Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online, Dar es Salaam
SHIRIKA la Legal Services Facility (LSF) limesaini mkataba wa kupokea ruzuku kiasi cha shilingi za kitanzania bilioni 5.6 (sawa na dola za Kimarekani milioni 2.4) kutoka Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Denmark (DANIDA) kwa ajili ya kutekeleza mradi wa upatikanaji wa haki nchini kwa kipindi cha mwaka mmoja kati ya Januari na Desemba, 2021.
LSF imepokea ruzuku hiyo ikiwa ni nyongeza kwa ajili ya kutekeleza mradi wa upatikanaji wa haki unaolenga kuboresha mazingira ya uwezeshaji wa kisheria nchini kwa kuzijengea uwezo taasisi zinazotoa huduma ya msaada wa kisheria pamoja na huduma za wasaidizi wa kisheria nchini kwa makundi mbalimbali katika jamii hususani wanawake na watoto.
Aidha, mradi huo unalenga kujenga msingi endelevu wa huduma za msaada wa kisheria nchini Tanzania kwa kupitia upya mifumo, sera na sheria mbalimbali kandamizi zinazorudisha nyuma ustawi na maendeleo ya wanawake na watoto katika jamii kwa lengo la kuboresha mifumo ya upatikanaji wa haki nchini katika ngazi mbalimbali.
Mradi huo unafanyika nchini Tanzania ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa malengo mawili endelevu ikiwemo lengo namba tano (SDG5) na namba 16 (SDG16), ambayo yanaangazia masuala ya usawa wa kijinsia na uwezeshwaji wa wanawake pamoja na kukuza upatikanaji wa haki kwa watu wote.
Kadhalika, mradi huo ni sehemu ya utekelezaji wa dira ya maendeleo nchini Tanzania ifikapo mwaka 2025, ambayo inatambua umuhimu wa masuala ya usawa kama njia ya kujenga msingi wa amani na utawala bora, ambayo vyote vinachangia kwa kiasi kikubwa katika kufikia mifumo endelevu ya upatikanaji wa haki nchini.
Akizungumza wakati wa hafla ya kutiliana saini, Balozi wa Denmark nchini Tanzania, Mette Norgaard Dissing-Spandet alisema kuwa, DANIDA imeamua kuwaongezea ruzuku LSF kwa kipindi cha mwaka mmoja ikiwa ni sehemu yake ya uwajibikaji katika kuhakikisha suala la upatikanaji wa haki nchini Tanzania linazingatiwa.
ìLSF ni mdau wetu mkubwa kwa takribani miaka 10 sasa, ambapo amekuwa akifanya kazi kubwa nchini Tanzania. Tumeamua kuongeza kiwango hiki cha ruzuku ili kusaidia zaidi utekelezaji wa mradi unaotekelezwa na LSF kwa ajili ya maendeleo ya kina mama na Watoto ambao ndio wahanga wakubwa wa maswala ya haki zao.
Aidha, tunaamini ruzuku hii itasadia katika kuboresha mifumo ya utoaji haki iliyo rasmi na isiyo rasmi ili kuwezesha upatikanaji wa haki kwa wakati;
ìLakini pia kuwezesha upatikaji wa sera na sheria bora zinazolinda maslahi ya watanzania wote hususani wanawake na watoto. Ufadhili huu ni sehemu yetu katika kuhakikisha kuwa jamii yote nchini Tanzania inakuwa na utawala wa sheria unaoheshimu kila mtu bila kujali umri au jinsia,îalisema Balozi huyo.
Kwa upande wake, Afisa Mtendaji Mkuu wa Legal Services Facility, Lulu NgÃwanakilala alisema kuwa, ruzuku iliyotolewa na wadau wake hao itasaidia kikamilifu katika kuendelea kutekeleza mradi wa upatikanaji wa haki nchini unaotekelezwa nchi nzima kwa upande wa Tanzania bara na visiwani Zanzibar.
Aidha, ikumbukwe kwamba mienzi sita iliyopita DANIDA walitoa ruzuku kwa LSF ya kiasi cha shillingi milioni 719,500,000 (zaidi ya dola za Kimarekani 311,471.86) ili kuwezesha elimu ya mpiga kura na usimamizi wa uchaguzi kwa mashirika 31 yaliyopewa vibali na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kuendesha shughuli hizo za uchaguzi.
NgÃwanakilala aliongeza kwa kusema kuwa, katika kipindi cha miaka mitano iliyopita LSF imekuwa ikishirikiana na wadau wake mbalimbali ikiwemo DANIDA, ambapo imeweza kusaidia kuboresha sekta ya msaada wa kisheria nchini kupitia uwezeshaji wa kisheria kwa kuyapa ruzuku mashirika zaidi ya 200 yanayotoa huduma za msaada wa kisheria pamoja na huduma za watetezi wa kisheria nchini kote.
ìUfadhili huu utaendelea kuwezesha upatikanaji wa huduma za msaada wa kisheria bure katika kila wilaya zote Tanzania bara na Zanzibar kupitia wasaidizi wa msaada wakisheria zaidi ya 4000 nchi nzima. Hivyo Tunawashukuru sana wadau wetu DANIDA kwa kuendelea kutusaidia katika utekelezaji mradi wetu wa upatikanaji wa haki nchi nzima.
Kwa takribani miaka 10 sasa DANIDA wamekuwa na mchango mkubwa katika kuhakikisha mradi wetu huu unawanufaisha wananchi wengi nchini hususani wanawake na watoto.
ìMwaka 2020, tumeweza kuwapatia msaada wa kisheria watu takribani 99,844, ambapo wanaume pekee walikuwa 39,641 sawa na asilimia 40, huku wanawake wakiwa ni 60,203 sawa na asilimia 60. Mashauri yanayofikishwa kwa wasaidizi wa kisheria ni pamoja na migogoro ya ardhi, ndoa, mirathi, matunzo kwa Watoto, pamoja na vitendo vya ukatili wa kijisia. Kati ya mashauri yaliyorepotiwa kwa wasaidizi wa kisheria asilimia 66 yalitatuliwa,îalieleza NgÃwanakilala.
More Stories
TARURA Kilimanjaro yatimiza ahadi ya Rais Samia
DCEA,Vyombo vya Ulinzi na Usalama vyafanya operesheni ya kihistoria
Wananchi wakubali yaishe Bangi kubaki historia Tarime