Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online
Waziri wa Madini, Dkt. Doto Biteko amewataka Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa kuondoa urasimu kwa wawekezaji wanaoonesha nia ya kuwekeza kwenye uchimbaji na biashara ya madini nchini.
Waziri Biteko ametoa agizo hilo leo mjini Morogoro kwenye kikao chake na Viongozi wa Tume ya Madini ikiwa ni pamoja na Wakurugenzi, Mameneja na Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa.
Kikao hicho pia kilihudhuriwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Profesa Simon Msanjila, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Martine Shigella na Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Albert Msando.
Viongozi wengine waliohudhuria kikao hicho ni pamoja na Kaimu Kamishna wa Madini kutoka Wizara ya Madini, Fransis Mihayo, Kamishna wa Tume ya Madini, Janeth Reuben Lekashingo, Kaimu Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Mhandisi Yahya Samamba pamoja na wakurugenzi kutoka Wizara ya Madini.
Waziri Biteko amesema kuwa wawekezaji wengi kutoka nje ya nchi hasa nchi za jirani wameonesha nia ya kuwekeza kwenye shughuli za madini hususan biashara ya madini hivyo ni vyema maafisa madini wakazi wa mikoa wakahakikisha wanawasaidia kwenye taratibu za kufanya biashara ya madini badala ya kuwawekea vikwazo.
” Kuna ofisi za Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa zilizopo mipakani hasa katika mikoa ya Mara, Ruvuma, Kagera ni vyema zikahakikisha zinawasaidia wadau wa madini kutoka nchi za jirani wanaohitaji huduma, ambao ninaamini watakuwa mabalozi kwa wengine,” amesisitiza Biteko.
Ameendelea kusema kuwa Wizara ya Madini sambamba na kupangiwa lengo la kukusanya kiasi cha shilingi bilioni 650 kwa mwaka wa fedha 2021-2022 na kuhakikisha Sekta ya Madini inakuwa na mchango kwenye Pato la Taifa kwa asilimia 10 ifikapo mwaka 2025, mikakati mbalimbali imewekwa ikiwa ni pamoja na kuvutia wawekezaji wengi kuja kuwekeza nchini.
Aidha, amewataka Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa kusimamia kwa karibu zaidi maafisa walio chini yao kwa kuhakikisha wanafanya kazi kwa weledi na uaminifu mkubwa na kuongeza kuwa Wizara haitamvumilia mtumishi yeyote atakayebainika anakiuka maadili ya utumishi wa umma.
Ili kuvuka lengo la ukusanyaji wa maduhuli kwa mwaka wa fedha 2021-2022 la shilingi bilioni 650, Dkt. Biteko ameitaka Tume ya Madini kuwekeza nguvu kwenye usimamizi wa madini ya ujenzi na madini ya viwandani.
“Mnatakiwa kuhakikisha mnaweka usimamizi wa karibu kwenye shughuli za uchimbaji wa madini ujenzi ikiwa ni pamoja na matumizi wa mfumo wa malipo kwa njia la kielektroniki ambao ninaamini utafanikisha kuendelea kuvuka lengo la ukusanyaji wa maduhuli kwa mwaka huu wa fedha unaoisha mwezi Juni,” amesema Dkt. Biteko.
Aidha amewataka maafisa madini wakazi wa mikoa kuhakikisha wanawahamasisha wachimbaji wadogo wa madini kuunda vikundi na kuwapa leseni ili kuondoa migogoro ya mara kwa mara inayojitokeza.
Wakati huohuo Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Martine Shigella amempongeza Waziri Biteko kwa kasi kubwa kwenye usimamizi wa Sekta ya Madini kupitia Wizara ya Madini na Taasisi zake na kusisitiza kuwa tangu amekabidhiwa Wizara hiyo yamekuwepo mabadiliko makubwa.
” Kwa usimamizi wako mahiri wa Sekta ya Madini, wananchi wameshuhudia mabadiliko makubwa ikiwa ni pamoja na mchango wa Sekta ya Madini kwenye Pato la Taifa kukua hadi kufikia asilimia 7.9, uanzishwaji wa Ofisi za Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa na masoko ya madini, ujenzi wa ukuta wa Mirerani na ongezeko kubwa la makusanyo ya maduhuli, amesema Shigella.
Ameongeza kuwa ofisi yake itaendelea kushirikiana kwa karibu na Wizara ya Madini kwenye usimamizi wa Sekta ya Madini hususan kwenye utatuzi wa mogogoro ya ardhi kwenye shughuli za uchimbaji wa madini.
Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Profesa Simon Msanjila amewataka maafisa madini wakazi wa mikoa kuimarisha ushirikiano na mawasiliano kwenye utendaji kazi.
Aidha, amewataka kujiendeleza kimasomo katika ngazi ya shahada ya uzamili na kusisitiza kuwa Wizara ya Madini imetenga fedha za kutosha kwa ajili ya programu mbalimbali za mafunzo.
Kikao hicho cha siku mbili kilichofanyika mjini Morogoro ni maelekezo ya Waziri Biteko kwa lengo la kuweka mikakati ya kuimarisha utendaji kazi wa Tume ya Madini.
More Stories
Waziri Jerry afanya uteuzi wa Makamu Mwenyekiti, Wajumbe watano wa bodi ya Shirika la Posta
Kapinga atoa maagizo TANESCO ,kuhusu Vijiji vinavyolipia gharama ya mijini kuunganisha umeme
Ukiukaji wa Uhuru wa Kidini na Kutovumiliana Huzusha Malumbano ya Kimataifa