January 5, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Maabara mpya wakala mbegu za kilimo yazinduliwa

Na Mwandishi Wetu,TimesMajira,Online

KATIBU Mkuu Kilimo, Gerald Kusaya, amezindua maabara ya kisasa iliyojengwa kupitia Mradi wa Kuongeza Tija na Uzalishaji kwenye zao la Mpunga (ERPP) kwa ajili ya kuboresha utendaji kazi wa Wakala wa Mbegu za Kilimo (ASA) mjini Morogoro.

Akizungumza kabla ya kuzindua maabara hiyo jana, Kusaya alisema jengo la maabara hiyo ni moja ya kazi nzuri iliyofanyika chini ya usimamizi wa Wizara ya Kilimo na hatimaye maabara hiyo iko tayari kuanza kutumika.

Amesema licha ya kuizindua maabara hiyo, kuna vifaa vingine ambavyo vinapaswa kununuliwa ili kuiwezesha maabara hiyo kufanya kazi kwa ufanisi na kwamba wizara itanunua vifaa hivyo mapema iwezekanavyo.

Kusaya amesema suala la kuongeza tija na uzalishaji katika kilimo ndiyo limesukumu sehemu kubwa ya mabadiliko ya kiutendaji katika maeneo mbalimbali ambapo; Ili taifa liongeze uzalishaji wa mazao ya biashara na chakula yanaenda sambamba na matumizi ya mbegu bora pamoja na pembejeo nyengine.

Mahindi

“Suala la kuongeza uzalishaji wa mbegu bora ni suala la msingi hasa kipindi hiki ambacho mahitaji na matumizi ya mbegu bora za kilimo, yameongezeka kwa kiasi kikubwa. Hata hivyo, bado kasi ya uzalishaji wa mbegu ni ndogo,”amesema.

Aidha, ametoa rai kwa watumishi wa Wakala wa Taifa wa Mbegu za Kilimo kuendelea kutoa huduma ya kuzalisha mbegu bora za mazao ya kilimo licha ya kukabiliana na changamoto kadhaa.

“Nafahamu changamoto nyingi zilizopo na mnazopitia kama Wakala wa Serikali lakini bado mnahitaji kuongeza juhudi, kasi na ufuatiliaji ulio makini katika suala zima la uzalishaji wa mbegu bora ili ziwafikie na kubadilisha maisha ya wakulima wetu.

Dhamana hii mliyopewa ni kubwa na usimamizi wake lazima uendane na kufanya kazi kwa kujituma na kwa uadilifu wa hali ya juu. Kufanya kazi ASA ni sawa na kufanya kazi benki kwani fedha zipo na unazishika kila siku lakini sio zako.” Amesema.

Wakati huohuo, Katibu Mkuu Kusaya ametumia fursa hiyo kuwakumbusha Watumishi wa Wakala wa Mbegu Bora (ASA) kufanya kazi kwa juhudi, maarifa na uhadilifu mkubwa.

“Ndugu zangu, napenda niwahimize kila Mtumishi afanye kazi kwa uhamimifu mkubwa; Binafsi uwa nachukia sana wizi wa mali za umma, matumizi mabaya ya rasilimali za umma. Niwaomba tufanye kazi na atakayekataa kufanyakazi kwa uadilifu; Tutamchulia hatua,”amesema.