May 3, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

LSF yazindua mradi kuwezesha wanawake

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online, Arusha

SHIRIKA la Legal Services Facility (LSF) kwa kushirikiana na Taasisi ya North-South Cooperation kutoka nchini Luxembourg limezindua mradi wa miaka miwili 2023/24 utakaotambulika kama ‘Wanawake Tunaweza’.

Wanawake Tunaweza ni mradi utakaotekelezwa wilayani Longido mkoani Arusha kwa ajili ya uwezeshaji wa wanawake na jamii ya kimasai nchini katika nyanja ya kiuchumi na kijamii.

Mradi huu unalenga kuwezesha kiuchumi wanawake wa kimasai kwa kuwasaidia kuunda vikundi vya kiuchumi, kuwajengea uwezo katika masuala ya kibiashara na ujasiriamali, pamoja na kuwawezesha kupata soko la bidhaa mbalimbali watakazozizalisha.

Katika kuhakikisha kuwa jamii hususani wanawake na watoto wa kike wanawezeshwa, mradi huu wa ‘Wanawake Tunaweza’ utakwenda kusaidia kuboresha upatikanaji wa elimu kwa watoto wa kike kwa kuwajengea mabweni, kuunda klabu za wasichana shuleni, pamoja na utoaji wa taulo za kike shuleni kutoka katika vikundi vya wanawake vitakavyozalisha bidhaa hizo.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mradi huo Jijini Arusha, Mkurugenzi Mtendaji wa LSF, Lulu Ng’wanakilala amesema kuwa LSF imeamua kutekeleza mradi huu kwa kushirikiana na wadau wengine ili kusaidia jamii ya kimasai hususani wanawake na watoto wa kike, ambao wamekuwa nyuma katika hatua za maamuzi, umiliki wa rasilimali ikiwemo ardhi na mifugo, pamoja na fursa sawa ya kwenda shule.

“Jamii ya kimasai ni ya kipekee nchini Tanzania kutokana na udumishaji wa mila na desturi zake kwa kipindi kirefu. Uchumi wa jamii ya kimasai unategemea zaidi shughuli za ufugaji kwa asilimia 85 ya shughuli zote za kiuchumi zinazoendeshwa na jamii hii.

Njia kuu za uchumi pamoja na uzalishaji mali kwa jamii ya kimasai zinamilikiwa na kuendeshwa na wanaume, hali inayosababisha haki za wanawake na wasichana wa kimasai kukiukwa. Kuanzishwa mradi huu hapa Longido utawezesha kutatua baadhi ya changamoto hizi na kuwawezesha wanawake wa kimasai kijamii na kiuchumi,” ameeleza Lulu Ng’wanakilala.

Kwa upande wake Mgeni Rasmi, Hassan Ngoma ambaye amemwakilisha Katibu Tawala wa Wilaya ya Longido amewapongeza LSF pamoja na wadau wa maendeleo kutoka Luxemburg kwa kuona vyema na kuamua kushirikiana kutekeleza mradi huu..

Mgeni rasmi huyo ameongeza kwamba, ujenzi wa mabweni ya watoto wa kike katika shule za sekondari za Lekule na Namanga utawezesha kutatua changamoto ya watoto kubanana kwenye bweni moja na kuongeza idadi ya watoto wa shule shuleni na kuboresha mzingira ya utoaji wa elimu utakaochochea ufaulu wa wanafunzi kuongezeka.

Aidha, amesisitiza kuwa kuviongezea nguvu vikundi hivi vya kina mama kutawaongezea nguvu ya kupambana na shughuli za uzalishaji utakaowawezesha kuwainua kiuchumi, kutoa huduma bora na malezi kwa wototo na kukuza ustawi wa jamii nzima kwa ujumla.

Mradi mpya wa miaka miwili utakaofahamika kama ‘Wanawake Tunaweza’ ambao utatekelezwa Wilayani Longido Mkoani Arusha kwa ushirikiano kati ya LSF na Taasisi ya North-South Cooperation kutoka Luxembourg kwa ajili ya kuwezesha wanawake na wasichana kijamii na kiuchumi kwenye jamii ya kimasai umezinduliwa leo na Muwakilishi wa Katibu Tawala Wilaya ya Longido, Hassan Ngoma (mwenye kofia) pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa Legal Services Facility (LSF), Lulu Ng’wanakilala (wa pili kushoto) katika Shule ya Sekondari Namanga Longido.
Wanafunzi wa kike kutoka Shule ya Sekondari Namanga ambao watanufaika na ujenzi wa bweni kupitia mradi wa ‘Wanawake Tunaweza’ wakiwa katika picha ya pamoja na wageni wa meza kuu mara baada ya uzinduzi wa mradi huo. Pamoja na mambo mengine, mradi huu utasaidia kuboresha upatikanaji wa elimu kwa watoto wa kike, kuunda klabu za wasichana shuleni pamoja na kutoa taulo za kike shuleni.
Wanafunzi wa Shule ya Sekondari Namanga iliyopo wilayani Longido Mkoani Arusha wakitoa burudani katika shuguli ya uzinduzi wa mradi wa ‘Wanawake Tunaweza’ ambao umezinduliwa leo, ambapo mradi unatarajiwa kuwanufaisha moja kwa moja wanawake 209 na wasichana 1,214 kupitia shughuli za utoaji elimu.
Wanawake na wasichana kutoka jamii ya kimasai wakiwa kwenye picha ya pamoja na wageni wa meza kuu mara baada ya uzinduzi wa mradi wa ‘Wanawake Tunaweza’ uliofanyika leo wilayani Longido Mkoani Arusha.