Na Zena Mohamed,Timesmajiraonline,Dodoma
WIZARA ya Elimu,Sayansi na Teknolojia inatarajia kufanya maadhimisho ya Kitaifa ya Siku ya Kimataifa ya Wanawake na Wasichana katika Sayansi ambayo huadhimishwa Februari 11 kila mwaka yatakayofanyika ukumbi wa Jakaya kikwete jijini Dodoma,huku Waziri wa Wizara hiyo,Profesa.Adolf Mkenda akitarajiwa kuwa mgeni rasmi.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini hapa leo,Februari 7,2025 Naibu Waziri wa Wizara hiyo Omari Kipanga amesema kuwa Takwimu za elimu na ajira duniani zinaonesha kuwa ushiriki wa wanawake na wasichana katika elimu na ajira katika fani za sayansi ni mdogo ikilinganishwa na ushiriki wa wanaume.
Ambapo amefafanua kwa Tanzania ushiriki wa wanawake ni asilimia 36 na wanaume ni asilimia 64 , hali inayopunguza juhudi za kufikia usawa wa kijinsia katika elimu na ajira.
Hivyo ametaja lengo la kuadhimisha siku hiyo ni kutambua na kusherehekea mchango wa wanawake na wasichana katika nyanja za sayansi, teknolojia, uhandisi na hisabati (STEM).
“Maadhimisho haya ni fursa ya kuhamasisha wanawake na wasichana zaidi kujiunga katika nyanja hizi ili kubadili mustakabali wao na jamii zetu kwa ujumla.
“Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mwaka 2015, lilipitisha programu ya Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Wanawake na Wasichana katika Sayansi kwa kutangaza tarehe 11 Februari kuwa Siku ya Kimataifa ya Wanawake na Wasichana katika sayansi.,”amesema
Aidha amesema Tanzania inatambua kuwa usawa wa kijinsia ni muhimu sana kwa kufikia malengo ya maendeleo yaliyokubaliwa kimataifa, ikiwa ni pamoja na Ajenda ya 2030 ya Maendeleo Endelevu.
Kipanga alifafanua kuwa kutokana na maazimio hayo ya Umoja wa mataifa, Tanzania imekuwa ikiadhimisha siku ya Kimataifa ya Wanawake na Wasichana katika Sayansi kuanzia mwaka 2021.
“Masuala ya wanawake na wasichana ni mtambuka na hivyo yanahitaji ushiriki na mchango wa wadau wote bila kujali wako katika sekta ya umma au binafsi.
“Tunahitaji kuhamasisha kizazi kilichopo na kijacho cha wasichana kupenda na kujiunga na masomo ya sayansi kwa kuondoa dhana potofu na kutoa fursa sawa katika elimu na maendeleo ya kitaaluma,”amesema
More Stories
Watanzania wakumbushwa kudumisha na kulinda amani
Mbaruku:Lushoto haikutakiwa kuwa na shida ya maji
Mawaziri wa EAC,SADC wakutana Dar kujadili usalama wa Congo