January 9, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Lucy Lugome kuwainua kiuchumi wanawake Kisukuru

Na Heri Shaaban, TimesMajira Online

MGOMBEA udiwani wa kata ya Kisukuru Manispaa ya Ilala Lucy Lugome amewataka Wanawake wa Kata hiyo kujitokeza kwa wingi Oktoba 28 mwaka huu kumchagua na kumpa ushindi wa kishindo ili aweze kuwaletea maendeleo.

Lucy amayasema hayo wakati wa kumuombea kura mgombea wa nafasi ya Urais Dkt. John Magufuli na Ubunge wa Jimbo la Segerea kwa tiketi ya CCM, Bonah Ladslaus Kamoli.

“Wanawake wenzangu nawaomba mnichague Oktoba 28, 2020 ili niwe diwani wenu na niwaletee maendeleo pamoja na Mbunge wetu Bonah Kamoli lakini bila kumsahau Dkt. Magufuli ambaye amewezesha nchi yetu kufikia uchumi wa kati, ” amesema Lugombe.

Pia amewataka wanawake kujikwamua kiuchumi ili waweze kijishughulisha kwa sababu wanawake siku zote wanawaweza. na ameahidi kuwasimamia katika vikundi vya ujasiriamali na mikopo ya Serikali inayotolewa ngazi ya Halmashauri hivyo waandae katiba zao ili wasajili vikundi wale wasio sajili vikundi atashirikiana nao katika kuwasaidia uwandaaji wa Katiba.

Akielezea mikakati yake mingine Mgombea huyo amesema, Kata ya Kisukuru itakuwa ya kisasa kwa kusogeza huduma za jamii zote karibu na wananchi kwa kuwajengea vituo vya afya, soko, kituo cha Polisi na viwanja vya michezo .

Pia amewaahidi wafanyabishara wa Bodaboda kuwekewa utaratibu maalum ili watambulike kwa kusajiliwa na waendeshe biashara zao kwa kufuata sheria na taratibu za nchi.

Mgombea ubunge Viti Maalum Mkoa Dar es Salaam Janeth Masaburi amewataka wananchi kumpigia kura Dkt. John Magufuli, mgombea ubunge Bonah Ladslaus Kamoli na diwani Lucy Lugome ili waweze kuwaletewa maendeleo.

Amesema, Magufuli ni jembe, kiongozi anayesimamia maendeleo katika ukusanyaji mapato mpaka kuifikisha Tanzania hapa tulipo hivyo ili kumalizia kazi aliyoianza ni vema akapatiwa miaka mingine mitano.