi Mohamed Hamza tayari wawili hao wamekutana kwa mara ya kwanza Mjini Kibaha kwa ajili ya kufanya ziara ya kukagua maandalizi ya vituo vilivyopangwa kwa ajili ya kufanyia Sensa ya mwaka 2022.
Ziara ya makamishna hao ilifanyika juzi kwa kumshirikisha Mkuu wa Wilaya ya Kibaha, Sarah Msafiri na wataalamu wa masuala ya Sensa ambapo walitembelea kituo cha Muheza kilichopo Kibaha Mjini, eneo ambalo litatumika katika sensa ya majaribio itakayofanyika Agosti, mwaka huu.
Katika ziara hiyo, Makinda amesema kuwa, lengo kubwa ya ziara yao ni kuangalia na kukagua maandalizi yaliyofanyika juu ya kutenga maeneo ambayo yatatumika katika kuhesabia watu katika Sensa ya mwaka 2022.
Makinda amesema kuwa, Sensa ya mwaka 2022 itakuwa ya kisasa na bora zaidi kwa kuwa imepangwa kufanyika mpaka ngazi ya kitongoji tofauti na ile ya 2010 iliyofanyika kwa kuishia ngazi ya wilaya.
Amesema kuwa,wameweka utaratibu mzuri wa kuhakikisha kila mtu anahesabiwa kwa wakati na kwamba kila kituo kitatumia kuhesabu kaya 50.
“Sensa ya mwaka 2022 itafanyika kwa kiwango cha juu kwa kuwa tumejipanga vizuri kuendesha zoezi hilo na tumeandaa vifaa vya kutosha vikiwemo Vishikwambi vitakavyotumika (Tablets) kwa hiyo wananchi wawe tayari kutoa ushirikiano mara baada ya zoezi hilo kuanza,”amesema Makinda.
Nae Kamishna wa Sensa kutoka Zanzibar, Balozi Mohamed Hamza amesema kuwa, kwa sasa wapo katika maandalizi ya awali ya kugawa maeneo ya Sensa na Kibaha ni miongoni mwa maeneo yatakayofanyikia Sensa ya majaribio.
Balozi Hamza,alitumia nafasi hiyo kueleza umuhimu wa Sensa na kusema kuwa Sensa inasaidia kupata idadi sahihi ya watu na hivyo kuifanya Serikali kutoa huduma za kijamii kulingana na idadi ya watu wake.
Amesema kuwa, Serikali inapokosa idadi sahihi ya watu inasababisha kushindwa kutoa huduma za kijamii kwa watu wake jambo ambalo linaweza kuwanyima haki wananchi.
“Umuhimu wa Sensa ni mkubwa kwa nchi zetu kwani tunapopata idadi sahihi ya watu ndipo inaposaidia Serikali kutoa huduma sahihi kulingana na watu wake kwahiyo tunaomba kila mwananchi hawe na utayari wa jambo hili,”amesema Balozi Hamza
Balozi huyo,aliwataka wataalamu waliopewa jukumu la kufanyakazi hiyo wahakikishe wanatumia lugha ya upole na unyenyekevu ili kila mwananchi ajisikie furaha kuhesabiwa kuliko kutoa matusi na dharau zitakazosababisha watu kuacha kuhesabiwa.
Kwa upande wake mrasimu ramani kutoka ofisi ya takwimu inayoshughulikia masuala ya Sensa Mkoa wa Pwani, Tumaini Komba kazi ya kugawa maeneo hayo ilianza Juni 18, mwaka huu.
Komba alisema, kazi hiyo ilianza katika Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha na baadae kumalizia Halmashauri ya Kibaha Mjini ambapo mpaka sasa maandalizi hayo yamefanyika vizuri .
Alisema kuwa,kwa Mtaa wa Muheza pekee wamefanikiwa kutenga maeneo madogo madogo 17 ambapo kila eneo litakuwa na kaya 50 za watu watakaohesabiwa.
Mkuu wa Wilaya ya Kibaha, Sarah Msafiri,alisema kuwa amefurahishwa na hatua ya kupewa kipaumbele kwa eneo lake kuwa sehemu ya kufanyika kwa Sensa ya majaribio Agosti, mwaka huu.
Hata hivyo, Msafiri aliwaomba wataalamu hao kuendelea kushirikiana kwa kila jambo hili kuhakikisha wanatatua kwa pamoja changamoto zinazojitokeza na kufanya zoezi la sensa litakapoanza liwe la mafanikio zaidi.
More Stories
Kongamano la Uwekezaji kati ya Tanzania na Ubelgiji lafanyika Dar
CCM kuhitimisha kampeni kwa kishindo
Walimu elimu ya lazima watatakiwa kuwa wabobezi kwenye masomo wanayofundisha