January 22, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Lushoto wamshukuru Rais Samia kwa miradi ya maji

Na Yusuph Mussa, Lushoto

Wananchi wa Kijiji cha Tewe, Kata ya Lunguza, Wilaya ya Lushoto mkoani Tanga wamemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwawekea mradi wa maji ya bomba, kwani tangu nchi ipate Uhuru mwaka 1961, wananchi hao hawajawahi kuona maji ya bomba kwenye kijiji chao.

Moja ya changamoto walizokutana nazo, ni wao kuchangia kunywa maji na wanyama ikiwemo mbwa kwenye mifereji ya maji . Lakini pia mama akifua nguo zenye uchafu wa mtoto juu ya mfereji huo, kwa chini wananchi wanachota maji hayo kwa ajili ya kunywa.

Hayo yalisemwa Oktoba Mosi, 2024 na Diwani wa Kata ya Lunguza Yassin Billa kwa niaba ya wananchi mbele ya viongozi wa Wakala wa Majisafi na Usafi wa Mazingira (RUWASA) Wilaya ya Lushoto na Mkoa wa Tanga, na wawakilishi wa Benki ya Dunia nchini Tanzania, na kutoka Makao Makuu ya Benki hiyo Washington DC nchini Marekani.

Ni kwenye Uzinduzi wa Mradi wa Maji Tewe uliojengwa kwa gharama ya sh. milioni 454.8, huku ukiwahudumia wananchi 2,235 wa Kijiji cha Tewe kwa kuwekewa vituo vya kuchota maji (Vilula) 10, huku tenki la kuhifadhi maji likiwa na ujazo wa lita 90,000.

“Watu kutoka World Bank, niwashukuruni sana kwa niaba ya wananchi wa Tewe. Watu hawa walikuwa wanatumia maji pamoja na wanyama sehemu moja. Wanyama kama mbwa wanapokunywa maji, mtiririko huo huo wa maji (mfereji) ndiyo walikuwa wanatumia watu hawa. Lakini wanapokuwa wanajisaidia katika mazingira kama hayo, mtiririko huo huo ndiyo walikuwa wanatumia maji hayo. Lakini anaefua eneo la juu, kama anafua nepi za mtoto, nguo zake mwenyewe baada ya kutoka shamba, anaechota eneo la chini, anachota maji hayo hayo mtu mwingine alikuwa akifulia.

“Kitendo mlichokifanya leo hii ambacho kwa kipekee kabisa, nimshukuru Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambaye amekubali mtuletee huduma hii ya maji sahihi kutoka kwenye chanzo maalumu, ambayo maji hayo yatatumiwa na binadamu, yatatenganisha baina ya wanadamu na wanyama, kiukweli mmewakomboa sana wananchi wa Kijiji cha Tewe. Tumepata miundombinu ya kisasa, tumepata miundombinu ambayo haikuwahi kufikirika kutokea katika eneo hili.

Billa amemshukuru Meneja wa RUWASA Mkoa wa Tanga Mhandisi Upendo Lugongo, na Meneja wa RUWASA Wilaya ya Lushoto Mhandisi Erwin Sizinga kwa kazi kubwa waliyofanya kwenye Wilaya ya Lushoto, lakini ametaka vijiji vyake vingine viwili, Lunguza na Kivingo vipatiwe maji ya uhakika.

“Mimi kama mwakilishi wa wananchi wa kata nzima ya Lunguza, kijiji chetu cha Lunguza na Kijiji cha Kivingo bado havina huduma nzuri ya maji. Ni wananchi ambao tangu mwaka 1990 wanatumia tenki la lita 90,000 kama tenki lililopo hapa (Tewe). Nawaombeni sana, na bahati nzuri Injinia Upendo niliwahi kukuomba ukiwa na Aweso (Jumaa Aweso, Waziri wa Maji), na ukanikubalia hili, nakuomba pale Lunguza hawana chanzo ambacho ni imara, na wanahitaji tenki jingine jipya.

“Na wana Kivingo vivyo hivyo, hawana chanzo cha maji cha uhakika, na wanahitaji waboreshewe huduma hiyo ili waweze kuona maji safi na salama kama yalivyo haya ya hapa Tewe. Tulifikiria hata kumueleza Injinia Erwin, Meneja wa RUWASA Wilaya ya Lushoto kuwa kama ataweza kufanya Upembuzi Yakinifu, tenki hili hili la Tewe, kwani kwa mteremko mkali uliopo, anaweza kuwagawia maji ndugu zetu wa Lunguza, kwani tuna Kituo cha Afya Lunguza, mkiboresha huduma ya maji mtaondoa usumbufu kwa wananchi” alisema Billa.

Billa alisema pamoja na kuwekewa miundombinu ya maji, bado huduma ya afya kwenye Kijiji cha Tewe ni duni, kwani kwenye zahanati yao hasa upande wa kujifungulia hakuridhishi, hivyo kuwaomba Benki ya Dunia, kwa vile wanashughulikia miradi ya maji, elimu na afya, basi warudi tena Tewe kwa ajili ya kuwapelekea huduma za afya.

Meneja wa RUWASA Wilaya ya Lushoto Mhandisi Sizinga, alisema mradi huo wa maji ya mserereko, umetekelezwa kwa mwaka mmoja, na umegharimu sh. 454,893,687, huku ukiwa na tenki la ujazo wa lita 90,000, vilula (DP’s) 10, na utahudumia wananchi 2,235.

“Ujenzi wa miundombinu ya maji katika mradi wa maji wa Tewe, Kata ya Lunguza ni miongoni mwa miradi ya maji inayoendelea kutekelezwa na Ofisi ya Meneja wa RUWASA, Lushoto kupitia fedha za Mfuko wa Taifa wa Maji (National Water Fund) pamoja na fedha za PforR.

“Mradi huu unatekelezwa na Mkandarasi M/S Buzubona wa Karagwe-Kagera kwa Mkataba Namba AE-102/2022-2023/TAG/W/14. Utekelezaji wa Mradi wa Maji Tewe. Mkataba huu ulisainiwa 23.02.2023 na kutokana na changamoto ya uchelewaji wa msamaha wa kodi, mradi ulianza rasmi 12.07.2023 na mradi ni wa mwaka mmoja, na kwa sasa mradi umekamilika na upo kwenye matazamio ya siku 180 mpaka 15.01.2025” alisema Mhandisi Sizinga.

Meneja wa RUWASA Mkoa wa Tanga, Mhandisi Lugongo alisema wamepokea timu ya Benki ya Dunia, ambapo walikwenda Tanga ili kuangalia utekelezaji wa miradi ya PforR, na waliwapeleka kwenye wilaya mbili za Pangani na Lushoto, na huko kote wameridhika kwa utekelezaji wa miradi hiyo ikiwemo kupeleka maji kwenye vyoo vya shule.