May 22, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Bil. 24/- kuinua huduma ya maji Mtwara

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online, Mtwara

SERIKALI imetenga sh. bilioni 24 kwa ajili ya kazi ya ujenzi wa miradi ya maji katika vijiji 205, ikiwa ni hatua ya utekelezaji wa ahadi ya kumaliza tatizo la upatikanaji wa huduma ya maji kwa wakazi wa maeneo ya vijijini mkoani Mtwara, ambao kati yao asilimia 60.1 wanapata huduma hiyo.

Akizungumza na wataalamu wa Wizara ya Maji leo, Meneja wa Wakala wa Usambazaji Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Mkoa wa Mtwara, Mhandisi Mbaraka Ally amesema fedha hizo zimetengwa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi 31 itakayonufaisha wakazi zaidi ya 300,000.

Meneja huyo amekuwa na wataalamu hao ambao wako katika ufuatiliaji na kutathmini ujenzi wa miradi ya maji ya Kilidu Mnui na Mnolela Wilaya ya Newala.

“Kati ya sh. bilioni 24 zilizotengwa, tumeshapokea sh. bilioni nane na zimeanza kutumika kwenye ujenzi wa mradi wa maji wa Kilidu Mnui, ambao umeshakamilika kwa gharama ya zaidi ya sh. bilioni 1.4, ukiongeza lita 720,000 kwa siku na kuhudumia wanachi 60,000 wa Newala mjini na vijiji jirani.

“Changamoto iliyopo ni umeme ambapo tayari tumeshachukua hatua ya kubadilisha mita ya LUKU na baada ya muda mfupi mradi utaanza kutoa huduma,’’ amesema Mhandisi Ally.

“Vilevile mradi wa maji wa Mnonela umefikia asilimia 45 na utakamilika Desemba mwaka huu kwa gharama ya zaidi ya sh. milioni 400 na kuhudumia wakazi 2,805 wa vijiji vya Dodoma, Mkunjo, Mtanda na Mnonela katika Halmshauri ya Wilaya ya Newala inayopata huduma ya maji kwa asilimia 55”.

Amesema, wakazi 17,060 wa vijiji vya Lukuledi, Nasindi, Polapola, Kalinga na Napata wameanza kupata huduma ya maji safi na salama mara baada ya mradi wa maji wa Lukuledi kukamilika kwa asilimia 95 kwa kiasi cha zaidi ya sh. milioni 600 na kumaliza kilio cha muda mrefu.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Huduma ya Ubora wa Maji, Philipo Chandy ameipongeza Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Masasi-Nachingwea (MANAWASA), kwa kazi ya uboreshaji wa chanzo cha maji cha Mbwiji katika Halmashauri ya Wilaya ya Masasi.

Amesema, maendeleo ya ujenzi ni mazuri na utakapokamilika, utaimarisha zaidi huduma ya maji kwa wananchi waishio katika Wilaya za Masasi mkoani Mtwara, Nachingwea na Ruangwa Mkoa Lindi.