November 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Maadhimisho siku ya nyuki Duniani ni fursa adhimu kiuchumi

Na Mwandishi wetu, Timesmajira

Maadhimisho ya Siku ya Nyuki Duniani ambayo kitaifa yanaadhimishwa Jijini Dodoma, ni fursa kubwa ya kiuchumi kwa wafugaji nyuki, wajasiriamali na wafanyabiashara wa mazao ya nyuki na wadau wengine wa sekta ya ufugaji Nyuki kukutana kwa lengo la kujengeana uwezo wa namna bora ya kuendeleza Sekta ya Nyuki.

Hayo yameelezwa na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Rosemary Senyamule kwenye ufunguzi rasmi wa Maadhimisho hayo yenye kaulimbiu ‘‘Nyuki kwa Afya na Maendeleo. #APIMONDIA 2027 Tanzania ipo Tayari’’ iliyobeba ujumbe wa mchango wa mdudu nyuki katika afya njema kutokana na matumizi ya mazao ya mdudu Nyuki, pamoja na kujipatia kipato kupitia mazao hayo.

Senyamule ametoa rai kwa wananchi wote wa mkoa wa Dodoma na mikoa mingine nchini kufuga nyuki kwa kutumia mbinu rafiki kwa mazingira ili kuimarisha afya na kujiongezea kipato.

“Siku ya leo kama ishara ya ufunguzi wa maadhimisho haya nimeweka mizinga ya nyuki wasiodunga (maarufu kama nyuki wadogo) katika eneo letu la bustani ya miti Medeli, hivyo nitoe wito kwa wanachi wote Mkoa wa Dodoma kufuga Nyuki hawa ili kujipatia kipato” Ameongeza Senyamule.

Aidha, Senyamule ametoa wito kwa wananchi wa Mkoa wa Dodoma kujitokeza kwa wingi kwenye maadhimisho hayo yatakayofikia kilele tarehe 20 Mei, 2024 huku mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt Philip Isidor Mpango.

Akimkaribisha Mgeni rasmi Mkurugenzi wa Misitu na Nyuki, Deusdedith Bwoyo amesema kuwa Dunia nzima huadhimisha Siku ya Nyuki ambayo ni matokeo ya makubaliano ya Baraza la Umoja wa Mataifa mnamo Mwaka 2017, lengo kuu likiwa ni kutambua mchango wa Sekta ya Nyuki katika maisha ya mwananchi mmoja mmoja, Taifa na Dunia kwa ujumla.