January 9, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Lugangira:Tunapambania mitaa 28

Na Ashura Jumapili TimesMajira online Kagera ,

Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Kagera kupitia Chama Cha Mapinduzi ( CCM ), anayewakilisha kundi la asasi za kiraia Tanzania Bara Neema Lugangira, amesema kati ya mitaa 66 ya Bukoba Mjini 38 wagombea wake wameshapita.

Hivyo wanapambana na mitaa 28,ambapo amedai kuwa watashinda kwa kishindo katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajia kufanyika Novemba 27,2024.

Lugangira,amesema hayo Novemba 20,2024 wakati wa uzinduzi wa kampeni za Uchaguzi wa Serikali za Mitaa Mkoa wa Kagera kwa wagombea wa CCM,uliofanyika uwanja wa shule ya msingi Kashai, Halmashauri ya Manispaa ya Bukoba.

Amesema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan,anawadai wananchi wa Bukoba, kwa mambo mengi ya maendeleo ambayo ameyafanya ikiwemo ujenzi wa shule ya sekondari Samia Suluhu,kituo cha afya Kashai,zahanati ya Hamgembe,kibeta na hospitali ya Wilaya.

“Tutamlipa Rais,kwa ushindi wa kishindo kwa wagombea wa CCM wa mitaa 28 iliyobaki,sisi wanawake ni jeshi kubwa na tuna jambo letu tutatafuta kura nyumba kwa nyumba,kitanda kwa kitanda,uvungu kwa uvungu na shuka kwa shuka,”amesema Lugangira.

Naye Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa( MNEC)kutoka Kagera Karim Amri,amesema hawataki kichefuchefu ndani ya Kata ya Kashai wanataka ushindi wa asilimia 99.

Amri,amesema wakiharibu katika uchaguzi huu wa serikali za mitaa watampa wakati mgumu mgombea Udiwani wa Kata hiyo kwenye uchaguzi mkuu ujao.

Amesema Wananchi wa Kata ya kashai ndiyo mahakama ya Jimbo la Bukoba Mjini ndiyo wenye maamuzi ya ushindi kukiwezesha chama hicho kushinda kwa kishindo.

Hata hivyo amewataka wanachama wa CCM kuwa wamoja na mshikamano katika kipindi hiki cha uchaguzi wa serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika Novemba 27 mwaka huu.