January 23, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Ma-DC wapya Tabora watakiwa kutatua kero za wananchi

Na Allan Vicent, TimesMajira Online,Tabora

WAKUU wa Wilaya walioteuliwa hivi karibuni na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan wakiwemo waliohamishwa vituo vya kazi na kuletwa Mkoani Tabora wametakiwa kutekeleza wajibu wao kwa weledi mkubwa ikiwemo kusikiliza na kutatua kero za wananchi.

Wito huo umetolewa jana na Mkuu wa Mkoa huo Balozi Dkt Batilda Burian alipokuwa akiwaapisha kabla ya kuanza majukumu yao katika wilaya walizopangiwa.

Alisema dhamana waliyopewa na Mheshimiwa Rais ni kutumikia wananchi, hivyo kila mmoja anapaswa kuhakikisha anasikiliza na kutatua kero za wananchi na kusimamia kwa dhati fedha zote za miradi ya maendeleo zinazoletwa na serikali.

Aidha aliwataka kusimamia sheria ya matumizi bora ya ardhi na kuainisha maeneo ya uwekezaji kwa ajili ujenzi wa viwanda vya uzalishaji bidhaa mbalimbali ili kwenda na kauli mbiu ya Mkoa huo ya ‘Ifanye Tabora kuwa Mkoa wa Viwanda’.

Balozi Batilda alibainisha kuwa amani ndiyo msingi wa maendeleo katika jamii yoyote ile, hivyo akawataka kwenda kuimaraisha ulinzi na usalama katika wilaya zao na kushirikiana na wananchi ili kufanikisha mipango yao.

Aidha aliwataka kuongeza mapato, kulinda vyanzo na maji, kukemea vitendo vya ukataji miti ovyo, uchomaji mkaa, kudhibiti uvamizi wa maeneo ya hifadhi na kuhamasisha ufugaji wa kisasa ili kuongeza thamani ya mifugo yao.

‘Hadi kufikia Januari 31, 2023 ni asilimia 67.3 tu ya watoto wote waliofaulu darasa la 7 waliokwisha ripoti shuleni, nendeni mkalisimamie hili, nataka watoto wote    waliochaguliwa kujiunga kidato cha kwanza waripoti shuleni, alisema.

 Alisisitiza kuwa ameelekeza Watendaji wa Vijiji na Kata kupita katika shule zote ili kubaini nani karipoti na nani hajaripoti, aliagiza Ma DC kufuatilia zoezi hilo na kuchukua hatua stahiki, aidha alibainisha kuwa hata kama mtoto hana viatu wala sare za shule apokelewe hivo hivo.

Kwa upande wake Mstahiki Meya wa halmashauri ya manispaa ya Tabora Ramadhan Kapela alisema wana imani na Wakuu hao wa wilaya walioletwa katika Mkoa huo hivyo akawataka kuchapa kazi kwa bidii kama Rais Samia anavyofanya.

Alisisitiza kuwa Mkuu wa Mkoa huo ni jembe la kazi, kipenzi cha wananchi, mchapakazi hodari na mwenye roho ya imani hivyo wanapaswa kujifunza kutoka kwake ili kufanisha utekelezaji majukumu yao.

Akiongea kwa niaba ya Ma DC wenzake, Zakaria Mwansansu (Mkuu wa wilaya ya Uyui) alisema wamejipanga vizuri na wako tayari kusimamia maendeleo ya wananchi katika wilaya walizopangiwa, hawatamwangusha Mheshimiwa Rais.

Ma DC wengine walioteuliwa au kuhamishiwa katika Mkoa huo ni Laitapwaki Tukai (Nzega), Simon Chacha (Sikonge), Dkt. Mohamed ChuaChua (Kaliua), Said Mtanda ( Urambo), Luis Bura (Tabora) na Sauda Mtondoo (Igunga).

Mkuu wa Mkoa wa Tabora Balozi Dkt Batilda Salha Burian (aliyeketi katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Wakuu wa Wilaya 7 za Mkoa huo, wa pili kushoto ni Katibu Tawala wa Mkoa huo Dkt John Mboya. Picha na Allan Vicent.