Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online
Kuelekea kwenye kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Nyuki Duniani, Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Singida imeanza maandalizi ya Maadhimisho hayo yatakayofanyika kitaifa mkoani humo Mei 20,2023
Akizungumza jana mara baada ya kufanyika kwa kikao cha kamati cha maandalizi ya maadhimisho hayo, Kaimu Mkurugenzi Msaidizi wa Maendeleo ya Ufugaji Nyuki kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii,Daniel Pancras amesema Maadhi misho hayo kwa mwaka huu yatakuwa ya namna yake ambapo yatatanguliwa na maonesho.
Amesema Maadhimisho hayo yatatanguliwa na Maonesho mbalimbali ya mazao ya nyuki yatakayoanza Mei 17,2023 hadi Mei 20,2023 ambapo wananchi watapatiwa mafunzo ya ufugaji pamoja na faida za mazao ya mdudu nyuki,
Ameongeza kuwa katika kipindi hicho cha maadhimisho mada mbalimbali zitatolewa ikiwemo namna ya kuangalia ubora wa mazao ya nyuki ikiwemo asali na nta
“Wapo wadau mbalimbali ambao wamethibitisha ushiriki wao na upande wetu Sisi tunaendelea kuratibu zoezi hili likiwa ni jukwaa muhimu kwa wafugaji nyuki hapa nchini ” amesema Pancras.
Kufuatia hatua hiyo Mkurugenzi huyo ametoa wito kwa Wadau wa ufugaji nyuki nchini kujitokeza kwa wingi kushiriki katika Maadhimisho hayo
Ameongeza kuwa ” Tunawakaribisha wananchi wote waje kujifunza ili waweze kuchangamkia fursa ya ufugaji nyuki “
Kwa upande wake, Katibu Tawala Msaidizi Uchumi wa Mkoa wa Singida, Stanslaus Choaji amesema maandalizi ya maadhimisho yanazidi kupamba moto hivyo amewataka wakazi wa Singida wajipange kutumia fursa hiyo kiuchumi ili mkoa huo uwe kinara kwa ufugaji nyuki nchini.
Naye Mratibu wa Maadhimisho hayo kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii, Philip Mwampamba amewataka wafanyabiashara mbalimbali kujitokeza kutumia fursa hiyo kujitanua kibiashara
More Stories
Mbowe akuna wengi kuhusu maridhiano
Waziri Chana amuapisha Kamishna uhifadhi NCAA, ampa maagizo mazito
Amos Lengael Nnko afariki kwa ajali ya gari