March 15, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Lukuvi alitaka Baraza Ofisi ya Waziri Mkuu kuelimisha watumishi wengine 

Na Zena Mohamed,Timesmajiraonline,Dodoma

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu,anayeshughulikia Sera,Bunge na Uratibu,Willium Lukuvi amelitaka Baraza la Wafanyakazi la Ofisi hiyo kuelewa kwa ufasaha mipango ya Wizara hiyo ili  kuelimisha watumishi wengine kuhusu mipango hiyo.

Lukuvi amesema hayo jijini hapa  leo,Machi 14,2025 wakati akifungua  Mkutano wa Baraza hilo wa kupitia makadirio ya mpango wa bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu ya mwaka wa fedha 2025/26.

Amesema kuwa hiyo ni moja ya jukumu kubwa na muhimu kwa Baraza la wafanyakazi hilo ni fursa pekee kwao kuwakilisha watumishi wengine katika kupanga muelekeo wa Ofisi hiyo kwa mwaka mwingine wa fedha .

“Hivyo mnawajibika pia kuelewa vyema bajeti kupitia Wizara jinsi mipango iliyowekwa katika kipindi cha mwaka wa fedha 2025/26 itakavyotekelezwa kwa kufuata sera na mikakati ya mipango hiyo. 

“Katika utekeleza wa mipango tuliyonayo tunaweza kuwa na changamoto zitakazojitokeza hata hivyo Baraza hili liwe mshiriki mkubwa kubuni mbinu mpya za utekelezaji na namna ya kukabiliana na changamoto zinazojitokeza na siyo kusubiri mtu mwingine aje kutatua changamoto hizo,”amesema Lukuvi.

Waziri Lukuvi amesema kuwa pamoja ya kwamba ni lazima watumishi washirikishwe mkutano huo ni ishara kubwa wa muongozo wa Ofisi ya Waziri Mkuu sera bunge na uratibu unadhamira ya dhati ya kuwashirikisha watumishi kwenye mipango ya Wizara.

“Kwa miaka yote serikali imekuwa ikisisitiza Wizara na Taasisi kujenga kutekeleza utaratibu wa kuwashirikisha watumishi kwenye mipango yake sababu ushirikishwaji watumishi kwenye mipango ya Wizara unaongeza umiliki wa mipango iliyowekwa unatusaidia kupata mawazo lakini unafanya watumishi wajione wanahusika moja kwa moja kuhakikisha mipango iliyowekwa inatekelezwa,”amesema Lukuvi.

Aidha amesema ni  wakati mzuri wa kuyapitia maeneo muhimu yaliyopewa kipaumbele katika mwaka wa fedha 2025/26 na kubaini mipango na mikakati mizuri zaidi katika kutekeleza vipaumbele hivyo.

Pamoja na hayo amelitaka Baraza hilo kutofanyakazi kwa kupokea malalamiko tu kutoka kwa wafanyakazi bali liwe chombo cha mazingira mazuri kitakachowafanya watumishi waweze kutimiza majukumu yao vizuri na kwa ukamilifu.

“Kama nilivyosema mara ya kwanza tunajua moja ya kazi kubwa ya Ofisi hii ni kumsaidia Waziri mkuu katika kutimiza jukumu lake kubwa na la msingi la kuratibu shughuli za serikali,hivyo 

Ofisi ya Waziri Mkuu lazima muwe mfano wa kutekeleza Ilani ya Chama Cha Mapinduzi kwa kuratibu shughuli kama hizo za kuratibu Ilani ya CCM katika ofisi ya Waziri Mkuu na Ofisi zingine za serikali,”amesema Waziri Lukuvi.

Amesema kuwa Ofisi hiyo inajukumu la kuunganisha kazi kubwa zinazofabywa na serikali na kuwaambia wananchi kwa uhakika.

“Katika uongozi wa Dkt.Samia tumepata mafanikio kwahiyo lazima mchukue jukumu lenu sasa la uratibu na  kuunganisha faida zilizopatikana chini wa utawala wa Rais Samia wananchi wazijue jinsi serikali yao inavyofanyakazi,”amesema Lukuvi.

Aidha amesema kuwa moja ya kazi ya kuratibu ni kuhakikisha kila Wizara inatekeleza jukumu lake vizuri hivyo wawahimize wale ambao bado hawajakamilisha miradi wamalize kwa wakati.

“Vilevile tumihize Idara na Wizara ziseme,hatuna manung’uniko tuelezee mafanikio yetu wananchi wayajue.

“Taarifa za utekelezaji katika maeneo yote tuhakikishe zinasikika kwa watanzania hii siyo tu kwajili ya uchaguzi bali wananchi wanahaki ya kusikia serikali yake imefanya nini na hasa tunajuvunia utekelezaji mzuri ambao wananchi wameona watashangaa sana kama sisi hatusemi wao wameo lakini sisi hatusemi,”amesema Lukuvi.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt.Jim Yonazi amesema mkutano huo umeshirikisha Baraza la wafanyakazi na wageni wengine akiwemo mwakilishi kutoka Baraza la wafanyakazi Ofisi ya Tughe ya Mkoa.

Ambapo kwa pamoja  wanajukumu  moja la kukaa kuangalia bajeti yao ambayo wataitumia mwaka unaofuata.

Amesema kuwa pamoja na ajenda nyingine ambazo zitajadiliwa lakini ajenda kubwa ni mpangilio wa mpango wa bajeti wa mwaka 2025/26.